- Mamia wajitokeza kuomboleza kifo chake
- Yumo Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam
Na BAKARI MTAULA-Dar es
Salaam
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 29 Desemba, 2024 amewaongoza Viongozi
mbalimbali kushiriki katika dua maalum ya kumuombea na kumuaga Jaji wa Mahakama
ya Rufani Tanzania, Mhe. Mwanaisha Athuman Kwariko aliyefariki Dunia tarehe 27
Desemba, 2024 nchini India alipokuwa anapatiwa matibabu.
Dua hiyo iliyohudhuriwa
na Watumishi wa Mahakama na Viongozi mbalimbali wa Serikali imefanyika nyumbani
kwa Marehemu maeneo ya Masaki Mwisho, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar-es-salaam.
Jaji Mkuu alipata wasaa
wa kutoa salamu za pole kwa familia, huku akionesha hisia zake baada ya kuguswa
na msiba huo ambao umeacha pengo kubwa kwa Mahakama ya Tanzania.
Mhe. Prof. Juma
amemwelezea Marehemu Kwariko kuwa mtumishi aliyekuwa anatekeleza majukumu yake
kuwa kuzingatia maadili na mchapakazi ambaye alitumia muda wake kuwasaidia
wenzake kuliko kujiangalia yeye.
“Jana nilipofika hapa
nilisaini kitabu cha maombolezo. Nilipata shida sana kumuelezea mtu
ninayemfahamu kuanzia kusoma kwake kwa sababu ni Mwanafunzi wangu na pia Jaji
tuliyefanya kazi kwa karibu, siyo rahisi kumuelezea mtu huyo kwa kuandika
mistari miwili,” amesema Jaji Mkuu.
Mhe. Prof. Juma amenukuu
maneno katika kitabu yaliyoandikwa na Mwandishi wa Vitabu Danai Lama yanayosema,
“Kama hatuwezi kuwasaidia wengine katika maisha yetu, tuhakikishe kwamba
hatuwakwazi na hatuwaharibii maisha watu wegine.”
Viongozi wa Mahakama
waliohudhuria dua hiyo ni Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji wastaafu wa Mahakama ya Rufani, Jaji Mkuu wa Zanzibar,
Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Majaji wastaafu wa Mahakama Kuu, Viongozi Waandamizi wa Mahakama na
watumishi wengine wengi.
Alikuwepo pia Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam na Viongozi wengine wa kiserikali katika Mkoa na Wilaya.
Mwili wa Marehemu Kwariko utaswaliwa kesho tarehe 30 Desemba, 2024 baada Swalat Fajr katika Msikiti wa Maamour Upanga Jijini Dar-es-salaam, kisha utasafirishwa kupelekwa Wilaya ya Kondoa Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya mazishi.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (juu na chini) akizungumza wakati wa dua ya kumwombea Marehemu Mwanaisha Athman Kwariko iliyofanyika nyumbani kwake Masaki leo tarehe 29 Desemba, 2024.
Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla akizungumza wakati wa dua hiyo. Picha chini ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni