Ijumaa, 29 Novemba 2024

IJA YAANZISHA KURUGENZI YA MAFUNZO YA KIMAHAKAMA, ELIMU ENDELEVU

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Lushoto

Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kimeanza kutumia muundo mpya ambao umeanzisha Kurugenzi ya Mafunzo ya Kimahakama na Elimu Endelevu (Directorate of Judicial Training and Continuing Education) ili kuhakikisha kinatekeleza kwa ufanisi majukumu yake ya msingi ya kuanzishwa kwake.

Hayo yamebainishwa leo tarehe 29 Novemba, 2024 na Mkuu wa Chuo cha IJA na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo alipokuwa anazungumza kwenye Mahafali ya 24 ya Chuo cha Mahakama Lushoto ambayo pia yamehudhuriwa na Wajumbe wa Baraza la Uongozi wa Chuo, Viongozi wa Mahakama na Viongozi wengine wa Serikali na Dini mbalimbali.

“Jukumu kubwa la Kurungezi hii ni kuratibu mafunzo ya kimahakama kwa maafisa wa Mahakama na mafunzo endelevu kwa watumishi wengine wa Mahakama pamoja na wadau wote wa sekta ya sheria nchini. Hii ni hatua kubwa katika kuimarisha utoaji wa mafunzo ya kimahakama,” Mhe. Kihwelo amesema.

Amemweleza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafali hayo kuwa mwezi Novemba, 2023, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha mabadiliiko ya sheria iliyoanzisha Chuo ambapo, pamoja na mambo mengine, Mafunzo ya Kimahakama na Elimu Endelevu yametambulika rasmi kisheria kama ni jukumu mojawapo la msingi la Chuo.

Mkuu wa Chuo amebainisha pia kuwa kupitia mabadiliko hapo, madaraka ya Jaji Mkuu yameongezwa,  ikiwemo kuteua wajumbe wa Baraza la Uongozi wa Chuo na kutoa maelekezo mahsusi au maelekezo ya jumla kwa Baraza tofauti na ilivyokuwa awali, huku Baraza la Uongozi wa Chuo likipewa mamlaka ya kupitisha kanuni mbalimbali za Chuo kwa idhini ya Waziri wa Katiba na Sheria.

“Mabadiliko haya yameongeza wigo wa maendeleo ya Chuo, kwani yamekisogeza karibu na Mhimili ambao unakitumikia kama wakala wa mafunzo na utafiti na hivyo kurahisisha utendaji kazi pamoja na kuwa bado kuna mambo mengi ya kisheria na kimuundo yanayohitaji kufanyiwa kazi,” amesema.

Mhe. Dkt. Kihwelo amebainisha kuwa Chuo kimeendelea na dhima yake ya kutoa mafunzo ya kimahakama, mafunzo elekezi pamoja na mafunzo endelevu kwa wadau wa sekta ya sheria nchini.

Kwa mfano, amesema, katika kipindi cha pili cha mwaka wa fedha 2023/2024, Chuo kimetoa mafunzo kwa maafisa, watumishi wa Mahakama na wadau wengine kwenye maeneo mbalimbali, ikiwemo kuandaa makongamano ya kikanda na kimataifa kwa nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Msumbiji, Malawi, Zimbabwe, Zambia, Afrika ya Kusini, Zambia, Botswana, Namibia, Ghana, Gambia, Nigeria na Mali.

“Naomba kipekee nitoa shukrani kwako wewe binafsi, Jaji Kiongozi, Mtendaji Mkuu wa Mahakama na Msajili Mkuu kwa ushirikiano mkubwa mnaotupatia kama Chuo. Vile vile, niwashukuru pia wadau wetu wakiwemo Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii na wengine wengi kwa kutoa vibali vya washiriki kila tunapowaomba,” amesema.

Akizungumzia upande wa mageuzi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Mkuu wa Chuo amesema kuwa IJA, kwa kuwezeshwa na Mahakama ya Tanzania, imeendelea kujizatiti katika matumizi ya TEHAMA katika kutoa mafunzo na imejenga mfumo wa jukwaa la kufundishia mtandaoni (E-learning Platform), kupitia Mradi wa Maboresho unaofadhiliwa kwa mkopo wa Benki ya Dunia.

“Hatua hiyo imeenda sambamba na usanifu wa jengo la studio ya kisasa ya kufundishia ambao ujenzi wake ulikamilika na mkandarasi alishalikabidhi. Hatua iliyosalia ni ya kuweka vifaa vya TEHAMA ikiwemo mitambo ya kurekodia maudhui ya kufundishia pamoja na kupakua katika mtandao ili mafunzo yaweze kuanza rasmi, Mhe. Dkt. Kihwelo amesema.

Tayari mafunzo ya jinsi ya kuandaa na kuingiza maudhui katika jukwaa hilo yameshatolewa kwa baadhi ya Watumishi wa Mahakama pamoja na wahadhiri wa Chuo. Hatua hiyo itakiwezesha Chuo kutoa mafunzo ya kozi fupi pamoja na kozi ndefu kwa kutumia elimu masafa na elimu mtandao na hivyo kuwafikia watu wengi zaidi wenye uhitaji.

Mkuu wa Chuo amemweleza Jaji Mkuu kuwa ujenzi wa jukwaa hilo pamoja na studio hizo za kufundishia mtandaoni ni maono yake katika kiu ya kuona kuwa Mahakama ya Tanzania inajikita katika TEHAMA ili kuendesha shughuli zake ikiwemo kutoa mafunzo kwa njia ya mtandao.

“Kipekee tunaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufadhili ujenzi wa jukwaa hilo kupitia mkopo wa Benki ya Dunia katika awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi wa Maboresho ya Mahakama ya Tanzania. Tunatambua tu kuwa ujenzi wa jukwaa hilo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama wa mwaka 2020/21-2024/25 na pia ni utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Kuelekea Tanzania ya Kidigiti, ambavyo kwa pamoja vinachagizwa na Mradi wa Kidigiti wa Taifa..

“Tunashukuru sana Uongozi wa Mahakama chini yako Mgeni rasmi, lakini pia Mkuu wa Kitengo cha Maboresho na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Angelo Rumishi, Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama na Endelevu, Mhe. Dkt. Patricia Kisinda, Mkurugenzi wa Raslimaliwatu na Utawala, Bi. Beatrice Patrick na Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo, Bi. Patricia Ngungulu kwa kusimamia zoezi hili na kuhakikisha kuwa linakamilika tena kwa ubora,” amesema.

Amebainisha pia kuwa katika kuhakikisha kuwa Chuo kinafikia malengo yake zaidi na kukua kimataifa kama kinavyotakiwa na Sheria inayokianzisha, IJA imeendelea kuimarisha uhusiano na wadau wake wa ndani na nje ya nchi na kuanzisha mahusiano mapya na kuimarisha mashirikiano na taasisi ambazo tayari imekuwa na mashirikiano nazo.

Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo (juu na chini) akizungumza wakati wa Mahafali ya 24 ya Chuo cha Ungozi wa Mahakama Lushoto leo tarehe 29 Novemba, 2024.


Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (juu na chini) ikifuatilia kwa karibu hotuba ya Mkuu wa Chuo (hayupo kwenye picha).

Wahadhili wa  Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto wakifuatilia kilichokuwa kinajiri wakati wa mahafali hayo. Picha chini ni wageni mbalimbali walioalikwa kwenye sherehe hiyo.




 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni