Jumatatu, 4 Novemba 2024

MIAKA MITATU YA MAHAKAMA YA MWANZO THEMI

Na. SETH KAZIMOTO – Mahakama Kuu Arusha

Mahakama ya Mwanzo Themi ni miongoni mwa Mahakama mbili zilizo chini ya Mahakama ya Wilaya ya Arusha. Hadi kufikia October 2021, Mahakama ya Wilaya Arusha ilikuwa na Mahakama ya Mwanzo moja, ambayo ni Mahakama ya Mwanzo Arusha Mjini (Maromboso). 

Baada ya kuona umuhimu wa kupunguza mlundikano wa mashauri katika Mahakama hiyo, mwaka 2021 Mahakama ya Tanzania ilianzisha Kituo Jumuishi cha utoaji Haki-(IJC) Arusha na Mahakama ya Mwanzo Themi. Mahakama hii ilianza kupokea mashauri tarehe 02 Novemba, 2021.

Akizungumza katika mahojiano maalum hivi karibuni, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Arusha, Mhe. Sheila Manento alieleza kuwa, hapo awali kabla ya kuanza kwa Mahakama ya Mwanzo Themi, Mahakama ya Mwanzo Arusha Mjini ilikuwa ikisikiliza takribani mashauri 3,900 kwa mwaka.

Hadi kufikia tarehe 30 Oktoba 2024, Mahakama ya Mwanzo Arusha Mjini ilikuwa imesajili mashauri 1,376 na kusikiliza mashauri 1,277.

Wakati huo huo, Mahakama ya Mwanzo Themi imesajili mashauri 2,122 na kusikiliza jumla ya mashauri 2,102 katika kipindi hicho. Kwa takwimu hizi ni dhahiri kuwa mlundikano wa mashauri katika Mahakama ya Mwanzo Arusha Mjini umepungua kwa kiasi kikubwa.

Mhe. Manento amewapongeza Mahakimu na watumishi wote wa Mahakama ya Mwanzo Themi kwa kufanya kazi kwa bidii, weledi na uadilifu wa hali ya juu, na Mahakama hiyo ni mfano wa kuigwa na Mahakama zingine.

Akieleza zaidi juu ya mafanikio hayo, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Mwanzo Themi, Mhe. Julieth Mbise alieleza kuwa, Mahakama yake siyo kwamba imepunguza mzigo wa mashauri kwa Mahakama ya Mwanzo Arusha Mjini bali pia imesogeza huduma karibu na wananchi.

“Kadri siku zinavyozidi kwenda, idadi ya mashauri yanayofunguliwa mahakamani hapa inazidi kupanda, kwani wadau wanazidi kupata taarifa juu ya uwepo wa Mahakama hi,i” aliongeza Mhe. Mbise. 

Mhe. Mbise aliipongeza Mahakama ya Tanzania kwa maboresho ya Mahakama yanayoendelea ambapo haki siy tu inaonekana kutendeka, bali inatendeka kwa wakati.



 Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Arusha, Mhe. Sheila Manento akizungumza na Afisa Habari wa Mahakama, Kanda ya Arusha.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Themi, Mhe. Julieth Mbise akizungumza na Afisa Habari wa Mahakama, Kanda ya Arusha.


Sehemu ya watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Themi wakiwa katika picha ya pamoja.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama-Dar es Salaam)

 

 

 

         

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni