Jumatano, 6 Novemba 2024

JAJI KIPENKA MSEMEMBO MUSSA APUMZISHWA

  • Jaji Mkuu aongoza mamia ya waombolezaji kumsindikiza
  • Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Kati atoa ujumbe mzito

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Singida 

Mamia ya Watanzania leo tarehe 6 Novemba, 2024 wamejitokeza kumsindikiza Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Kipenka Msemembo Mussa aliyefariki Dunia tarehe 2 Novemba, 2024 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (Mlonganzila) jijini Dar es Salaam.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewaongoza watumishi wa Mahakama na Watanzania kwa ujumla katika safari ya mwisho ya Jaji Kipenka ambaye amezikwa kwenye makaburi ya familia Kinampanda katika Wilaya ya Iramba, Mkoa wa Singida.

Viongozi wa Mahakama waliohudhuria maziko hayo ni Majaji sita wa Mahakama ya Rufani, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Majaji wanne wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mtendaji wa Mahakama Kuu, Msajili wa Mahakama Kuu, Mtendaji wa Mahakama ya Rufani, Naibu Wasajili, Watendaji wa Mahakama na Mahakimu kutoka Mahakama Singida. Alikuwepo pia Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Fatuma Masengi.

Kabla ya kulazwa kwenye nyumba yake ya milele ilifanyika ibaada iliyoongozwa na Mkuu wa Kanisa la Kiiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kati, Baba Askofu Dkt. Syprian Hilinti kumwombea Marehemu Kipenka kabla ya Viongozi wa Mahakama, Bunge na Serikali kutoa salamu za rambirambi.

Katika salamu zake, Jaji Mkuu wa Tanzania amemwelezea Marehemu Kipenka kama mtumishi wa umma aliyetekeleza majukumu yake kwa weledi, uaminifu na bidii ya hali ya juu na kwamba mchango wake kwa Taifa hautasahaulika kutokana na mambo makubwa aliyoyafanya.

“Ili kuweza kupata historia yake kamili ni vizuri kufanya ulinganifu maeneo gani alikuwa anafanya kazi na sheria gani muhimu zilipitishwa au uamuzi gani muhimu umefanyika,” amesema.

Alitoa mfano wa Marehemu Kipenka alipokuwa Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuna sheria nyingi muhimu zilipitishwa, ikiwemo Mkataba wa Afrika Mashariki, Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2002.

“Kwa hiyo, ukitaka kuandika historia yake ni lazima urejee matukio muhimu yaliyojitokeza ambayo alishiriki bila kupata sifa. Bahati nzuri, kazi alizozifanya akiwa mahakamani zipo katika maamuzi yake ambayo yapo kwenye mtandao wa TanzLII. Watoto mkitaka kuandika historia ya baba tayari kunataarifa nyingi sana ambazo zipo,” amesema.

Aliwaomba mama mzazi, mke wa marehemu na familia kwa ujumla kuwa na faraja kuwa Kipenka Msemembo Mussa ameacha historia na mchango mkubwa kwa nchi yake na kuwasihi kumshukuru Mungu kwa maisha yake.

Akizungumza kwa niaba ya Serikali, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Geofrey Peter Pinda ameiomba familia ya Marehemu Kipenka kuwa na utulivu katika kipindi hiki kigumu na kuwaomba Watoto wasisahau kuwa mwenza wa Kipenka Msemembo Mussa bado yupo.

“Tafrsi ya mwenza wengi hawaielewi, mwenza ni kitu kimoja ambacho kinakaa pamoja, hakuna aliyechini wala juu. Kwa hiyo, nguvu ya mama bado ipo pale pale. Kwako mama kizaa chema, Mungu akutie nguvu sana na uendelee kusihi na wajukuu wako vizuri ili muweze kulimaliza jambo hili salama,” amesema.

Akiwasilisha salamu kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendegu ameunga na wananchi wa Kinampanda katika maeombolezo hayo na kwa kutambua kazi kubwa aliyoifanya marehemu Kipenka kwa Kanisa la KKKT, Mahakama na Taifa kwa ujumla.

Alitumia fursa hiyo kutoa pole kwa Jaji Mkuu wa Tanzania, mke na mama wa marehemu kwa msiba huo mkubwa. “Hakuna jambo kubwa kama kupoteza mtoto wakati wewe ungali hai. Unategemea mtoto akuzike, inauma sana kwa mzazi anapomtanguliza yeye…

“Lakini ni mapenzi ya Mungu na tunaiombea familia ishikamane. Haya mazuri yaliyosemwa hapa mwende mkayaenzi, mwendelee kumheshimisha (marehemu Kipenka),” amesema.

Naye Askofu Hilinti akizungungumza kwenye mahubiri, aliwakumbusha waombolezaji kuwa vitu vyote walivyonavyo, ikiwemo cheo, heshima vitawaacha, ila matendo yao wataambatana nayo watakapoiacha Dunia.

“Ili matendo mabaya yasifuatane na sisi ni muhimu kutubu. Tubuni maana ufalme wa Mungu umekaribia. Wapendwa, kila mmoja, kwa nafasi yake, kwa kazi yake asali, awe na ibaada, amwamini Yesu Kristo mfufuka,” amesema.

Marehemu Jaji Kipenka alijiunga na Mahakama ya Tanzania mwaka 2004 alipoteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania hadi mwaka 2012 alipoteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania kabla ya kustaafu utumishi wa umma mwaka 2019.

Kabla ya kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu, Marehemu Kipenka alikuwa Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2004 alipoteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Marehemu Kipenka aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Haki za Binadamu katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakili wa Serikali, Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya kuchunguza mauaji ya wafanyabiashara wanne wa amadini Januari, 2006 na Katibu wa Tume ya Rais ya Kuchunguza mazingira ya mauji ya aliyekuwa Mkuu wa Usalama wa Taifa Tanzania, Luteni Kanali Imran Kombe Julai, 1996.

Mwili wa Marehemu Jaji Kipenka Msemembo Mussa ukiwa tayari kushushwa kwenye nyumba yake ya milele. Picha chini, mwili ukiwa unashushwa taratibu.


Mkuu wa Kanisa la Kiiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kati, Baba Askofu Dkt. Syprian Hilinti akiongoza ibaada ya mazishi mbele ya kaburi la Marehemu Jaji Kipenka Msemembo Mussa.

Mke wa Marehemu Jaji Kipenka Msemembo Mussa, Bi. Rehema Kipenka Mussa akiweka shada la maua kwenye kaburi la mume wake.

Watoto wa Marehemu Jaji Kipenka Msemembo Mussa wakiweka shada la maua kwenye kaburi la baba yao.

Mama mzazi wa Marehemu Jaji Kipenka Msemembo Mussa, Bi. Anna Thomas Mussa akisaidiwa kuweka shada la maua.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendegu pamoja na Viongozi wengine wa Serikali wakiweka mashada ya maua.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwaongoza Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania (juu na chini) kuweka mashada ya maua.


Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania (juu na chini) wakiweka mashada ya maua.


Wakurugenzi wa Mahakama ya Tanzania wakiweka mashada ya maua kwenye kaburi la Marehemu Jaji Kipenka Musemembo Mussa.


Mkuu wa Kanisa la Kiiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kati, Baba Askofu Dkt. Syprian Hilinti akiweka shada la maua kwa niaba ya Viongozi wengine wa dini.
Mwili wa Marehemu Jaji Kipenka Musemembo Mussa ukiwasili nyumbani kwao Kinampanda. Picha chini Afisa Utumishi wa Mahakama ya Tanzania Ezra Kyando akihakikisha kila kitu kinaenda sawia.


Mwili wa Marehemu Jaji Kipenka Musemembo Mussa ukiingizwa ndani ya nyumba ya wazazi wake Kinampanda.

Mwili wa Marehemu Jaji Kipenka Musemembo Mussa upo ndani kusubiri ibaada ya mazishi.

Mwili wa Marehemu Jaji Kipenka Musemembo Mussa ukitolewa ndani ya nyumba ya wazazi wake na kupokelewa na Majaji wa Mahakama ya Rufani wakiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.

Majaji wa Mahakama ya Rufani wakiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma wakitafakari kabla ya ibaada ya mazishi kuanza.

Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Viongozi Waandamizi wa Mahakama ya Tanzania wakiungana na waomboleza kutafakari msiba huo mkubwa.

Ibaada ya mazishi inayoongozwa na 
Mkuu wa Kanisa la Kiiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kati, Baba Askofu Dkt. Syprian Hilinti (picha).


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni