• Ni wakati akifunga Mkutano Mkuu wa EAMJA
• Asisitiza pia ushirikiano wa Mahakama za Ukanda huo
• Majaji na Mahakimu wa Ukanda huo waja na maazimio kadhaa ikiwemo kurekebisha na kuboresha Mifumo ya Haki ya Jinai
Na MARY GWERA, Mahakama-Arusha
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson ametoa rai kwa Majaji na Mahakimu wa Ukanda wa Afrika Mashariki kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) hususani Akili Mnemba (AI) ili kurahisisha utoaji wa huduma ya haki kwa wananchi.
Mhe. Dkt. Tulia aliyasema hayo jana 04 Desemba, 2024 wakati akifunga Mkutano Mkuu wa 21 wa Chama cha Mahakimu na Majaji wa Afrika Mashariki (EAMJA) katika Hoteli ya Gran Melia` jijini Arusha.
“Kuimarisha mifumo ya Kimahakama ni muhimu sana, hivyo ni muhimu kufanya hivyo ikiwemo kuimarisha matumizi ya Akili Mnemba katika huduma ya utoaji wa haki,” amesema Spika wa Bunge.
Ameongeza pia, ni vema kuangalia na kubainisha changamoto zinazohusiana na matumizi ya Akili Mnemba (AI) na TEHAMA kwa ujumla ili kuzitafutia ufumbuzi kwa mustakabali wa utoaji haki kwa wakati.
Katika hatua nyingine, Spika huyo amezikumbusha Mahakama za Nchi hizo kuendeleza ushirikiano katika kuwahudumia wananchi.
Kadhalika, Mhe. Dkt. Tulia ameishukuru Mahakama ya Tanzania na Chama cha Mahakimu na Majaji wa Afrika Mashariki (EAMJA) kwa kutambua umuhimu wa Mihimili ya Serikali na Bunge na kuwashirikisha katika ufunguaji na ufungaji wa Mkutano Mkuu wa 21 wa Chama hicho.
Ametoa rai kwa Viongozi wa Serikali na Mahakama katika Ukanda huo kuziwezesha Mahakama kwa kuvipa vitendea kazi muhimu ili kutekeleza majukumu yake kwa ufasaha na haraka.
“Ninaamini kupitia Mkutano huu, kile tutakachokubaliana kitaweza kuwekwa kama kigezo cha utekelezaji na uboreshaji wa huduma za kimahakama kwa Mahakama zote za Ukanda huu,” amesema Spika wa Bunge.
Naye, Rais wa Chama cha Mahakimu na Majaji wa Afrika Mashariki (EAMJA), Mhe. John Eudes Keitirima alisema kuwa, Chama hicho hakitasita kuwasilisha kwa Viongozi maazimio yaliyofikiwa na kukubalika katika Mkutano huo lengo likiwa ni kuboresha huduma ya utoaji haki kwa wananchi.
Mhe. Keitirima, ametoa rai kwa Mamlaka za Ukanda huo kuongeza bajeti za Mahakama ili kuziwezesha kufanya kazi kwa ufanisi kwa manufaa ya wananchi.
Wanachama cha Chama hicho wametoka na maazimio kadhaa ambayo ni pamoja na kuimarisha Uhuru na Utawala wa Mahakama ili Mahakama zitekeleze majukumu yake waliyopewa kikatiba, ufadhili ni muhimu, hivyo, Mkutano huo umeomba Serikali za Ukanda wa Afrika Mashariki (EAC) kutoa fedha za kutosha kwa Mahakama.
Azimio lingine ni kukuza ushirikiano wa Mahakama za Ukanda wa Afrika Mashariki (EAC) ambapo Mkutano huo umezitaka Nchi ambapo sio Wanachama wa Chama hicho kujiunga na EAMJA.
Maazimio mengine ni Kuimarisha Uwezo wa Mahakama kupitia Teknolojia na Ubunifu ambapo imeelezwa kuwa, Mahakama za Ukanda wa Afrika Mashariki ziweke alama kati yao juu ya matumizi ya teknolojia ambayo tayari iko tayari kubainisha teknolojia inayofaa kwa matumizi ya kawaida.
Mengine ni kurekebisha na kuboresha Mifumo ya Haki ya Jinai, kupanua Upatikanaji wa Haki kupitia Urekebishaji wa Mchakato wa Biashara, kukuza Marekebisho ya Mahakama na Vipimo vya Utendaji, kuoanisha sheria ya kazi kwa mazingira mazuri ya uwekezaji katika Ukanda wa EAC
Mkutano huo ulibebwa na Kaulimbiu isemayo, ‘Uboreshaji wa mifumo ya utoaji haki kwa ajili ya kuimarisha utengamano na Ukuzaji Uchumi katika Ukanda wa Afrika Mashariki.’
Mkutano huo uliosheheni mada mbalimbali umekutanisha zaidi ya wajumbe 387 kutoka Zanzibar, Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi na Sudani ya Kusini.
Washereheshaji wakiendelea kutoa matangazo mbalimbali wakati wa hafla ya kufunga Mkutano Mkuu wa 21 wa Chama cha Mahakimu na Majaji wa Afrika Mashariki (EAMJA) jana tarehe 04 Desemba, 2024.
Picha mbalimbali za washiriki wa Mkutano Mkuu wa 21 wa Chama cha Mahakimu na Majaji wa Afrika Mashariki.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni