Na Daniel Sichula- Mahakama, Mbeya
Naibu
Msajili wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Dyness Lyimo ametoa taarifa ya
mashauri yanayotarajiwa kuendeshwa na Jopo la Majaji wa Mahakama ya Rufani kwenye
kikao maalum cha kuwajulisha wadau wa Mahakama kuwa vikao vya Mahakama hiyo vilivyopangwa
kusikiliza mashauri Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya vitaanza kuendeshwa kuanzia
tarehe 25 Novemba, 2024 hadi tarehe 13 Desemba, 2024 vikijumuisha mashauri 23
kati ya mashauri hayo ya jinai ni 12, masahuri ya madai tisa (9) na mashauri ya
maombi ya madai ni mawili (2).
Akiendesha
kikao hicho maalum Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. Lugano Mwandambo ambaye pia
ni Mwenyekiti wa Jopo la Majaji watatu wa Mahakama ya Rufani watakao sikiliza
mashauri hayo wakiwemo Mhe. Licia Kairo na Mhe. Abdulhakim Issa alisema kuwa,
ni rai yake kwa wadau wote kutoa ushirikiano wa kutosha katika kipindi chote
cha uendeshaji wa vikao hivyo vya usikilizaji wa mashauri hayo. Mathalani
kuwafikisha wafungwa mapema mahakamani na kwa walioko mbali kufika kwa wakati.
“Lengo
la kikao hichi ni kufanikisha usikilizwaji wa mashauri yaliyopo mbele yetu ya
rufaani na kutoa haki kwa wadaawa kwa wakati ili kupunguza mlundikano wa
wafungwa na kuondoa malaamiko ya wadau,”. alisema Mhe. Mwandambo.
Aidha,
Mhe. Mwandambo aliwakumbusha Mawakili wa Serikali na wa Kujitegemea kusoma
vizuri nyaraka za kumbukumbu za mashauri hayo na wakati huo huo kuwasaidia
wateja wao wakiwa mahakamani ili kuisaidia Mahakama kuendesha mashauri hayo kwa
ufanisi mkubwa na kutoa maamuzi stahiki na ya haki kwa wadaawa.
Vilevile,
Mhe. Mwandambo aliwashauri Mawakili wote walioshiriki kikao hicho kujenga
utamaduni wa kwenda mahakamani mara kwa mara kusikiliza na kujifunza namna
uendashaji wa mashauri ya aina hiyo ili kuzijua taratibu za uendeshaji wa
mashauri na kuijua Mahakama zaidi kwani kufanya hivyo kutawajengea uwezo na
kuongeza weledi kitaaluma.
Awali
akisoma taarifa ya Magereza mbele ya Jopo la Majaji hao wa Rufani Inspekta wa Magereza
kutoka Gereza la Ruanda jijini Mbeya Frank Kakamba alisema, Gereza ya Ruanda
Mbeya lina idadi ya Wafungwa na Mahabusu wapatao 942. Wafungwa wanaosubiri
mashauri yao ya rufaani kusikilizwa kupitia vikao hivyo ni wafungwa 12 na
wafungwa sita (6) tayari wapo gerezani na wafungwa wengine sita (6)
wanaandaliwa kutoka magereza yaliyopo nje ya jiji la Mbeya, aliahidi kuwa wafungwa
hao watafikishwa gerezani hapo kabla ya mashauri yao kuanza kusikilizwa.
Naye,
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Aziza Temu, awashukuru Majaji
wa Mahakama ya Rufani na kuwahakikishia kwamba maandalizi yote ya vikao hivyo
yamekamilika na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano wakati wote wa uendeshaji
wa vikao hivyo pale utakapo hitajika.
Wakati
huo huo, Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya Bi. Mavis Miti alisema uwepo
wa vikao hivyo vya kusikiliza mashauri ya rufaani kunapunguza malalamiko ya
wafungwa walioko gerezani kwa kusikiliza rufaani zao pia kuna saidia kupunguza
wafungwa gerezani.
Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Dyness Lyimo (aliyesimama) ametoa taarifa ya mashauri yanayotarajiwa kuendeshwa na Jopo la Majaji wa Mahakama ya Rufani na kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. Lugano Mwandambo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jopo la Majaji watatu wa Mahakama ya Rufani.
Sehemu ya Wajumbe wa kikao hicho wakifuatalia majadiliano ya Kikao Kwa Makini
(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni