Na FESTO SANGA, Mahakama-Kigoma
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile amewataka wajumbe wa kamati ya Uongozi kuweka mkazo katika kusimamia viwango vya ndani vya muda wa usikilizaji mashauri katika Kanda hiyo ili kuondokana na mashauri ya mlundikano.
Mhe. Rwizile aliyasema hayo tarehe 02 Novemba, 2024 alipokuwa akifungua kikao cha kamati ya Uongozi kilichofanyika wilayani Kibondo.
“Tusipoweka mikakati madhubuti ya kuzuia na kuondokana na mashauri ya mlundikano tutalazimika kila wakati kuweka mikakati ya kusafisha mashauri hayo,” alisema Jaji Rwizile.
Aliwataka wajumbe wa kikao hicho kutathmini kwa kina iwapo mashauri ya mlundikano yaliyopo yanafaa kuwepo na kuweka mikakati madhubuti ya kuzuia na kuondoa mashauri ya mlundikano katika Kanda hiyo, huku akisema kuwa mwaka ujao nyakati kama hizo kusiwe na shauri ya mlundikano kwa kuiwekea mkazo mikakati iliyopo.
Viwango vya ndani vya usikilizaji wa mashauri ndani ya Kanda hiyo ukiacha vile vya kitaifa vya usikilizaji wa mashauri ni Mahakama za Mwanzo kudumu na shauri kwa miezi mitatu, Mahakama ya Wilaya/Hakimu Mkazi miezi sita na Mahakama Kuu mwaka mmoja.
Akitoa taarifa ya hali ya mashauri katika Kanda ya Kigoma, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe Gadiel Mariki aliwafahamisha wajumbe wa kikao kuwa hadi kufikia tarehe 31 Desemba, 2024 Mahakama Kuu itakuwa na jumla ya mashauri 45 yenye mwaka mmoja, Mahakama ya Mkoa na Wilaya zitakuwa na mashauri 128 yenye miezi sita (6) ambayo katika mpango wa ndani wa Kanda yatakuwa katika orodha ya mashauri mlundikano.
Aidha, Mhe. Mariki alibainisha kuwa, hadi kufikia tarehe 31 Desemba mwaka huu mashauri yote yatakuwa yamemalizika huku akiongeza kwamba utekelezaji kwa vitendo wa mpango wa Mahakama Kuu Kigoma unaendelea na vikao maalum na kwamba Mahakama za Wilaya zenye mashauri machache, Mahakimu wake wanatumika kusikiliza mashauri kwenye vituo vyenye mashauri mengi.
Naye, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Bw. Filbert Matotay akiwasilisha taarifa ya Utendaji kazi na bajeti alionesha kuwa Kanda ya Kigoma imepiga hatua kuelekea Mahakama isiyotumia karatasi kutokana manunuzi machache ya shajara kwa robo hiyo ukilinganisha na robo iliyopita.
Bw. Matotay aliwasihi wajumbe wa kikao kuendelea na mkakati wa Mahakama isiyotumia karatasi hasa katika maeneo ambayo hayalazimishi kutumia karatasi.
Kikao hicho kiliazimia kuwa, Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo kuanza kuchapa mienendo ya mashauri ikiwa ni maandalizi ya utayari wa kuingia kwenye mfumo mpya wa Kielektroniki wa Usikilizaji na Uratibu wa Mashauri (e-CMS) katika ngazi hiyo ya Mahakama.
Aidha, kikao hicho kilienda sambamba na mafunzo ya kuwajengea uwezo Viongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma juu ya utendaji kazi wa Pori la Akiba Moyowosi linalopakana na Mahakama ya Mwanzo Nyavyumbu iliyopo Wilayani Kibondo ili wajumbe hao wakiwa kama wadau muhimu wawe na uelewa wa pamoja na kuimarisha mshikamano.
Mhifadhi Wanyamapori kutoka Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA) wa Pori la Akiba Moyowosi, Bw. James Maundi aliushukuru Uongozi wa Mahakama kwa ushirikiano wanaoendelea kupatiwa.
Kikao hicho kilihitimishwa kwa mchapalo na mechi iliyochezwa na watumishi wa Mahakama dhidi ya Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo ambapo timu ya Halmashauri ya Wilaya hiyo iliibuka na ushindi wa goli mbili.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile (katikati) akiwa katika picha ya pamoja Viongozi wa Kamati ya Uongozi Kanda ya Kigoma. Walioketi pamoja naye ni Majaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, kushoto ni Mhe. John Nkwabi na kulia ni Mhe. Projestus Kahyoza.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Projestus Rweyongeza Kahyoza (aliyesimama) akichangia mada wakati wa kikao cha Kamati ya Uongozi wa Kanda hiyo. Kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile na kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Bw Filbert Matotay.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe Aristida Tarimo akichangia mjadala uliokuwa ukiendelea wakati wa kikao cha Uongozi kilichoketi tarehe 02 Novemba, 2024 wilayani Kibondo.
Mhifadhi Wanyapori kutoka mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA) wa Pori la Akiba Moyowosi, Bw. James Maundi akiwaonesha mipaka ya Pori hilo wakati akiwasilisha mada kwa wajumbe wa kikao hicho kilichofanyika hivi karibuni.
(Picha na Nasoro Kiyombe)
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni