Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Pwani
Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani imefanya hafla ya kuwaaga jumla ya watumishi 13 waliostaafu pamoja na waliohama kutokea katika Kituo hicho cha kazi.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika jana tarehe 01 Novemba, 2024 katika bustani za ZUS CABANA Kiluvya madukani mkoani Pwani, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi amesema watumishi hao wamefanya kazi kwa kujituma na kwa bidi, hivyo kufanyika kwa sherehe hiyo kunaashiria upendo ambao ulikuwepo baina ya watumishi hao.
“Ukiona wote tumekusanyika hapa ni kwa sababu tulifanya kazi vizuri tuliishi kwa ushirikiano, tulipendana ndio maana leo wote tumekusanyika hapa kwa ajili ya kuwaaga” alisema Mhe. Mkhoi
Mhe. Mkhoi pia aliwaomba wastaafu hao kuonesha ushirikiano katika jamii inayowazunguka na kuitumikia kama walivyokua wakitumikia umma wakiwa watumishi.
Naye mmoja wa wastaafu aliyekuwa Msaidizi wa Ofisi Mkuu Bi. Bertha Kalili amewaasa watumishi walioko kazini kuheshimu kazi maana yeye ameitumikia Mahakama ya Tanzania kwa takribani miaka 35 na kwamba katika kipindi chote hajawahi kuandikiwa barua ya onyo au kufanya kosa lolote katika vituo vyote alivyofanyia kazi.
Aidha, mstaafu mwingine, Bi. Angella Hokororo ambaye alikuwa Msaidizi wa Ofisi Mkuu alitoa shukrani zake kwa watumishi kwa njia ya utenzi na alikonga nyoyo zao kwa kuimba kwa ustadi. Kupitia utenzi huo aliwaasa pia watumishi kufanya kazi kwa uadilifu siku zote wawapo katika utumishi wa umma.
Naye, Hakimu Mkazi Mkuu, Mhe Salum Ally amewapongeza watumishi wa Mahakama Pwani kwa kuwa na utamaduni wa kuwaaga wastaafu kwakuwa kitendo hicho kinaongeza upendo.
“Mimi ni mnufaika mkubwa sana na hafla hizi kwani nimekaribishwa sana na kuagwa sana katika mkoa wa Pwani maana nimefanya kazi kazi Pwani na kuhama mara mbili na kurudi tena,” alisema Mhe. Salum.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani na Mahakama ya Wilaya Kibaha na Pamoja na Mahakama za Mwanzo zimekuwa na utaratibu wa kuwaaga watumishi wanaohama au kustaafu na kuwakaribisha wanaohamia katika Mahakama hizo.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi (kushoto) akimlisha kesho mmoja kati ya Wastaafu wa Mahakama hiyo katika hafla maalum iliyoandaliwa kwa ajili ya kuwaaga.
Keki maalum iliyoandaliwa kwa ajili ya watumishi wastaafu na waliohama kutoka Mahakama mkoani Pwani, hiyo ikiwa ni ishara ya upendo kwa waagwa.
Baadhi ya watumishi na wadau wa Mahakama wakiburudika kwa muziki katika hafla hiyo.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi akimpatia zawadi Hakimu Mkazi Mkuu, Mhe. Salum Ally ambaye ni mmoja kati wa wastaafu walioagwa katika hafla hiyo.
Baadhi ya watumishi wa Mahakama Pwani wakiwa wamebeba zawadi kwa ajili ya waagwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni