Jumatatu, 9 Desemba 2024

UJENZI MAHAKAMA YA WILAYA KILOSA, MAHAKAMA YA MWANZO MAGUBIKE WAIVA

  • Wakandarasi wakabidhiwa maeneo
  • Wananchi wapokea mradi huo kwa furaha

 Na Evelina Odemba - Mahakama Kilosa

Wananchi wa Wilaya ya Kilosa hivi karibuni walishuhudia tukio la kihistoria la makabidhiano ya mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Kilosa na Mahakama ya Mwanzo Magubike.

Tukio hili lilifanywa na aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi katika Viwanja vinavyotarajiwa kujengwa Mahakama hizo na kushuhudiwa na wananchi mbalimbali ambao hawakuificha furaha yao ya kusogezewa huduma ya Mahakama iliyoboreshwa.

Mhe. Prof. Kabudi aliambatana na viongozi mbalimbali wa Mahakama wakiongozwa na Mtendaji wa Mahahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha na mwenyeji wao, Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Morogoro, Bw. Ahmed Ng’eni, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kilosa, Mhe. Agnes Ringo, watumishi wa Mahakama na Viongozi wa Serikali ngazi ya Wilaya wakiongozwa na  Katibu Tawala, Bi. Salome Mkinga aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya, Watendaji wa Kata na Vijiji na Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji na wananchi kwa ujumla.

Akizungumza wakati akikabidhi miradi hiyo kwa Mkandarasi Mbaraka Kihame toka Kampuni ya Kika Consntractors anayejenga Mahakama ya Wilaya na Mkandarasi Godfrey Mogellah toka Gopa Contractors anayejenga Mahakama ya Mwanzo, Mhe. Prof. Kabudi alitoa rai kwa wananchi wa kuitunza miundombinu ya ujenzi huo kwa kuwa mradi huo umeletwa  kwa ajili yao.

“Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan ameweka uzito na umuhimu mkubwa katika Mhimiri wa Mahakama ikiwa ndio chombo pekee cha utoaji haki. Leo tunaishuhudia Mahakama ya kisasa kila tunapotembea ndani ya Nchi hii. Rai yangu kwenu, mradi huu ni wa kwetu, kama tulivyoupokea kwa furaha tuutunze na kutoa ushirikiano kadri tutakavyohitajika kufanya hivyo,” alieleza Mhe. Prof. Kabudi.

Aliendelea kueleza kuwa maboresho makubwa yananayofanywa na Mahakama ya Tanzania yamufanya Mhimiri huo kuwa kinara na mfano mzuri wa kuigwa katika ujenzi wa miundombinu, huku akitolea mfano wa watu toka mataifa mbalimbali wanaokuja kujifunzakujenga Vituo Jumuishi na kuongeza kuwa kila Mtanzania asikae kinyonge bali ajivunie maboresho makubwa ya Mahakama ya Tanzania.

Naye Bw. Magacha alieleza kuwa wanatarajia kukabidhiwa jengo la Mahakama ya kisasa na Mkandarasi likiwa limekamilika ifikapo tarehe 19 Agosti, 2025. Alieleza kuwa jengo hilo la kisasa litakuwa na ofisi za wadau pamoja na Mahakama ya Mwanzo Kilosa Mjini ili kurahisisha huduma ya utoaji wa haki kwa mwananchi.

“Natoa shukurani kwa uongozi wa Serikali wilayani hapa kwa ushirikiano wenu hadi leo tumepata maeneo ya kujenga Mahakama za kisasa. Naomba muendelee kushirikiana nasi katika kuhakikisha mwananchi anasogezewa huduma ya haki,” alisema.

Akitoa salamu za Wilaya kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, Bi. Salome Mkinga ambaye ni Katibu Tawala wa Wilaya hiyo alisema kuwa wapo tayari kushirikiana na Mahakama kama ambavyo wamekuwa wakifanya hivyo na kusema kuwa mradi huo upo sehemu salama.

Naye mwananchi Yusuph Pandije kutoka Kata ya Magubike alisema kuwa ujenzi wa Mahakama hiyo umewatua mzigo mkubwa wa gharama za utafutaji haki kwa kuwa wamekuwa wakilazimika kuifuata huduma hiyo wilayani Gairo, jambo linalowapelekea kutumia kiasi kikubwa cha nauli.

Mradi huo utaambatana na ujenzi wa Mahakama zingine za Wilaya tisa ambazo ni Ukelewe mkoani Mwanza, Nyasa mkoani Ruvuma, Masasi mkoani Mtwara, Biharamulo mkoani Geita, Momba mkoani Songwe, Kishapu mkoani Shinyanga, Tarime mkoani Mara, Kalambo mkoani Rukwa na Kilosa mkoani Morogoro.

Sambamba na hilo, katika mpango huo zitajengwa pia Mahakama tatu za Mwanzo ambazo ni Mgubike iliyoko Kilosa Morogoro, Nanjirinji iliyoko Lindi na Mahakama ya Mwanzo Mkuyuni iliyoko Tanga. Mahakama hizi zote zinajengwa kwa pesa za ndani ambazo ni makusanyo ya mapato ya Serikali.

Aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (kushoto) akikabidhi mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Kilosa kwa Mkandarasi Mbaraka Kihame toka Kampuni ya Kika Construction Company.

 Aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (kulia) akikabidhi mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Magubike kwa Mkandarasi Godfrey Mogellah toka kampuni ya Gopa Contractors.

Aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akiwaoneshea wananchi wa Magubike picha ya jengo la Mahakama ya Mwanzo Magubike litakavyokuwa mara baada ya kukamilika. 

Aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamaga Kabudi akizungumza na wananchi wa Kata ya Magubike wakati wa hafla ya kukabidhi mradi kwa Mkandarasi kwa ajili ya Ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Magubike.

 Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha akizungumza katika hafla hiyo.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilosa, Bi. Salome Mkinga akizungumza na wananchi wakati wa hafla hiyo.

 Mtendaji wa Mahakama ya Tanzania Kanda ya Morogoro, Bw. Ahmed Ng’eni akitoa utambulisho wa msafara wa Mahakama wakati wahafla ya kukabidhi mradi wa ujenzi wa Mahakama Wilayani Kilosa.

 

Vifaa vya ujenzi vikiwa vinawasili kwenye eneo la mradi wa Mahakama ya Mwanzo Magubike.

 Wananchi wa kata ya Magubike wakipokea kwa shangwe makabidhiano ya mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Magubike. 

Aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akinyanyua jiwe toka kwenye gari na kulitua kwenye eneo la ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Magubike kuashiria kuwa sasa shughuli za ujenzi zimeanza rasmi.

Wananchi wakishirkiana kupakua mawe kutoka kwenye gari kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama hiyo.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni