Na SALUM TAWANI-Mahakama, Dar es Salaam
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim
Hamis Juma jana tarehe 5 Novemba, 2024 aliungana na Viongozi mbalimbali wa
Kidini na Serikali katika Misa maalum ya kuuaga mwili wa marehemu, Jaji Mstaafu
wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Kipenka Msemembo Mussa katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT)
Wazo Hili jijini Dar es salaam kwa ajili ya kutoa salamu za mwisho kwa Marehemu.
Mhe. Prof. Juma aliwapa salamu za pole wanafamilia kwa niaba
ya Mahakama ya Tanzania kwa kusema kuwa, anawasilisha salamu zake za faraja kwa
Mama, Mke wa marehemu, watoto, ndugu na jamaa wote kwa kufikwa na msiba huo
mzito ambao ni mkubwa kwetu sote.
Mhe. Prof. Juma alisema kuwa, alipokea
salama za rambirambi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan ambaye amewatakia salama za faraja. Naye Spika wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson alituma salamu zake za
faraja kwa wanafamilia.
“Nimepokea salaam nyingi kutoka kwa
Wahe. Majaji wa Mahakama ya Rufani ambao walipata nafasi ya kufanya kazi na
Mhe.Mussa Kipenka na pengine salam zao zinatoa taswira hasa Jaji Kipenka
aliishi namna gani na Wahe. Majaji wenzake na aliishi namna gani na watumishi
wengine wa Mahakama na nina amini aliishi wa watumishi wengine Serikalini kwa
upendo na mshikamano.” Aliongeza Jaji Mkuu.
“Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani Mhe.
Edward Rutakangwa ambaye alifanya kazi kwa muda mrefu na marehemu anasema ni
huzuni nzito iliyojaa mioyoni mwetu baada ya kupata taarifa ya kifo cha Mhe.
Mussa Kipenka aliongeza kuwa kifo chake
ni pigo kubwa kwa wale wote wanaomfahamu
kwa karibu na kufanya kazi naye alikuwa ni mtu mwema ni Jaji aliyezingatia
viwango vya juu katika kutenda haki, alikuwa na uwezo mkubwa wa kujituma na
alikuwa haogopi kufanya kazi yoyote ambayo alipewa,” alisema Mhe. Prof. Juma.
“Mimi katika salamu zangu nawataka wanafamilia,
ndugu na jamaa watambue hiyo ndiyo picha tubaki nayo milele, kwamba marehemu
alikuwa ni mtu ambaye alitumikia Taifa lake kwa kutukuka sana kwa zaidi ya
miaka 42. Na pia alifanya kazi zake kwa bidii kubwa pamoja na wasifu ambao tumesomewa
leo kutokana na vituo vingi vya kazi nyingi ambazo amefanya, tukiamua
kuorodhesha mambo mema aliyofanya katika kila kituo chake cha kazi sidhani kama
tutapata muda wa kutosha kuelezea. Kwa sababu hizo na nyingine nyingi niwaomba
Mke, Mama na watoto wa marehemu mrudi nyumbani mkiwa na furaha kwamba Mhe.
Kipenka ameacha historia na heshima kubwa kwa Taifa Lake. Bwana ametoa Bwana
ametwaa jina lake lihimidiwe Amina,” alisema Jaji Mkuu.
Mapema jana Jaji Mkuu Mhe. Prof.
Juma alifika msibani nyumbani kwa Marehemu, Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani
Tanzania, Mhe. Kipenka Msemembo Mussa maeneo ya Madale jijini Dar es Salaam kwa
ajili ya kutoa salamu za pole na baadae kuelekea katika Kanisa la K.K.T Wazo
Hili kwa ajili ya kutoa salamu za mwisho kwa Marehemu.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam
Mhe. Albert Chalamila alitoa salamu za pole kwa Mahakama ya Tanzania na familia
kwa jumla, alisema kuwa, Mhe. Jaji Kipenka amefanya kazi kubwa sana ndiyo maana
leo tunamuenzi hapa kifo kinaonyesha mwisho wa nguvu za mwanadamu pia
inaonyesha mipaka ya muda wa mwadamu.
“Naomba kusisitiza kwa kusema, huwa
tunatumia pesa nyingi sana katika kuandaa mazishi na baada ya mazishi watoto na
familia ya Marehemu hatuijali tena. Ninaomba sana ule urafiki wetu tuliokuwa
nao na Marehemu tuendelee nao na tungalie namna tutakavyoweza kuisaidia familia
ya Mhe. Kipenka ili iweze kufikia malengo yake.” Aliongeza Mhe. Chalamila.
Kwa upande wake, Mtoto wa Marehemu
Bw. Anorld Kipenka Mussa kwa niaba ya familia aliishukuru sana Mahakama ya
Tanzania chini ya Uongozi wa Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwa kuwa pamoja na
familia tangu kipindi cha ugojwa mpaka katika kipindi hiki cha kuandaa mazishi ya
mpendwa wao.
Mwili wa Marehemu utasafirishwa kwenda
kijijni kwao Kinampanda mkaoni Singida kwa ajili ya mazishi siku ya tarehe
6 Novemba, 2024. Marehemu Kipenka alifikwa na umauti tarehe 2 Novemba, 2024
katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (Mloganzila) alipokuwa amelazwa kwa
matibabu.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa pili kushoto aliyeweka mkono kwenye sanduku) pamoja na Wahe. Majaji wengine wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania wakisimdikiza sanduku lililobeba Mwili wa Marehemu Mhe. Kipenka Msemembo Mussa ambaye alikuwa Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila.
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akitoa salam
za pole kwa niaba ya Mahakama ya Tanzania katika msiba wa Marehemu, Jaji Mstaafu
wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Kipenka Msemembo Mussa.
Wanafamilia wa Marehemu
Mhe. Kipenka Msemembo Mussa ambaye alikuwa Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani wakiwa
katika Kanisa la K.K.T Wazo Hili jijini Dar es salaam kutoa heshima zao za mwisho kwa mpendwa wao.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akimfariji Bi. Rehema Kipenka Mussa ambaye ni Mke wa Marehemu wa Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Kipenka Msemembo Mussa.
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa kwanza kushoto) akijadiliana
jambo na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila katika msiba wa aliyekuwa Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani Mhe. Kipenka Msemembo Mussa.
Picha hii inaonyesha sanduku lililobeba Mwili wa Marehemu Mhe. Kipenka Msemembo Mussa ambaye alikuwa Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania.
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akitia saini
kwenye kitabu cha maombolezo katika msiba wa Marehemu, Jaji Mstaafu wa Mahakama
ya Rufani, Mhe. Kipenka Msemembo Mussa.
(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni