Na SETH KAZIMOTO, Mahakama-Arusha
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel ametembelea Mahakama ya Mwanzo na Wilaya Longido lengo likiwa ni kuona hali halisi ya mazingira ya kazi pamoja na kutambua mafanikio na changamoto zinazoikabili Mahakama hizo.
Akizungumza na watumishi wa Mahakama hizo tarehe 07 Novemba, 2024, Prof. Ole Gabriel alisema kuwa, amezitembelea ili kufahamu nini kinaendelea hususani Mahakama ya Mwanzo Longido ikizingatiwa kuwa, takribani asilimia 70 ya mashauri yote nchini hutokea katika Mahakama za Mwanzo.
Mtendaji Mkuu huyo alisema pia, amefika mahakamani hapo kuwapongeza na kuwatia moyo watumishi ikizingatiwa kuwa mazingira wanayofanyia kazi yana changamoto kadhaa, lakini wanaendelea kufanya majukumu yao ya kikazi kwa mafanikio, ambapo alisema, “ninawapongeza kwa kazi nzuri na endeleeni kuwa wabunifu katika kazi wakati tunashughulikia changamoto zilizopo hapa Longido.”
Katika taarifa iliyosomwa na Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Longido, Mhe. Fredrick Shayo ilitaja changamoto kadhaa wanazokumbana nazo kazini ikiwa ni pamoja na uhaba wa watumishi, ukosefu wa maji, eneo la Mahakama kutokuwa na uzio na Mtandao wa Mahakama kuwa chini hali inayosababisha Mahakama hiyo wakati mwingine kushindwa kuendesha mashauri katika Mfumo wa Uratibu na Usimamizi wa Mashauri (e-CMS).
Mhe. Shayo alitaja changamoto zingine kuwa ni mahabusu kutoka Magereza kupelekwa Longido mara moja kwa wiki na kadhalika.
Akizungumzia changamoto hizo, Prof. Ole Gabriel alisema kuwa, katika ajira mpya zilizotangazwa hivi karibuni Mahakama ya Wilaya Longido itazingatiwa katika mgao wa watumishi wapya.
“Mahakama imeweka mikakati kadhaa ya kutatua changamoto ya maji ikiwa ni pamoja na kununua mtambo wa kuchimba visima vya maji ili kuondokana na tatizo la maji katika Mahakama zetu ikiwemo na Longido,” aliongeza Mtendaji Mkuu.
Aliongeza kuwa, Mahakama imeanzisha Kitengo cha Ujenzi “Building Brigade” ambacho kitafanya baadhi ya kazi za ujenzi katika Mahakama ikiwemo ujenzi wa uzio wa Mahakama ya Wilaya Longido.
Akizungumzia kuhusu changamoto ya mtandao wa Mahakama kuwa chini, Prof. Ole Gabriel alimuelekeza Afisa TEHAMA wa Mahakama Arusha afike mahakamani hapo kutatua changamoto hiyo.
Kadhalika, Mtendaji Mkuu alizungumzia kuhusu suala la uzinduzi wa Mahakama ya Wilaya Longido, ambapo alieleza kwamba, taratibu zianze ili uzinduzi ufanyike na alimuelekeza Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Arusha kufanya mawasiliano na Mtendaji wa Mahakama Kuu ili utaratibu huo uanze.
Katika hatua nyingine, Prof. Ole Gabriel alipendekeza kuangalia uwezekano wa kuweka mfumo wa umeme unaotumia nishati ya jua ili kupunguza changamoto kutokana na kukatika kwa umeme ikizingatiwa kuwa mashauri yanaratibiwa kwa njia ya kielektroniki na hivyo uhakika wa uwepo wa umeme ni mojawapo ya mazingira wezeshi katika usikilizaji wa mashauri kwa ufanisi zaidi.
Baada ya kutembelea Mahakama ya Wilaya na Mwanzo Longido, Mtendaji Mkuu wa Mahakama alipata fursa pia ya kupita Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha kwa ajili ya kumsalimia Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Ilvin Mugeta katika.
Ujio wa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania wilayani Longido umeleta faraja, matumaini na ari mpya kwa watumishi kwa sababu utatuzi wa changamoto za kikazi mahakamani hapo unakwenda kupatikana hivi karibuni na watumishi wamefurahi kutembelewa na Mkuu huyo.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati mstari wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama ya Wilaya na Mwanzo Longido tarehe 07 Novemba, 2024 alipotembelea Mahakamani hapo. Wa pili kushoto ni Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Longido, Mhe. Fredrick Shayo, wa kwanza kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Bw. Festo Chonya, wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Namanga, Mhe Shila Dyumu na wa pili kulia ni Afisa Utumishi wa Mahakama ya Wilaya Longido, Bi. Flora Katega.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akikagua mipaka ya eneo la Mahakama ya Wilaya Longido alipotembelea Mahakama hiyo tarehe 07 Novemba, 2024. Kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Bw. Festo Chonya.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) akisaini kitabu cha wageni katika Ofisi ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda Arusha alipowasili kumsalimia Jaji Mfawidhi, Mhe. Ilvin Mugeta (kushoto).
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni