Ijumaa, 8 Novemba 2024

MAHAKAMA YA MWANZO HAYDOM YAZINDULIWA KABILA LA WAHDZABE LAFUNIKA ‘SHOO’

Na CHRISTOPHER MSAGATI – Mahakama, Manyara

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara, Mhe. John Kahyoza,  leo tarehe 08 Novemba, 2024 amezindua Mahakama ya Mwanzo Haydom iliyopo katika Kata ya Haydom, Tarafa ya Haydom Wilaya ya Mbulu mkoani Manyara, lengo ikiwa ni kuendeleza jitihada za Mahakama za kusongeza huduma za utoaji haki karibu zaidi na wananchi.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, Mhe. Kahyoza aliwapa pole wakazi wa Kata ya Haydom walioteseka kwa muda mrefu kutokana na umbali wa kufuata huduma ya  haki na kupelekea wengine kukosa haki hiyo ya msingi, kwani awali wananchi walilazimika kusafiri zaidi ya umbali wa kilomita 45 kufuata huduma za Mahakama ya Mwanzo.

“Niwape pole wakazi wa kata hii kwa kipindi cha nyuma kabla ya kuanzishwa kwa Mahakama hii ya Mwanzo Haydom ambapo mlikuwa mnasafiri kwa umbali mrefu kufuata huduma za Mahakama, katika Mahakama ya Mwanzo Dongobesh. Na pia wananchi wengine walilazimika kwenda katika Mahakama za Mwanzo zilizopo Daudi na Endagkot. Vilevile wengine walikosa haki zao kwa kushindwa kusafiri kwa kukosa kumudu gharama za kujikimu,” alisema Mhe Jaji Kahyoza.

Jaji Mfawidhi huyo, alitumia fursa hiyo kuwaomba wananchi kutumia Mhimili wa Mahakama kupata haki zao badala ya kwenda kwenye Mahakama zisizo rasmi kwani, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 107A, Mahakama ndiyo Taasisi pekee iliyopewa jukumu la kutoa haki.

“Ndugu wageni waalikwa, natambua kuna Mahakama nyingi mtaani, lakini nchi yetu inayoongozwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, na kwa mujibu wa Ibara ya 107A, Mahakama ndiyo Mhimili uliopewa jukumu la kutoa haki. Hivyo wanachi wenzangu tutumie Mahakama iliyopewa jukumu la kikatiba na kuepuka kutumia njia isiyo rasmi,” alisema Mhe. Kahyoza.

Jaji Mfawidhi huyo, ametoa rai kwa Viongozi wote wa Mahakama kuhakikisha kwamba, watumishi wote wa Mahakama wanatoa huduma nzuri zinazoendana na uzuri wa jengo, bila kusahau kubadili mienendo na tabia ambazo zinakiuka miiko na maadili ya kazi kwa watumishi wa umma. Pia aliwasisitiza wananchi kuendana na mabadiliko ya TEHAMA kwa sababu ulimwengu wote kwa sasa unaingia katika mabadiliko hayo makubwa ya kimifumo.

“Natoa rai kwa Viongozi wote wa Mahakama, majengo haya ya kisasa na miundombinu yake ni bora na mizuri, hivyo mnapaswa kuhakikisha watumishi wote wanatoa huduma nzuri zinazoendana na uzuri na ubora wa jengo, na kubadili mienendo na tabia ambazo zinakiuka miiko na maadili ya kazi kwa watumishi wa umma, pia wananchi msiogope kutumia mabadiliko ya TEHAMA kwa kuwa yanarahisisha upatikanaji wa haki na taarifa sahihi wakati wowote zinapohitajika” alisema Mhe. Kahyoza.

Kwa upande mwingine, mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Mbulu ambaye ni Afisa Tarafa wa Haydom Bi. Anna Phillip Mpanda aliipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kupata wazo la kusogeza huduma ya Mahakama karibu na wananchi na kujenga Mahakama ya Mwanzo Haydom kwa kuwa ni jambo ambalo lilikuwa na uhitaji wa muda mrefu.

“Eneo hili la Haydom lina watu wengi wanaofanya shughuli mbalimbali za kilimo, biashara pamoja na ufugaji, maeneo kama haya migogoro haikosekani. Uwepo wa Mahakama hii utasaidia sana kukua kwa Uchumi kwa kuwa sehemu ya utatuzi wa migogoro ambayo itakuwa inajitokeza,” alisema Bi. Mpanda.

Aidha, katika uzinduzi wa Mahakama hiyo, shughuli ilipambwa na vikundi mbalimbali vya nyimbo pamoja na wacheza ngoma wa kabila la Wahdzabe ambao ni wenyeji katika eneo hilo. Pia shughuli hiyo ilikwenda sambamba kwa Waheshimiwa Majaji kupanda miti ya Kumbukumbu na Ukataji keki kama ishara ya uzinduzi wa Mahakama hiyo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara Mhe. John Kahyoza (aliyesimama kwenye zulia jekundu katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wacheza ngoma wa Kabila la Wahdzabe mara baada ya hafla ya uzinduzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Haydom. Wengine ni Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara Mhe. Nenelwa Mwihambi (wa tatu kushoto), Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe. Devotha Kamuzora(wa nne kushoto), Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara, Mhe. Frank Mirindo (wa tatu kulia), Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe. Bernard Mpepo (wa kwanza kulia) na wa nne kutoka kulia ni Bi. Anna Mpanda Muwakilishi wa Mkuu wa Wilaya Mbulu.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara Mhe. John Kahyoza akitoa salamu na kuzungumza na hadhira wakati wa Uzinduzi wa Mahakama ya Mwanzo Haydom.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe. John Kahyoza akifunua kitamba kilichoziba kibao kuashiria ufunguzi rasmi wa Mahakama ya Mwanzo Haydom.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe. John Kahyoza  akishirikiana  na Majaji wengine wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara, kukata utepe kama ishara ya ufunguzi wa Mahakama ya Mwanzo Haydom.

Sehemu ya Wananchi wa eneo la Haydom walioshiriki hafla ya uzinduzi wa Mahakama ya Mwanzo Haydom wakifuatilia kwa makini shughuli mbalimbali za uzinduzi wa Mahakama hiyo.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha -Mahakama)




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni