Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Lushoto
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewasihi Wadau wa Mahakama kuwa makini na kauli
wanazozitoa zinazolenga kubeza mfumo mzima wa utoaji haki nchini.
Mhe. Prof. Juma ametoa
wito huo leo tarehe 30 Novemba, 2024 katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama
Lushoto kwenye hafla ya uapisho na ufunguzi wa mafunzo elekezi kwa Mahakimu 88
wapya.
“Wito wangu kwa wadau
wetu ni kwamba watofautishe kukosoa na kubeza. Mahakama tuko tayari kukosolewa
ila hatuko tayari kubezwa kwa lengo tu la kuchafua taswira ya Taasisi yetu na
kuwakatisha tamaa Majaji na Mahakimu ambao wanafanya kazi muhimu sana kwa maendeleo
ya Taifa letu,” amesema.
Jaji Mkuu amerejea ‘video
clip’ iliyosambazwa mitandaoni hivi karibuni ikimnukuu Mwananchi mmoja akieleza
kuwa hukumu zinazotolewa siku hizi na kuchapishwa kwenye mtandao wa Mahakama,
TanzLII, hazina kitu chochote, huku akidai pia kuwa Mahakama ya Rufani ina
Majaji ‘Spoilers” na Majaji wa Serikali.
Hata hivyo, Jaji Mkuu
anasema wapo Wananchi wengine ambao wana maoni tofauti na wamejitokeza kuweka
wazi kuwa, wameona maamuzi ya Mahakama ya Tanzania yamewasaidia kwa vitendo
katika kuboresha huduma za utoaji haki na kufanya tafiti mbalimbali.
“Kwa mfano, msongamano
katika magereza unagusa haki kadhaa za binadamu. Majaji na Mahakimu huona kazi
zao zinathaminiwa na zina faida kubwa zaidi ya maamuzi yaliyokusanywa na
Mwananchi huyu mwaka 1997 (miaka 27 iliyopita),” amesema.
Mhe. Prof. Juma ameeleza
kuwa wiki chache zilizopita alitembelewa ofisini kwake na Kamishna Jenerali wa
Magereza, Jeremiah Yoram Katungu na yeye kwa uzoefu wake wa hali ya sasa
akilinganisha na zamani alisema uwezo wao wa kuhifadhi Wafungwa na Mahabusu ni
29,90,2 lakini kutokana na ufanisi wa Mahakama kuendesha mashauri kwa
teknolojia kwa sasa wana Mahabusu 27,000 tu na akaipongeza Mahakama kwa
maboresho hayo.
Jaji Mkuu amebainisha pia
kuwa amebaini kuwa hata yule Mwananchi aliyekuwa analalamikia ubora wa hukumu
za Mahakama bado ametupa fursa nzuri ya kujua nini cha kuelimisha jamii. Kwa
hiyo, amesema Mahakama lazima iongeze mawasiliano na Umma ili kujitangaza na
kueleweke na wananchi, kwa wale ambao wako tayari kuelewa.
Mhe. Prof. Juma amesema
kazi ya Jaji au Hakimu ni kutoa maamuzi au hukumu ambayo hutatua mgogoro baina
ya walioleta mgogoro wao mahakamani, hivyo suala la kupenda au kutopenda uamuzi
ni utashi wa anayeguswa na hukumu au msomaji.
“Kwa mantiki hii, hata
mtu mmoja kuona kuwa hukumu ni bora au sio bora inategemea anaangalia kwa jicho
lipi, kwa lengo lipi na kwa hisia gani na hii husababisha kuwa na mwelekeo wa
kutathmini kwa namna tu ya kudhania (subjectively) kwa jinsi yeye anavyodhania,”
amesema.
Hivyo ametoa wito kwa
Watanzania kuwa waungwana kukiri kwamba, zama za kukusanya maamuzi na
kuchapisha vitabu vyenye maamuzi ya Majaji zimepitwa na Mapinduzi ya Teknolojia
na kwamba kupandishwa maamuzi yote na kupatikana kwa urahisi kupitia mtandao wa
TANZLII ni matunda ya maboresho yanayoendelea.
“Huu mfumo wetu wa
TANZLII unasifiwa duniani na unatembelewa kuliko mifumo mingine yote duniani.
Mahakama ya Tanzania, kwa kushirikiana na AfricanLII na Laws Africa,
wameanzisha Sheria Mkononi kusaidia kupatikana kwa hukumu hata bila kuwa na
mtandao. Watanzania tujivunie cha kwetu na kama kuna hoja za kuboresha, basi
tufanye hivyo kwa kutumia njia sahihi baada ya kuwa na ushahidi wa kisayansi
usiotiliwa shaka,” amesema.
Akizungumzia suala la
Majaji Spoilers au Majaji wa Serikali, Jaji Mkuu amekiri hii ni mara ya kwanza
kwake kusikia kutoka kwa yule Mwananchi mtaalamu wa sheria kwamba Mahakama ya
Rufani, katika upangaji wa Majopo, na katika kufikia maamuzi, kulikuwa na Jaji
mmoja mahsusi wa Serikali mwenye kazi moja tu, ya kuharibu (spoiler).
“Kwa bahati nzuri bado
wapo Majaji wa Rufani wastaafu, kwa mfano Jaji Januari Msoffe na Jaji Edward
Rutakangwa, ambao walihudumu kama Wasajili zamani hizo, ambao wanaweza kutoa
mwanga zaidi…
“Nimgependa pia
kumjulisha yule Mwananchi aliyekuwa analalamika kuwa ubora wa hukumu za
Mahakama unaharibiwa na “spoilers” kuwa hakujawahi kuwa na hao “spoilers,” na
Mahakama ya Tanzania ina Majaji wa Mahakama Kuu na Majaji wa Mahakama ya
Rufani. Hakuna Majaji wa Serikali,” Jaji Mkuu amesema.
Hivyo, amewaomba Majaji
na Mahakimu kutokatishwa tamaa na kauli hasi, au kejeli watakazokutana nazo,
bali watumikie Watanzania kwa misingi ya uwazi, uweledi na maadili mema bila
upendeleo katika utoaji haki.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni