Jumamosi, 30 Novemba 2024

MAHAKIMU KUTOKA MSUMBIJI WATEMBELEA KITUO JUMUISHI CHA MASUALA YA FAMILIA TEMEKE

Mahakimu wa Temeke na Msumbiji wabadilishana uzoefu wa utendaji kazi

Na NAOMI KITONKA, Mahakama-Temeke

Kuelekea maadhimisho ya kilele cha maadhimisho ya miaka mitatu tangu kuanzishwa kwa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia (OSC Temeke), Kituo hicho kimepokea wageni ambao ni Mahakimu kutoka Mahakama ya Msumbiji ikiwa ni ziara fupi ya mafunzo ya kubadilishana uzoefu.

Wageni hao waliwasili katika Mahakama hiyo tarehe 28 Novemba 2024 wakiongozwa na Naibu Wasajili wa Mahakama Kuu OSC Temeke, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mhe. Kiswaga, pamoja na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya OSC Temeke, Mhe. John Msafiri.

Wageni hao walipata nafasi ya kuzunguka maeneo mbalimbali ya jengo la Mahakama yakiwemo vyumba vya kusikilizia mashauri na chumba cha kunyonyeshea watoto na kujionea shughuli mbalimbali za utoaji huduma kutoka ofisi za wadau mbalimbali wanaopatikana zikiwemo ofisi za msaada wa kisheria na ofisi za ustawi wa jamii. 

Vile vile, wageni hao walipata fursa ya kupewa elimu kuhusu mada zilizowasilishwa kutoka kwa Mhe. John Msafiri na Mhe. Orupa Mtae ambaye ni Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Watoto.  

“Katika Kituo chetu, mashauri yote ya ndoa yanayosikilizwa yanazingatia kanuni, taratibu na sheria zake kulingana na aina ya ndoa huku mgawanyo wa mali kwa wanandoa pia ukifanywa kwa makini ili kutoa haki kwa wakati na pande zote husikilizwa na kupewa ruhusa ya kukata rufaa pale wasiporidhika na uamuzi,” alisema Mhe. Msafiri wakati akitoa wasilisho kwa Mahakimu kutoka Msumbiji.

Mhe. Msafiri alizungumzia pia maendeleo makubwa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika uendeshwaji wa shughuli za Mahakama, ambapo  alisema, “tunao mfumo wa kusajili wateja wetu wote wanaokuja kupata huduma mahakamani pamoja na mfumo wa matangazo katika jengo zima unaomruhusu mteja kusikia kesi yake inapoitwa akiwa sehemu yoyote katika jengo la Mahakama na pia mfumo wa kusajili unatusaidia kama Kituo kujua takwimu zitakazotusaidia kufanya maboresho mbalimbali ya huduma zetu za utoaji haki kwa ubora na kwa haraka.”

Aliongeza kuwa, Mahakama ya Tanzania inatumia pia Mfumo katika uendeshaji wa mashauri wa Usimamizi na Uratibu wa Mashauri (e-CMS) ambapo mteja anaweza kufungua shauri lake kwa njia ya mtandao, kujua shauri lake limepangwa lini na pia kuona mwenendo wa kesi nzima inayotengenezwa kwa Mfumo wa Unukuzi na Tafsiri (TTS) pamoja na hukumu za kesi pasipo kufika Mahakamani au kuhudhuria kwa njia ya mtandao mashauri (Video conferencing).

Akiongezea katika wasilisho hilo, Mhe. Orupa Mtae alizungumzia jinsi Mahakama ya Watoto inavyofanya kazi pamoja na vipaumbele vyake katika utoaji haki kwa haraka zaidi.

“Sisi kama Mahakama ya Watoto wajibu wetu mkubwa ni kuhakikisha suala la upatikanaji haki kwa watoto linafanyika kwa ufanisi ikiwemo pia kuwasaidia wazazi pale wanapohitaji haki ya malezi na matunzo ya watoto baada ya ndoa kuvunjika,” alisema Mhe. Orupa.

Wageni hao walipata nafasi pia ya kujifunza kwa vitendo namna mashauri yanavyoendeshwa kupitia Mfumo wa Unukuzi na Tafsiri (TTS) baada ya kuhudhuria shauri la Mirathi katika moja ya Mahakama ya wazi katika kituo hicho lililoendeshwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya, Mhe. Manfred Sanga.

Aidha wageni hao, walipata nafasi ya kuuliza maswali na walishangazwa na utofauti wa ugawaji mali baada ya ndoa kuvunjika na pia mwekezaji ambaye anamiliki miradi ambao kwa upande wa nchi ya Tanzania ni tofauti na Msumbiji hasa pale ambapo mwekezaji atafariki na mali zinabaki chini ya Serikali hasa ardhi.

Ziara hiyo ilifungwa kwa kushiriki chakula na kupata picha ya pamoja baina ya pande mbili. 

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Temeke, Mhe. John Msafiri (aliyesimama) akitoa wasilisho kwa Mahakimu kutoka nchini Msumbiji waliofika Kituoni hapo tarehe 28 Novemba 2024. 

Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Watoto katika Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Orupa Mtae (aliyesimama) akitoa wasilisho kwa Mahakimu kutoka nchini Msumbiji iliyofanyika jana tarehe 28 Novemba, 2024 kituoni hapo.

Mahakimu kutoka Mahakama ya Msumbiji wakisikiliza kwa makini wasilisho kutoka kwa Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Watoto, Mhe. Orupa Mtae (hayupo katika picha) alipokuwa akiwasilisha mada kwa Mahakimu kutoka Mahakama ya Msumbiji walipofanya ziara katika Mahakama hiyo tarehe 28 Novemba, 2024. 

Mahakimu kutoka Mahakama ya Msumbiji pamoja na wateja wa mashauri ya mirathi (hawapo katika picha) wakimsikiliza kwa makini Afisa TEHAMA wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke, Bw. Fredrick Ponceous alipokuwa akitoa maelezo ya Mfumo wa Unukuzi na Tafsiri (TTS).


 Mahakimu kutoka Mahakama ya Msumbiji pamoja na wateja wa mashauri ya mirathi wakimsikiliza kwa makini Afisa TEHAMA wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Bw. Fredrick Ponceous (hayupo katika picha) alipokuwa akitoa maelezo kuhusu Mfumo wa Unukuzi na Tafsiri (TTS) katika moja ya ukumbi wa Mahakama ya Wazi unaotumika kituoni hapo.

Mahakimu kutoka Mahakama ya Msumbiji wakimsikiliza kwa makini Jaji Mfawidhi wa Mahakama Ya Kituo Jumuishi Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa (aliyeketi mbele) akizungumza jambo na wageni hao walipomtembelea ofisini kwake wakati wa ziara yao iliyofanyika tarehe 28 Novemba 2024 Kituoni hapo. 


Mahakimu Kutoka nchini Msumbiji wakiwa katika picha ya pamoja   baada ya kumaliza kufanya ziara yao ya Mafunzo katika Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke. 

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Arusha)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni