Na ARAPHA RUSHEKE- Mahakama Kondoa
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof.Elisante Ole Gabriel jana tarehe 4 Desemba, 2024 amekagua shughuli zinazoendelea katika mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Haubi na kutoa maelekezo mahsusi ya kukamilisha mradi huo kwa wakati, viwango na ubora uliokusudiwa kwa mujibu wa mkataba.
Mradi huo ambao unajengwa katika Wilaya ya Kondoa, iliyoko jijini Dodoma unatekelezwa na kampuni ya Moladi Construction, ambapo katika ukaguzi huo Mtendaji huyo, alionesha kufurahishwa na hatua zilizochukuliwa na kukamilisha ujenzi kwa kuzingatia matakwa ya mkataba na maelekezo mbalimbali ambayo yamekuwa yakitolewa.
“Najua mradi huu unatakiwa kuisha Machi 2025 lakini nitashukuru sana kama mtaweza kumaliza mwishoni mwa Januari 2025, lengo ni moja bila kuharibu ubora, ubora ubaki vilevile lakini likiisha mapema nitashukuru sana lazima tukiri tuna changamoto kubwa na wakandarasi wengi, sasa imetokea kwamba miradi mingi ambayo tumempa Moradi ndiyo ambayo inafanya vizuri, sasa ningetamani tukisimama mbele ya watu tukasema kampuni ya Moradi inafanya vizuri tuwe na mifano halisi…
“Sasa mkiweza kukazana likaisha 31 Januari, 2025 itakuwa na faida nyingi kwani wananchi wa Haubi wamesubiri hili jengo kwa muda mrefu sana,”alisema Prof.Ole Gabriel.
Aidha Mtendaji Mkuu huyo aliwahimiza wakandarasi kuzingatia kalenda ya shughuli zilizopangwa kufanyika kwa kipindi cha utekelezaji wa mkataba huo wa ujenzi.
Aliongeza pia anatamani tutume ujumbe kwa wengine kwamba inawezekana kumaliza mapema jengo letu hilo na lazima tujivunie pale ambapo panawezekana ili tunaposhindwa ijulikane pia imeshindikana kwa sababu ambazo ni za msingi. Hivyo pale panapo wezekana tuweze kujivunia na wakandarasi wetu kama inavyosisitizwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan kila wakati kwamba wapeni kipaumbele wazawa.
Alisisitiza kwamba vifaa vyote viwepo tayari na muda wowote katika eneo la mradi ikiwa ni pamoja na mpangilio wa nguvu kazi iliyopo ili kukidhi kalenda ya matukio ya ujenzi wa jengo hilo unakamilika kama ambavyo ilivyokusudiwa.
Kwa upande wao wakandarasi hao kutoka Ogm na Moladi walimshukuru Mtendaji huyo kwa kuwatembelea na kushukuru kwa kupewa fursa ya kufanya hiyo kazi na wanaahidi kuifanya kadri ya uwezo wao usiku na mchana ili kuweza kutimiza lengo ambalo lililokubaliwa.
1.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni