Jumapili, 29 Desemba 2024

JAJI MKUU ASHIRIKI DUA KUMWOMBEA MAREHEMU MWANAISHA ATHUMAN KWARIKO

  • Mamia wajitokeza kuomboleza kifo chake
  • Yumo Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam

Na BAKARI MTAULA-Dar es Salaam

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 29 Desemba, 2024 amewaongoza Viongozi mbalimbali kushiriki katika dua maalum ya kumuombea na kumuaga Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Mwanaisha Athuman Kwariko aliyefariki Dunia tarehe 27 Desemba, 2024 nchini India alipokuwa anapatiwa matibabu.

Dua hiyo iliyohudhuriwa na Watumishi wa Mahakama na Viongozi mbalimbali wa Serikali imefanyika nyumbani kwa Marehemu maeneo ya Masaki Mwisho, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar-es-salaam.

Jaji Mkuu alipata wasaa wa kutoa salamu za pole kwa familia, huku akionesha hisia zake baada ya kuguswa na msiba huo ambao umeacha pengo kubwa kwa Mahakama ya Tanzania.

Mhe. Prof. Juma amemwelezea Marehemu Kwariko kuwa mtumishi aliyekuwa anatekeleza majukumu yake kuwa kuzingatia maadili na mchapakazi ambaye alitumia muda wake kuwasaidia wenzake kuliko kujiangalia yeye.

“Jana nilipofika hapa nilisaini kitabu cha maombolezo. Nilipata shida sana kumuelezea mtu ninayemfahamu kuanzia kusoma kwake kwa sababu ni Mwanafunzi wangu na pia Jaji tuliyefanya kazi kwa karibu, siyo rahisi kumuelezea mtu huyo kwa kuandika mistari miwili,” amesema Jaji Mkuu.

Mhe. Prof. Juma amenukuu maneno katika kitabu yaliyoandikwa na Mwandishi wa Vitabu Danai Lama yanayosema, “Kama hatuwezi kuwasaidia wengine katika maisha yetu, tuhakikishe kwamba hatuwakwazi na hatuwaharibii maisha watu wegine.”

Viongozi wa Mahakama waliohudhuria dua hiyo ni Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji wastaafu wa Mahakama ya Rufani, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Majaji wastaafu wa Mahakama Kuu, Viongozi Waandamizi wa Mahakama na watumishi wengine wengi.

Alikuwepo pia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Viongozi wengine wa kiserikali katika Mkoa na Wilaya.

Mwili wa Marehemu Kwariko utaswaliwa kesho tarehe 30 Desemba, 2024 baada Swalat Fajr katika Msikiti wa Maamour Upanga Jijini Dar-es-salaam, kisha utasafirishwa kupelekwa Wilaya ya Kondoa Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya mazishi.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (juu na chini) akizungumza wakati wa dua ya kumwombea Marehemu Mwanaisha Athman Kwariko iliyofanyika nyumbani kwake Masaki leo tarehe 29 Desemba, 2024.


Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla akizungumza wakati wa dua hiyo. Picha chini ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila.

 

Huzuni kubwa ikiwa imetawala wakati wa maombolezo (picha juu na mbili chini).





Sehemu ya waombolezaji (juu na chini) wakiwa kwenye sala maalum.


Dua ikiendelea.

Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakisaini kwenye kitabu cha maombolezo. Juu ni Mhe. Dkt. Yose Mlyambina na chini ni Mhe. Wilbert Chuma.



(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)








Hakuna maoni:

Chapisha Maoni