Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Pwani
Kufuatia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mnamo tarehe 27 Novemba, 2024 Mahakimu wote wa Mahakama mkoani Pwani wamepatiwa mafunzo ya namna bora ya kuendesha mashauri ya uchaguzi.
Mafunzo hayo yalitolewa jana tarehe 08 Novemba, 2024 katika ukumbi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani na kufunguliwa na Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Hamidu Rajabu Mwanga.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Mhe. Mwanga ambaye pia aliambatana na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaaam, Mhe. David Ngunyale alisema lengo na dhumuni la Mahakama ya Tanzania katika mafunzo hayo ni kuimarisha na kuwajengea uwezo Mahakimu wa Mkoa wa Pwani kuamua mashauri ya uchaguzi kwa weledi, uwazi, usawa na kwa wakati.
“Mahakama ndio mlinzi mkubwa wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo tusimamie kwa uadilifu, tukitengeneza tatizo huku chini litaenda mpaka juu,” alisema Jaji Mwanga.
Aidha, Mhe. Mwanga alisema kuwa, mafunzo hayo yanatolewa kwa kuzingatia kuwa jukumu la Mahakama ni kulinda maadili katika mchakato wa uchaguzi, hivyo Maafisa wa Mahakama wana wajibu wa kusimamia vema mashauri ya uchaguzi yanayofikishwa mbele yao.
Akitoa mada katika Mafunzo hayo, Mhe. Mwanga aliwakumbusha Mahakimu wote kuwa, kutokana na Kanuni C kanuni ndogo ya nane (8) ya Mwenendo na Maadili ya Maafisa wa Mahakama ya mwaka 2020 (Code of Conduct and Ethics for Judicial Offices 2020) hairuhusiwi Mahakimu kushiriki shughuli za kisiasa isipokuwa kujiandikisha na kupiga kura tu.
Naye Mwezeshaji ambaye ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Aziza Mbadjo aliwatoa wasiwasi Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo kuonekana kutokuhusika kutokana na kwamba mashauri ya uchaguzi yanafunguliwa Mahakama za Wilaya na Mahakama za Hakimu Mkazi pekee, alisema ipo migogoro kabla ya uchaguzi na baada ya uchaguzi ambayo hata Mahakama za Mwanzo zinaweza kusikiliza.
Mhe. Mbadjo alitoa mfano wa mashauri hayo kuwa ni pamoja na kufanya fujo wakati wa kampeni, lugha zisizo na staha wakati wa kampeni na kadhalika.
Alisema pia, katika kutatua migogoro hiyo zipo Taasisi za Wadau wa Mahakama zinazohusika ikiwa ni pamoja na Polisi, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na wadau wengine.
Wakufunzi wengine katika mafunzo hayo ni Jaji Ngunyale, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Ardhi, Mhe. Mwajuma Lukindo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Ilala, Mhe. Janeth Kinyage na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Ilala, Mhe. Mohamed Burhan.
Mada zilizofundishwa katika mafunzo hayo ni pamoja na Utawala wa Kidemokrasia, Sheria zinazosimamia Uchaguzi, kutatua migogoro kabla na baada ya uchaguzi na jinsi ya kushughulikia masuala muhimu yanayohusisha uhalifu katika uchaguzi, uandishi wa mwenendo na hukumu katika mashauri ya uchaguzi na maadili katika kusikiliza mashauri ya uchaguzi.
Washiriki wa mafunzo wakimsikiliza mtoa mada Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Hamidu Rajabu Mwanga (hayupo katika picha) wakati akitoa mada katika mafunzo ya namna bora ya kuendesha mashauri ya uchaguzi yaliyotolewa kwa Mahakimu wa Mkoa wa Pwani.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. David Ngunyale akitoa mada kwa washiriki wa mafunzo namna bora ya kuendesha mashauri ya uchaguzi.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Aziza Mbadjo akitoa mada ya namna ya kutatua migogoro kabla na baada ya uchaguzi.
Meza kuu ikiwa katika picha ya pamoja na wawezeshaji na washiriki wote wa mafunzo. Aliyeketi katikati ni Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Hamidu Rajabu Mwanga, kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. David Ngunyale na kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Aziza Mbadjo.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni