Na Innocent Kansha- Mahakama
Naibu
Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambaye pia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Mhe. Franco Kiswaga leo tarehe 25 Novemba, 2024
amewaongoza Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi na Wilaya za
jijini Dar es salaam kuwapokea Majaji na Mahakimu wapatao nane (8) kutoka Jimbo
la Niassa nchini Msumbiji waliokuja kwa ziara ya kikazi ya kujifunza na kubadilishana
uzoefu wa namna bora ya uendeshaji wa shughuli za kimahakama.
Akizungumza
wakati wa hafla fupi ya kuwakaribisha Majaji na Mahakimu hao, waliokuja nchini kwa
ajili ya ziara ya kujifunza iliyofanyika Kituo cha Mafunzo cha Mahakama kilichopo
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam Mhe. Kiswaga amesema,
wamepokea ugeni huo kwa furaha kubwa. Lengo la ziara hiyo ikiwa ni kujifunza na
kubalishana uzoefu wa namna bora ya uendeshaji wa shughuli za kimkakati za kimahakama
kwa nchi zote mbili katika ngazi mbalimbali za kimuundo na kimamlaka katika
uendeshaji wa mashauri na utawala.
“Ziara
hii ya kujifunza ya Majaji na Mahakamu wapatao nane (8) kutoka Jimbo la Niassa
nchini Msumbiji itakuwa ya siku tano kuanzia tarehe 25 Novemba hadi tarehe 29 Novemba,
2024. Katika kipindi hicho Majaji hao watapata nafasi ya kutembelea Vituo
Jumuishi vya Utoaji Haki vya Kinondoni na Temeke, kujifunza namna ya usikilizaji
wa mashauri katika Mahakama ya hakimu Mkazi Kisutu…
Kutembelea
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam, Mahakama ya Watoto Mkoa wa Dar es salaam, Kituo
cha Huduma kwa Mteja cha Mahakama, Mahakama ya mwanzo Kawe, Baraza la Ardhi na
Nyumba la Wilaya ya Temeke ili kujifunza kwa vitendo na kubadilishana uzoefu
katika maeneo hayo,” amesema Mhe. Kiswaga.
Aidha,
Mhe. Kiswaga amesema ziara hiyo inathibitisha ubora wa maboresho ya Mahakama yanayoendelea
kufanyika nchi zima katika kuhakikisha Mahakama inatoa huduma bora kwa
wananchi. Sifa hizi zinapaswa kupelekwa kwa Uongozi mzima wa Mahakama ya
Tanzania chini ya Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
“Sisi
Kama Mahakama ya Tanzania tumejipanga kuhakikisha tunatoa kile tulichonacho ili
kuhakikisha tunatimiza malengo ya ziara yenu ya kikazi ya kujifunza na kubadilishana
uzoefu katika nyanja mbalimbali za kazi, kupitia uzoefu tulionao ni rai yetu
kwenu msisite kuchangia yale mazuri mlionayo ili nasi tujifunze kutoka kwenu. Tunatambua
nchi yenu ya Msumbiji mnatumia mfumo wa kutafsiri sheria ambao ni tofauti wa
kwetu wa Jumuiya ya Madola (Common Law System verses Civil Law System) lakini sote
tunafanya kazi moja ya kutoa haki na kuwahudumia wananchi,” amesisitiza Mhe.
Kiswaga.
Mhe.
Kaswaga amesema, ratiba ya ziara hiyo ya kujifunza imejitosheleza kuhakikisha
pande zote zinapata manufaa kutokana na ziara hiyo kusheheni Majaji na Mahakimu
wenye weledi na ufanisi wa hali ya juu. Vilevile watajifunza namna Mahakama
zinavyosikiliza mashauri, namna ya kusoma hukumu na maamuzi mbalimbali, namna
mashahidi wanavyotoa ushahidi mahakamani, namna ya kupokea nyaraka za maombi
mbalimbali mahakamani na Matumizi ya mifumo ya kielektroniki yanavyosaidia utoaji
wa haki kwa wakati.
Kwa
upande wake, Kiongozi wa ujumbe huo wa Majaji na Mahakimu kutoka Jimbo la
Niassa nchini Msumbiji, Jaji Mkuu wa Jimbo la Niassa Mhe. Oscar Basilio
ameushukuru uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa kuwakulia na kuwapa nafasi hiyo
adhimu ya kuja Tanzania kujifunza na kubadilisha uzoefu kwani kwao ni chuchu ya
kuengeza ufanisi katika tasnia ya sheria.
“Napenda
kutoa salaam za dhati na za upendeleo kwa Mahakama ya Tanzania kutoka kwa Jaji
Mkuu wa Msumbiji na Rais wa Mahakama ya Upeo ya Msumbiji Mhe. Adelino Manuel Muchanga kwa kutoa baraka
zote za sisi kuja Tanzania kujifunza mambo mazuri ya uendeshaji wa shughuli za
Mahakama kupitia kwenu. Tunaamini mwisho wa ziara hii ndiyo mwanzo wa mafanikio
ya Mahakama ya Msumbiji,” amesema Mhe. Oscar Basilio.
Mhe.
Basilio amesema, wamekuja Tanzania kujifunza jinsi mfumo wa Mahakama
unavyofanya kazi za utoaji haki. Kupitia mpango kazi huo ulioandaliwa na
Mahakama ya Tanzania unaonyesha dhahiri ubora wa shughuli za utoaji haki.
Vilevile wanaamini Mahakama ya Tanzania imepiga hatua kubwa na ni sehemu sahihi
ya kujifunza mambo mengi mazuri ikiwa ni pamoja matumizi ya Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kusaidia kuharakisha utoaji haki kwa
wakati.
Majaji na Mahakimu wapatao nane (8) kutoka Jimbo la Niassa nchini Msumbiji waliokuja nchini Tanzania kwa ziara ya kikazi ya kujifunza na kubadilishana uzoefu wa namna bora ya uendeshaji wa shughuli za kimahakama wakiwa wanafuatilia wasilisho (mada)
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambaye pia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Mhe. Franco Kiswaga akitoa mada ya Muundo wa Mahakama ya Tanzania
(Picha na Innocent Kansha-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni