• Imepanga kusikiliza jumla ya mashauri 21
• Yawaomba Wadau kutoa ushirikiano ili kumaliza mashauri kwa wakati
Na ARAPHA RUSHEKE, Mahakama- Dodoma
Mahakama ya Rufani Tanzania imepiga kambi katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma katika moja ya vikao vyake vya kusikiliza mashauri ambapo, katika kikao hicho Mahakama hiyo imepanga kusikiliza jumla ya mashauri 21.
Akizungumza na wadau mbalimbali wakati wa kikao cha ufunguzi (pre-session meeting) kilichofanyika jana tarehe 22 Novemba, 2024 katika ukumbi wa mikutano uliopo katika Mahakama hiyo, Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania na Mwenyekiti wa jopo hilo, Mhe. Shaban Ali Lila alitoa rai kwa wadau wote wanaohusika na mashauri kuonesha ushirikiano ili kuhakikisha mashauri yote yaliyopangwa yanasikilizwa na kuamuliwa kwa wakati.
“Nawashuruku wadau wote mliohudhuria kwenye kikao hiki muhimu cha kufungua rasmi kikao cha Mahakama ya Rufani hapa Dodoma, aidha niwaombe wote mnaohusika na mashauri yaliopangwa kuhakikisha mnatoa ushirikiano wa kutosha wakati wa kikao hicho ili kutimiza lengo kwa ufanisi, tuhakikishe kikao hiki kinafanyika kwa asilimia 100 kwahiyo tunaangalia tumejiandaaje kama kulikuwa kuna changamoto yeyote tunapaswa kukabiliana nayo kabla hatujakutana nayo,” alisema Mhe. Lila.
Aliongeza kuwa, ni vema wadau hao kutambua kuwa, Mahakama ya Rufani ni ngazi ya mwisho ya Mahakama nchini ambayo mtu anapata haki kwa mara ya mwisho, hivyo kila mtu anapaswa kuisaidia Mahakama kutoa hiyo haki ya mwisho kwa ufasaha.
Kwa upande wake Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Wanjah Hamza akizungumza wakati akitoa taarifa ya kikao hicho, alisema kwamba katika kuhakikisha ufanisi wa kikao hicho na kwa mantiki ya kufikia malengo yaliyokusudiwa yalifanyika mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na kuandaa Ratiba ya kikao (Causelist) kwa wakati, kusambazwa mapema kwa Hati za kuitwa shaurini na nyingine bado zinaendelea kusambazwa.
Kikao hicho ambacho kitaanza rasmi tarehe 25 Novemba, 2024 huku kikitarajiwa kuhitimishwa tarehe 13 Desemba, 2024 kitaendeshwa na jopo la Majaji watatu, ambao ni Mhe.Shaaban Ali Lila (Mwenyekiti), Mhe. Zainabu Muruke na Mhe. Gerson Mdemu.
Naye, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo aliwakaribisha Majaji hao na kuwaahidi ushirikiano wa kutosha kutoka kwa watumishi wa Mahakama hiyo katika kipindi chote cha kikao hicho.
“Sisi viongozi na watumishi wa Kanda ya Dodoma, tunawakaribisha sana Majaji wa Mahakama ya Rufani na watumishi wengine mliombatana nao na tunaahidi ushirikiano wa kutosha kadri itakavyohitajika wakati wote wa kikao ili kuwezesha usikilizwaji wa mashauri kufanyika katika mazingira rafiki na tulivu,” alisema Mhe.Dkt. Masabo.
Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mwenyekiti wa Jopo la Majaji watakaosikiliza mashauri katika kikao cha mashauri Dodoma, Mhe. Shaban Lila akizungumza na wadau mbalimbali (hawapo katika picha picha) wakati wa kikao cha ufunguzi (Pre-session meeting) kilichofanyika jana tarehe 22 Novemba, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Kituo cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt.Juliana Masabo (kulia aliyevaa miwani) akifuatilia kikao cha ufunguzi (Pre-session meeting). Kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Upendo Ngitiri.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni