- Ni katika kuadhimisha miaka mitatu ya Kituo hicho tangu kuanzishwa kwake
- Chasisitiza matumizi ya Usuluhishi katika utatuzi wa migogoro ya familia
Na NAOMI KITONKA, Mahakama- Temeke
Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke kimeendesha kikao maalum pamoja na Wadau wa Mahakama cha kufanya tathmini ya miaka mitatu tangu kuanzishwa kwa Kituo hicho.
Akitoa neno la utangulizi katika kikao hicho hivi karibuni katika ukumbi wa Mikutano wa Mahakama hiyo, Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa aliwakaribisha wadau katika kituo Jumuishi Temeke alisema lengo la kikao hicho kufanya tathimini ya miaka mitatu tangu kuanzishwa kwa kituo hicho ili kuweza kubadilishana uzoefu wa namna bora ya kuboresha zaidi huduma.
“Lengo pia la kikao chetu ni kuleta kufanya tathmini ya miaka mitatu tangu kuanzishwa kwa kituo hiki ili kuweza kubadilishana uzoefu wa namna bora ya kushughulikia masuala ya Mirathi, Ndoa na Familia ili kuzidi kuimarisha Kituo chetu tuweze kumaliza mashauri kwa muda mfupi tukishirikiana nanyi wadau wa muhimu katika kurahisisha zoezi la upatikanaji haki kwa haraka hasa kupitia masuala ya usuluhishi kabla ya kuendesha mashauri,” alisema Mhe. Mnyukwa.
Jaji Mnyukwa alisema, wao kama Kituo Jumuishi Temeke wanazingatia usuluhishi kabla ya kuendesha mashauri na huo ni mkakati wa Mahakama wa kumaliza mashauri kwa njia mbadala ya usuluhishi ili kupunguza muda wa ufuatiliaji, gharama za uendeshaji na kuleta tumaini na faraja kwa pande zote mbili.
“Tunatambua mchango mkubwa wa Mabaraza ya usuluhishi katika Mahakama zetu katika kusaidia zoezi la upatikanaji haki na kupunguza migogoro isiyo na lazima katika familia hasa katika masuala ya Mirathi na ndoa na hii ni muhimu kwa ajili ya maendeleo mazima ya nchi na mustakabali wa kizazi kijacho,” alisisitiza Jaji Mfawidhi huyo.
Katika kikao hicho wadau pia walipata nafasi ya kujifunza mada mbalimbali kuhusu taratibu za uendeshaji wa mashauri ya mirathi katika Mahakama ya Mwanzo na Wilaya pamoja na Usimamizi wa Mirathi kuanzia Mahakama ya Wilaya mpaka Mahakama Kuu, Usuluhishi katika Mashauri ya ndoa na mwisho ilikuwa mada ya Jinsi ya kuandika Wosia.
Watoa mada katika kikao hicho walikuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Temeke, Mhe. John Msafiri, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo, Mhe. Hamis Mlaponi, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Watoto-Temeke, Mhe. Orupa Mtae, Msaidizi wa Sheria wa Jaji ambaye pia ni Hakimu Mkazi, Mhe. Dominician Kafuba pamoja na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya, Mhe. Simon Swai ambao wote kwa pamoja waliwasilisha mada kwa ubora na ufanisi.
Baada ya mada kutolewa, Wadau hao wa haki walipata fursa ya kuuliza maswali na kupata uelewa zaidi katika mada zilizowasilishwa na kuomba Mahakama kuwasaidia kujua ni vitu gani muhimu vinavyohitajika kwao kama viambatanisho hasa kwa wafuatiliaji wa masuala ya Mirathi hasa RITA, BRELA, Ardhi na Benki ikiwa pamoja na kuiomba Mahakama kupitia vitu vinavyohitajika kwao ili kuondoa vikwazo katika kuharakisha kwa usikilizwaji wa Mashauri.
Akitoa hitimisho katika kikao hicho, Jaji wa Mahakama Kuu Temeke, Mhe. GladysNancy Barthy alisema, “tumefurahia ushiriki wenu pamoja nasi katika kikao hiki muhimu na Kama Kituo Jumuishi Temeke tumechukua michango yenu na tutaiboresha ili kuweza kusaidia mashauri yaende kwa haraka mkiwa ni kiungo muhimu katika zoezi la utoaji elimu kwa wananchi ambao ni wateja wetu.”
Mhe. Barthy alisema kuwa, wana imani na Wadau hao kuwa watasaidia kuifikisha elimu hiyo muhimu na kuifanyia kazi ili kuondoa ukwamishwaji wa haki kwa namna yoyote ile.
Kikao hicho kilihudhuriwa na wadau kutoka RITA, Wizara ya Ardhi, Halmashauri ya Mkoa wa Dar es Salaam, WLAC, Benki za Mkoa wa Dar es Salaam, Ustawi wa Sheria pamoja na wadau wengine wa Mahakama.
Washiriki wengine ni Mahakimu Wafawidhi kutoka Mahakama ya Mwanzo, Mahakama ya Wilaya pamoja na Mahakama ya Mtoto wakiwa pamoja na Mahakimu kutoka Mahakama ya Mwanzo na Mahakama ya Wilaya katika Kituo Jumuishi Temeke.
Jaji wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Gladys Nancy Barthy akitoa neno la shukrani katika kikao cha wadau kilichofanyika katika Kituo hicho.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Watoto katika Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Mwamini Kazema akizungumza katika kikao cha wadau kilichofanyika hivi karibuni katika Kituo hicho.
Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya Katika Kituo Jumuishi Temeke, Mhe. Simon Swai (aliyesimama mbele) akitoa mada kuhusu umuhimu wa kuacha wosia katika Mirathi katika wakati wa kikao cha Wadau kilichofanyika hivi karibuni kituoni hapo.
Afisa Ustawi Mfawidhi wa Mahakama ya Watoto, Bi. Asha Ally Mbaruku akichangia mawazo katika kikao cha Wadau kilichofanyika hivi karibuni katika Kituo Jumuishi Cha Masuala ya Ndoa na Familia Temeke.
Mdau akiuliza maswali baada ya mawasilisho kutoka kwa Watoa mada (hawapo katika picha) wakati wa kikao kilichofanyika hivi karibuni kituoni hapo.
Mdau akiuliza maswali na kuchangia mada baada ya mawasilisho katika kikao kilichofanyika hivi karibuni kituoni hapo.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni