Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma
Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi amewaongoza watumishi wa Mahakama hiyo pamoja na washabiki wa mpira wa miguu kushuhudia mtanange wa mechi iliyopigwa katika ya Timu ya watumishi wa Mahakama Kuu Kigoma na Timu ya watumishi Chuo cha Mafunzo Kigoma (KTC) ikiwa ni kukuza mahusiano baina ya Taasisi.
Mechi hiyo ilichezwa jana tarehe 23 Novemba, 2024 katika uwanja wa mpira wa shule ya Sekondari Kigoma ililenga pia kuimarisha afya za watumishi ili kujiepusha na magonjwa yasiyo ya kuambukizwa.
Akizungumza mara baada ya mechi kumalizika, Mhe. Nkwabi aliwapongeza wanamichezo hao kwa kuwa na mechi iliyokuwa na ushindani mkubwa.
“Tunafahamu kuwa mpira huu umechezwa kwa kiwango kizuri ambacho timu zote zimeonesha hamu ya ushindi na niwapongeze washindani wetu kwa matokeo na zaidi niwapongeze timu ya watumishi wa Mahakama kwa kuwapiga chenga nyingi ambazo zimeleta faraja kwa washabiki wenu licha ya kufungwa,” alisema Jaji Nkwabi.
Hata hivyo, kwa upande wa timu ya wanawake (Netball) upande wa Mahakama walijizolea pointi tatu (3) muhimu kwa wapinzani wao kuogopa kufika uwanjani na kucheza kwa kisingizio kuwa maandalizi yao ni hafifu na kukubali kupoteza pointi hizo.
Akizungumza mara baada ya mechi hiyo kumalizika, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Gadiel Mariki aliipongeza timu ya wanawake inayoongozwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Aristida Tarimo kwa ushindi huku akiwataka Uongozi wa timu pinzani kuzingatia muda hii ni mara baada ya Timu za Mahakama kuonesha nidhamu ya kutunza muda kwa kufika kwa wakati huku timu pinzani ilichelewa kufika kwa wakati.
Aidha watumishi wa Mahakama hawakuridhishwa mara baada ya timu pinzani kujaza wachezaji ambao sio watumishi wa Chuo cha Mafunzo Kigoma kama ilivyokusudiwa na kuahidi kukata rufaa.
Alisikika kwa sauti mtumishi mmoja wa Mahakama akisema, “hawa Chuo cha mafunzo Kigoma wameleta wachezaji wa ligi kuu badala ya watumishi wa chuo,” na kuongeza kuwa mechi ijayo utafanyika uhakiki wa kina ili kuweka sawa mizani ya ushindani.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo cha Mafunzo Kigoma (Kigoma Training College) ambaye pia ni Mtaaluma Mkuu aliishukuru Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma kwa kukubali wito wa kushiriki mtanange huo wa kirafiki na kwamba huo ni mwanzo tu kwakuwa wanategemea kuimarisha afya na mahusiano ya kufahamiana zaidi kupitia michezo hiyo.
“Aidha, tunaendelea kuwasisitiza wachezaji kujiandaa vema kwa mechi zingine, matokeo haya ni ya mchezo tu, lengo letu ni kuimarisha afya zetu kisha tuendelee na shughuli za kuwahudumia wananchi,” alisema Mkuu huyo.
Mechi hiyo iliisha ndani ya dakika 90, ambapo Mahakama Kuu Kigoma ilinyukwa bao sita kwa moja.
Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Aristida Tarimo (wa pili kushoto), wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kigoma, Mhe. Eva Mushi, na wa pili kulia ni Msaidizi wa Sheria wa Jaji, Mhe. Varelian Msole, akifuatiwa na mchezaji wa timu ya Mahakama Kuu Kigoma, wakifuatilia mtanange wa mpira wa miguu katika uwanja wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Kigoma.
Kocha Mkuu wa timu ya Mahakama Kuu Kigoma ambaye pia ni Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Mhe. Gadiel Mariki (kushoto) pamoja na Msaidizi wake ambaye ni Msaidizi wa Sheria wa Jaji, Mhe. Varelian Msole (kulia) wakisisitiza jambo na kutoa maelekezo kwa wachezaji wa Mahakama wakati wa mtanange wa mechi hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Wavulana Kigoma.
Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi (aliyesimama upande wa pili kulia) akitoa pongezi kwa timu zote mbili na kuwataka kudumu katika kufanya mazoezi kwani suala la mazoezi ni endelevu katika kuimarisha afya na ubora wa timu husika.
Mchezaji kiungo mkabaji na mzuiaji wa timu ya Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Bw. Martin Pares (katikati) akionesha madoido ya mpira na kuleta furaha kwa washabiki wa kandanda hiyo iliyokuwa ikipigwa katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Wavulana Kigoma.
Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi (mwenye track suit ya bluu bahari) pamoja na viongozi wengine wa Mahakama na Chuo cha Mafunzo Kigoma (KTC) wakiwa katika picha ya pamoja na vikosi vya timu zote mbili mara baada ya kumalizika kwa mechi ya kirafiki iliyopigwa tarehe 23 Novemba, 2024 katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Wavulana Kigoma.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni