Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 27 Novemba, 2024 ameungana na Watanzania kushiriki kwenye zoezi la kupiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaofanyika kote nchini.
Akiwa ameongozana na mke wake, Mama Marina Juma, Mhe. Prof. Juma aliwasili kwenye kituo cha kupigia kura kilichopo katika Shule ya Msingi Oystebay Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam majira ya saa 8.55 asubuhi kwa ajili ya kushiriki zoezi hilo.
Baada ya kupokelewa na Viongozi waliokuwa wanaratibu zoezi hilo, Jaji Mkuu alienda moja kwa moja kwenye kituo alichokuwa amejiandikisha na kukagua majina yake kabla ya kuingia kwenye chumba maalum kilichokuwa kimeandaliwa kwa ajili ya upigaji kura.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unawapa uwezo wananchi wa Tanzania kuchagua wenyeviti wa vijiji, mitaa na vitongoji pamoja na wajumbe wa halmashauri. Kadhalika, unnalenga kuimarisha uwakilishi na kuzipa jumuiya za wananchi uwezo mkubwa wa kufanya maamuzi katika maeneo kama vile matumizi ya ardhi, miradi ya jamii na utoaji wa huduma.
Uchaguzi wa mwaka 2024 ni muhimu hasa kwa kuzingatia mageuzi ya kidemokrasia yanayoendelea chini ya utawala wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Serikali imesisitiza kuwa mageuzi hayo yanalenga kuboresha uwazi na uaminifu katika mchakato wa uchaguzi.
Tanzania imekuwa ikifanya uchaguzi wa serikali za mitaa kila baada ya miaka mitano tangu miaka ya 1980, kufuatia mageuzi ambayo yalianzisha muundo wa utawala wa madaraka. Chaguzi hizo ni sehemu muhimu ya juhudi za Tanzania kuwezesha jamii na kuimarisha ushiriki wa umma katika kufanya maamuzi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni