Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma
Jumla ya watumishi wanne kutoka Idara ya Mipango na Utafiti ya Mahkama ya Zanzibar ikiongozwa na Mkurugenzi wa Mipango na Utafiti wa Mahkama hiyo wamekutana na Watumishi wa Idara ya Mipango na Uratibu ya Mahakama ya Tanzania ili kujifunza na kupata uzoefu kuhusu utendaji kazi wa Idara hiyo lengo likiwa ni kuboresha utendaji kazi wa Mhimili wa Mahkama Zanzibar.
Wakiwa katika kikao cha kujifunza na kubadilishana uzoefu kilichofanyika leo tarehe 13 Novemba, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Mipango na Uratibu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Erasmus Masumbuko Uisso amesema lengo la ujio wa ugeni huo ni kupata uzoefu katika Idara ya Mipango ya Mahakama ya Tanzania.
“Watumishi wenzetu kutoka Mahakama Zanzibar, wamekuja kwa lengo la kujifunza na kupata uzoefu katika Idara yetu ambapo wanatarajia kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo usimamizi na uratibu wa miradi, uandaaji na utekelezaji wa bajeti na kadhalika,” amesema Bw. Uisso.
Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa, watumishi hao kutoka Mahkama ya Zanzibar wameomba kujifunza na kupata uzoefu juu ya usimamizi na uratibu wa miradi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa kuwa nao wanatekeleza Mradi wa unaofadhiliwa na fedha za mkopo kutoka Benki hiyo.
Kadhalika, watumishi hayo pamoja na mambo mengine watajifunza kuhusu usimamizi, uratibu na ushirikiano wa wadau wa Kitaifa, Kikanda na Kimataifa, Uratibu na usimamizi wa Mpango Mkakati kwa Watendaji, Wakuu wa Divisheni na Vitengo sambamba na kupata uzoefu katika uandishi wa maandiko mbalimbali ya kuomba miradi.
Naye Mkurugenzi wa Mipango na Utafiti wa Mahkama ya Zanzibar, Bw. Mohamed Salum Mohamed amesema kuwa, Mahkama ya Zanzibar pamoja na Mahakama ya Tanzania wana ukaribu wa kimahusiano jambo ambalo limeleta ukaribu wa kusaidiana katika maeneo mbalimbali ikiwemo kuboresha utendaji kazi baina ya Mihimili hiyo.
“Mahakama ya Tanzania na Mahkama ya Zanzibar tumekuwa na ushirikiano wa miaka mingi, hivi sasa ushirikiano huu umekuwa ukitusaidia katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuboresha maeneo ya kazi, kuboresha taaluma na hata ujuzi,” amesema Bw. Mohamed.
Amesema kuwa, lengo la ziara yao ni kujifunza na kupata uzoefu wa namna Idara ya Mipango na Ufuatiliaji ya Mahakama ya Tanzania inavyofanya kazi kwa kuwa wao bado wako nyuma.
“Lengo la ziara yetu kama Maafisa wa Mipango na Utafiti ni kufahamu namna wenzetu wanavyofanya kazi kwakuwa wao wamepiga hatua, sisi bado tupo nyuma kidogo hivyo, lengo ni kubadilishana mawazo juu ya maandalizi ya bajeti na utekelezaji wake, usimamizi wa miradi na kadhalika ambayo kimsingi yatatusaidia nasi kuboresha huduma,” amesema Mkurugenzi huyo.
Ameongeza kwa kukiri kuwa, ziara yao imekuwa ya mafanikio makubwa kwa kuwa wamepata zaidi ya kile walichokusudia.
Mahakama ya Tanzania imeendelea kuwa sehemu ya kujifunzia kwa Mahakama na Taasisi mbalimbali ndani na nje ya nchi kufuatia kupiga hatua za kimaboresho katika uendeshaji wa shughuli yake ya msingi ya utoaji haki kwa wananchi.
Watumishi wa Idara ya Mipango na Ufuatiliaji wa Mahkama ya Zanzibar wakifuatilia wasilisho lililokuwa likitolewa na Mkurugenzi Msaidizi wa Mipango na Ufuatiliaji Mahakama ya Tanzania, Bi. Gladys Qambaita (hayupo katika picha).
Picha ya pamoja kati ya Watumishi wa Idara ya Mipango na Ufuatiliaji ya Mahakama ya Tanzania na Idara ya Mipango na Utafiti ya Mahkama ya Zanzibar. Waliosimama mbele katikati ni Mkurugenzi wa Mipango na Ufuatiliaji Mahakama ya Tanzania, Bw. Erasmus Masumbuko Uisso, kushoto ni kurugenzi wa Mipango na Utafiti wa Mahkama ya Zanzibar, Bw. Mohamed Salum Mohamed na kulia ni Afisa Mipango kutoka Mahkama ya Zanzibar, Bi. Saada Mussa Shaaban.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni