- Jaji Mfawidhi aongoza ziara ya utalii huo
- Lengo ni kuboresha ushirikiano kazini baina ya pande mbili
Na RICHARD MATASHA, Mahakama-Mtwara
Katika juhudi za kukuza umoja, ushirikiano na upendo kazini, watumishi wa Mahakama ya Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara pamoja na baadhi ya wadau, wakiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo, Mhe. Rose Ebrahim wamefanya ziara ya kipekee kwenye Hifadhi ya Bahari ya Ghuba ya Mnazi na maingiliano ya mto Ruvuma-Msimbati ambapo walipata fursa ya kuona pomboo (dolphins) wakiwa katika mazingira yao ya asili.
Ziara hiyo ilifanyika tarehe 09 Novemba, 2024 katika moja ya maeneo ya ufukwe wa Bahari ya Hindi na ililenga kuimarisha uhusiano kati ya watumishi hao na kutoa nafasi ya kupumzika pamoja huku wakishiriki katika michezo mbalimbali ya ufukweni.
Pamoja na kushuhudia viumbe wa baharini, watumishi hao walifanya shughuli za kujenga timu ikiwemo michezo ya kuhamasisha ushirikiano kama vile mpira wa miguu, mikono na kufanya mazoezi kwa pamoja.
Jaji Mfawidhi, Mhe. Ebrahim aliwapongeza watumishi kwa juhudi zao za kuimarisha utawala wa sheria na alisisitiza umuhimu wa kuweka kando changamoto za kazi na kujenga mazingira bora ya kazi kupitia ushirikiano wa pamoja.
“Ziara hii inatufundisha kuwa kama pomboo (dolphins) wanavyoshirikiana katika bahari, ndivyo tunavyopaswa kushirikiana sisi katika kazi zetu za kila siku – kwa umoja na upendo, tunaweza kushinda changamoto yoyote inayotukabili,” alisema Jaji Mfawidhi.
Watumishi wa Mahakama Kanda hiyo walifurahia na kuridhika na ziara hiyo huku wakisema kuwa, ilikuwa ni fursa ya kipekee ya kujenga uhusiano wa karibu na wenzao pamoja na kuboresha mazingira ya kazi.
“Ni muhimu kuwa na nafasi kama hii ambapo tunapata fursa ya kuzungumza na kushirikiana nje ya mazingira ya kisheria, jambo hili linakuza ushirikiano," alisema mmoja wa watumishi.
Ziara hiyo ilikamilika kwa chakula cha pamoja kati ya watumishi wa Mahakama Mtwara pamoja na wadau ambapo pia walifanya majadiliano kuhusu njia bora za kuboresha utendaji kazi na kuimarisha huduma kwa wananchi. Watumishi wa Mahakama walionesha nia ya kuendeleza desturi hii ya kufanya shughuli za kijamii ili kudumisha ushirikiano mzuri na umoja kazini.
Aidha, ziara hiyo ambayo ililenga zaidi ya kutembelea maeneo ya kitalii, kujenga na kuimarisha maadili, upendo, kuhamasisha kazi kwa pamoja na kuleta umoja kwa watumishi wa Mahakama hiyo.
Picha mbalimbali za matukio ya utalii kwenye hifadhi ya Bahari ya Ghuba ya Mnazi na maingiliano ya mto Ruvuma – Msimbati.
Picha mbalimbali za Viongozi, watumishi na wadau wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara wakiongozwa na Jaji Mfawidhi Mhe. Rose Ebrahim wakifurahia utalii katika fukwe za hifadhi ya bahari ya Ghuba ya Mnazi na maingiliano ya mto Ruvuma – Msimbati mkoani Mtwara.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni