Na Daniel Sichula – Mahakama, Mbeya
Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. Dkt. Mary Caroline Levira ameongoza kikao cha tathmini ya kufunga kikao cha uendeshaji wa mashauri ya Mahakama ya Rufaa jijini Mbeya kilichoanza tarehe 21 Oktoba, 2024 Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Mbeya.
Akisoma taarifa ya awali Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama ya Rufani Tanzania Mhe. Emmanuel G. Mrangu alisema, asilimia 81 ya mashauri yote yaliyopangwa kusikilizwa yamesikilizwa, ambayo idadi yake ilikuwa mashauri 26 yaliyopangwa, mashauri 18 ya jinai na madai yamesikilizwa na mashauri matatu (3) yanasubiri kufanyiwa uwamuzi huku mashauri matano (5) yamehairishwa kutokana na sababu mbalimbali.
Mhe. Mrangu alisema, katika tathmini hiyo kuwa usikilizwaji wa mashauri hayo umebaini changamoto kadhaa walizokutananazo wakati wa uendeshaji wa vikao vya mashauri hayo miongoni mwake ni kuchanganywa kwa nyaraka, mapungufu ya mienendo ya mashauri na vielelezo na hivyo kusababisha baadhi ya mashauri kutokamilika kutokana na mapungufu hayo.
Aidha, Mhe. Dkt. Levira aliwashauri Mawakili wa Serikali na wa kujitegemea kuwaongoza mashaidi vizuri wawapo mahakamani na kujitahidi kusoma vielelezo vizuri wakati wa uendeshaji wa mashauri hayo. “Mashauri mengi yaliyosikilizwa nimeona yana mapungufu makubwa kwa upande wa mawakili katika kuwaongoza mashahidi ambapo inapelekea wadaawa kukosa haki zao,” alisema Jaji Levira.
Wakati huo huo Mhe. Dkt. Levira awapongeza Jeshi la Magereza Kanda ya Mbeya kwa kuzingatia muda wa kuwafikisha wafungwa mahakamani kwa wakati na kwa muda uliopangwa kwa kipindi chote cha uendeshaji wa vikao hivyo vya Mahakama ya Rufani.
Vilevile Mhe. Dkt. Levira aliwashukuru Majaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Mfawidhi na Majaji Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Mawakili wa Serikali na wa Kujitegemea, Ofisi ya Mashtaka, Jeshi la Polisi pamoja na Magereza kwa ushirikiano walioutoa wakati wote wa usikilizwaji wa mashauri ya rufani Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya.
Naye, Jaji wa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania Mhe. Issa John Maige alisema mawakili wa Serikali na Kujitegemea wanapaswa kupitia nyaraka mbalimbali za taarifa za mashauri na kujiweka sawa ili kuweza kuepuka na kuzuia dosari wakati wa usikilizwaji wa kesi mahakamani.
Kwa upand wake Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. Dkt. Benhajj Shaaban Masoud alisema, kukosea taratibu au kanuni za kisheria, kunaharibu utaratibu wote wa usikilizwaji wa mashauri, alichukua nafasi hiyo kuwahasa Majaji na Mahakimu kuzingatia kanuni na sheria katika uendeshaji na usikilizaji wa mienendo ya mashauri.
Kikao
hicho kilihudhuriwa na Majaji wa Mahakama ya Rufani na wale wa Mahakama Kuu Kanda
ya Mbeya ikwa ni pamoja na Mhe. Issa J. Maige, Mhe. Dkt. Benhaji S. Masoud,
Naibu Msajili Mfawidhi Emmanuel G. Mrangu, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya
Mbeya Mhe. Joachim Tiganga, Mhe. Victoria Nongwa na Mhe. Aisha A. Sinda,
Mahakimu, Mawakili wa Serikali na Kujitegemea wa Mahakama Mkoa wa Mbeya.
Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama ya Rufani Tanzania Mhe. Emmanuel G. Mrangu (kushoto) akisoma taarifa ya tathimini ya uendeshaji wa kikao cha Mahakama ya Rufani kilichofanyika Mahakama Kuu Mbeya, Kulia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. Dkt. Mary Caroline Levira aliyeongoza kikao hicho.
Jaji wa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania Mhe. Issa John Maige (kulia) na Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. Dkt. Benhajj Shaaban Masoud (kushoto) wakiwa nasikiliza taarifa ya tathmini ya Kikao cha Mahakama ya Rufani.
Majaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya wakiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Tiganga wa kwanza kushoto wakisikiliza kikao hicho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni