Na AMANI MTINANGI, Mahakama-Tabora
Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Zainabu Diwa Mango amewaongoza wadau wa Mahakama katika kikao cha kujadili jinsi ya kuanzisha huduma za Mahakama Inayotembea katika Wilaya ya Sikonge.
Akizungumza wakati wa kikao hicho jana tarehe 19 Novemba, 2024 katika ukumbi wa Mahakama Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Mango alisema lengo la kuanzisha huduma hiyo ya kimahakama ni kusogeza huduma kwa wananchi hasa kwa kuzingatia kuwa, Wilaya ya Sikonge ina mahitaji makubwa ya Mahakama za Mwanzo kwani hadi sasa ina Mahakama moja pekee pamoja na ukubwa wa Wilaya hiyo.
“Pamoja na ukubwa wa Wilaya ya Sikonge, bado tuna Mahakama ya Mwanzo moja tu, ni dhahiri kuna mahitaji makubwa ya Mahakama hizo, tunajipanga kuanzisha huduma ya Mahakama Inayotembea kwa ajili ya Vituo vitatu ambavyo ni Kitunda, Kipili na Nyahua, nyinyi ni wadau muhimu katika kufikisha huduma hiyo kwa wananchi hivyo tunawaomba sana ushirikiano,” alisema Jaji Mango.
Alisema, dhana ya Mahakama inayotembea ilikuwepo tangu mwaka 1920, wakati huo Mahakama ilikuwa ikitumia kiberenge kwenda kusikiliza mashauri katika maeneo yaliyokuwa yakifikiwa na usafiri huo kwa lengo la kumfuata shahidi ambaye ama alikuwa mgonjwa au kufuata vielelezo visivyohamishika.
Naye, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Pamela Mazengo alieleza kuwa Mahakama ipo katika utekelezaji wa Dira na Mpango Mkakati wake kwa kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati na karibu na wananchi na kwamba ili kufanikisha hilo Kanda hiyo inapanga kuanzisha huduma ya Mahakama Inayotembea ili kusogeza huduma hiyo kwa wananchi na wadau wa Mahakama.
Kwa upande wake, Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Bw. Emmanuel John Munda alisema Mahakama inapoenda kukamilisha utaratibu wa kuanzisha huduma hiyo wadau waendelee kutoa elimu kwa wananchi ili wawe na uelewa kuhusu huduma hiyo.
“Mahakama inaelekea kukamilisha utaratibu wa kuanzisha huduma hiyo tunawaomba muendelee kuwafahamisha wananchi waipokee ma wawe na uelewa kuhusu huduma hiyo,” alisema Bw. Munda.
Mahakama inayotembea ni gari maalumu ambalo limeundwa na vifaa muhimu kwa ajili ya kutolea na huduma Mahakama ambazo hakimu anazihitaji wakati wa kutekeleza wajibu wake wa uendeshaji wa mashauri.
Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Zainabu Diwa Mango akizungumza na wadau wakati wa kikao cha wadau kilichofanyika tarehe 19 Novemba, 2024 kuhusu uanzishaji wa Mahakama Inayotembea.
Mdau wa Mahakama (aliyesimama) akichangia jambo wakati wa kikao hicho.
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Bw. Emmanuel John Munda akizungumza jambo wakati wa kikao hicho.
Mdau wa Mahakama Tabora (aliyesimama) akichangia jambo wakati wa kikao hicho.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni