Jumatano, 6 Novemba 2024

KAMATI YA JAJI MKUU YAFANYA UKAGUZI MKOANI SONGWE

Na Iman Mzumbwe - Mahakama, Songwe

Kamati ya Jaji Mkuu ya Ukaguzi, Ufuatiliaji na Tathimini imefanya ziara ya kikazi Mkoani Songwe, ikiongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro Mhe. Stephen Magoiga akiambatana na Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi na Ukaguzi wa Shughuli za Kimahakama, Mrejesho kwa Umma na Maadili Mhe, Maira. S. Kasonde pamoja na Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya Mhe, Aziza Temu.

Kamati hiyo ilifanya ziara hiyo mkoani Songwe mnamo tarehe 4 Novemba, 2024 na kupokelewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Songwe Mhe. Francis Kishenyi aliyewasilisha Taarifa fupi ya utendaji kazi wa shughuli za kimahakama Mkoa Songwe. Vilevile Kamati hiyo ilifanya ukaguzi wa Rejista za mashauri katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe, Mahakama ya Wilaya Mbozi na Mahakama ya Mwanzo Vwawa Mjini.

“Katika ukaguzi huu tumeabaini uwepo wa changamoto chache katika ujazaji wa Rejista za mashauri ni rai yangu watumishi wakumbushwe na kupewa elimu na maelekezo juu ya ujazaji wa rejista za mashauri ya kesi lengo ikiwa ni kupata ufanano wa ujazaji wa rejista katika Mahakama zote nchini.” alisema Mhe. Magoiga  

 Mhe. Magoiga aliwapongeza Mahakimu kwa kazi nzuri wanayofanya na jitihada wanazofanya  katika kupunguza mlundikano wa mashuari mahakamani pamoja na kutoa nakala za hukumu na mwenendo wa kesi kwa wakati na  pia kuwepo kwa mpango mkakati waliojiwekea wa kupunguza mahabausu wenye makosa yanayodhaminika kwenye gereza la Mbozi.

Aidha, Mhe. Magoiga aliwasisistiza Mahakimu Wafawidhi kushughulikia Mashauri ya mirathi kwa waledi na uadilifu na pia kuhakikisha wanaonufaika na mirathi wanalipwa stahiki zao kwa wakati na kuhimiza wanufaika hao kufunga mashauri hayo ya mirathi baada ya kukamilika kwa taratibu husika za shauri.

Mhe, Magoiga alizungumza na watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe, Mahakama ya Wilaya Mbozi na Mahakama ya Mwanzo Vwawa mjini ambapo aliwapongeza kwa kazi nzuri wanayofanya na kuwasisistiza watumishi hao kufanya kazi kwa bidii, ushirikiano na upendo, aliendelea kusema kuwa kila mtumishi akiwa na uadilifu, weledi na uwajibikaji basi Mahakama itaendelea kujenga na kuongeza imani kwa wananchi na wadau wake katika utoaji wa haki.

Kamati hiyo ya Ukaguzi, Ufuatiliaji na Tathmini  imeendelea na ziara  ya kikazi Mkoa wa Songwe na wametembelea Mahakama ya Wilaya Momba na Mahakama na Mahakama ya Mwanzo Tunduma ikiwa ni hitimsho la ziara hiyo Mkoani Songwe na kutoa maelekezo kuwa changamoto zilizobainika zifanyiwe kazi kufikia Disemba, 2024 ziwe zimetatuliwa.

Kamati ya ufuatiliaji na Tathmini wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama ya Hakamu Mkazi Songwe, Wilaya ya Mbozi na Mahakama ya Mwanzo Vwawa mjini.

Naibu Msajili Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Aziza Temu  akiwa katika picha na Mkurugenzi wa Usimamizi na Ukaguzi wa shughuli za Mahakama Mhe. Maira Kasonde wakifuatilia namna Mfumo wa e-CMS unavyafanya kazi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe.

Watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa Songwe, Wilaya ya Mbozi na Mahakama ya mwanzo Vwawa mjini wakisikiliza maelekezo kutoka kwa Kamati ya Ufuatiliaji na Tathmini Mkoa wa Songwe.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Jaji Mkuu Mhe.Stephen Mgoige akizungumza na watumishi wa Mahakama katika ofisi ya Hakimu Mkazi Songwe.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Jaji Mkuu Mhe.Stephen Mgoige akitoa elimu na maelekezo juu ya ujazaji wa rejista za mashsuri kwa Wahe,Mahakimu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe.

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Mbozi Mhe. Nemes Chami akitoa taarifa ya utendaji kazi kwa Kamati ya ufuatiliaji na Tathmini.


Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Jaji Mkuu Mhe. Stephen Magoige akisoma Taarifa ya utendaji kazi Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha-Mahakama)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni