- Ataka mwelekeo mpya ufundishaji, kuongeza mapato
Na FAUSTINE
KAPAMA-Mahakama, Lushoto
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameliagiza Baraza la Uongozi la Chuo cha Uongozi
wa Mahakama Lushoto (IJA) kujitathmini na kubadili mwelekeo wa ufundishaji ili
kupanua wigo na vyanzo vya mapato.
Mhe. Prof. Juma ametoa
rai hiyo leo tarehe 29 Novemba, 2024 wilayani hapa katika Mahafali ya 24 ya
Chuo cha Mahakama Lushoto ambayo pia yamehudhuriwa na Wajumbe wa Baraza la Ugonzi
wa Chuo, Viongozi wa Mahakama na Viongozi wengine wa Serikali na Dini
mbalimbali.
“Sheria iliyounda Chuo
inaruhusu kufundisha, kutafiti na huduma za ushauri, ni vyema mkatafuta wadau
wengine nje ya Mahakama kwa ajili ya kuwapa huduma kwa kuwafuata na pia
kuwaleta Lushoto. Fanyeni tathmini ya uhalisia wa gharama zenu ili kujiridhisha
kuhusu faida,” amesema.
Jaji Mkuu ametumia nafasi
hiyo kuupongeza uongozi wa Chuo kwa kuhakikisha kuwa, mafunzo yanayotolewa IJA
yanazingatia mabadiliko makubwa katika matumizi ya teknolojia, hususan
Artificial Intelligence (Akili Mnemba).
Mhe. Prof. Juma amefarijika
pia kusikia kwamba maandalizi ya jukwaa la kujifunzia ki-elektroniki
(e-Learning Platform) yamekamilika na kuwa ujenzi wa studio ya kisasa
umekamilika kwa asilimia 95, huku mafunzo ya kuandaa, kutengeneza na kutumia
maudhui ya kwenye mtandao kwa ajili ya kufundishia na kujifunzia pia yakiwa
yamefanyika.
“Hili ni jambo la faraja
kwangu kwani uwepo wa jukwaa hilo la kufundishia kwa njia ya kidigitali ni
ukombozi mkubwa kwa Chuo na Mahakama katika utoaji mafunzo kwa watumishi wa
Mahakama na wadau kwa ujumla,” amesema.
Kufuatia uwepo wa faida
nyingi za kujengwa kwa jukwaa hilo, Jaji Mkuu amekitaka Chuo kuwa imaginative,
innovative ili kuvuna faida nyingi zaidi.
“Kwa mfano, sioni
kinachoweza kuizuia Chuo kisitumie mfumo huu kutoa mafunzo kwa vitendo juu ya
matumizi ya Kanuni inayoratibu ufunguaji wa mashauri kwa njia
ya mtandao. Chuo cha Uongozi wa Mahakama kinaweza kutumia e-Learning Platform
kutoa mafunzo kwa vitendo kuhusu matumizi ya mifumo ya video conference,”
amesema.
Aidha, Jaji Mkuu amesema
kuwa Chuo cha Uongozi wa Mahakama kina nafasi muhimu ya kushirikiana na Jeshi
la Polisi na Mahakama ya Tanzania kutumia jukwaa hilo kuwafundisha Polisi namna
kutekeleza Kanuni zilizotungwa zinazowawezesha kurekodi kwa njia ya video
mahojiano baina yao na watuhumiwa, hivyo kupunguza malalamiko ya kubambikiwa
kesi za jinai.
“Tayari zipo kanuni
zinazowataka polisi waache kutegemea maelezo ya onyo wanayoaandika na badala
yake warekodi kwa njia ya sauti na video mahojiano hayo,” amesema.
Vile vile, Mhe. Prof.
Juma amewakumbusha Wahadhiri na watumishi wote wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama
Lushoto kuwa dirisha la kuhama kutoka matumizi ya analojia hadi matumizi ya
kidijitali linazidi kuwa dogo na kwamba Sera ya TEHAMA ya Mahakama ya Tanzania
ni kufikia huduma zote zitolewe kwa njia za kidijitali.
“Watumishi wote wa Chuo
cha Uongozi wa Mahakama, wakiwemo Wahadhiri na Wanafunzi, hawana nafasi ya
kubaki katika mifumo ya analojia wakati Mahakama ya Tanzania, Bunge na Serikali
ya Tanzania wanaimba lugha ya Tanzania ya kidijitali. Huu sio wakati tena wa
Wahadhiri wa Chuo cha Lushoto kutoa mafunzo kwa njia za analojia,” amesema.
Kuonyesha kuwa mwelekeo
sasa hivi ni Tanzania ya Kidijitali, Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa, hivi
karibuni alitangaza kuwa Baraza la Mawaziri linahamia katika matumizi ya mfumo
wa kielektroniki (e-Cabinet) na kwamba matumizi ya eCabinet yataboresha
utendaji kazi na kuleta ufanisi zaidi katika kuwahudumia wananchi.
Hivyo, Jaji Mkuu
amemwomba Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo na Baraza lake, kutunga Sera
ambayo itawataka Wahadhiri na watumishi IJA, ndani ya muda mfupi kadri
inavyowezekana, watumie mifumo ya kidijitali kufundisha, kusoma na kutoa huduma.
Amesema kuwa kukamilika
kwa jukwaa kujifunzia la ki-elektroniki ni dalili ya wazi kuwa mifumo ya
kidijitali ndio jibu la kurahisisha utoaji wa mafunzo na elimu kwa wanachuo
watakao kuwa huoni na wale watakaopta mafunzo yao wakiwa nje ya Lushoto.
Hivyo, Mhe. Prof. Juma
ametoa wito pia kwa Uongozi wa Chuo kutumia faida ya maboresho kwa kuongeza
thamani ya mafunzo yanayotolewa na Chuo, kwa kushirikiana na vyuo vingine ndani
na nje ya Tanzania ili kuweza kutoa mafunzo ya aina mbalimbali kwa kutumia
jukwaa kujifunzia la kielektoniki.
Meza Kuu inayoongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Wahitimu Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (juu na picha mbili chini).
Mwonekano kwa nje wa studio ya kisasa ambayo imejengwa katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati picha ya juu na wa kwanza kushoto picha chini) akiwa ndani ya studio hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni