• Yakipongeza Kituo hicho kwa kuwajengea uwezo Wasuluhishi wa Ndoa ambao wamepewa jukumu hilo kwa mujibu wa sheria
Na NAOMI KITONKA, Mahakama- Temeke
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila amekipongeza Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke kwa kazi kubwa iliyofanya na inayoendelea kufanywa na Kituo hicho katika kuwahudumia wananchi wa Mkoa huo pamoja na Vitongoji vyake kwenye usuluhishi wa mashauri ya Mirathi, Ndoa, Talaka na Watoto.
Mhe. Chalamila aliyasema hayo tarehe 05 Desemba, 2024 alipokuwa akifungua mafunzo kwa wajumbe 195 wa Mabaraza ya Usuluhishi wa Ndoa yaliyofanyika katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka mitatu tangu kuanzishwa kwa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke.
“Nichukue fursa hii kuipongeza Mahakama ya Tanzania hususani Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia na Mirathi kwa kuandaa maadhimisho ya miaka mitatu ya kuanzishwa kwake, kwa hakika ni jambo la kujivunia kwa kazi kubwa iliyofanya na Kituo hiki katika kuhudumia wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam na Vitongoji vyake kwenye mashauri ya Mirathi, Ndoa, Talaka na Watoto,” alisema Mkuu wa Mkoa.
Aliongeza kuwa, “suala la usuluhishi ni muhimu sana katika kushughulikia migogoro ya familia na usuluhishi unapokosekana baina ya wanandoa husababisha madhara mbalimbali ikiwemo Wanandoa kuachana, Watoto kulelewa katika mazingira yenye migogoro na chuki, Watoto kukosa huduma muhimu kama vile ada za shule, matibabu na matunzo mengine muhimu huku baadhi ya wanandoa kuathirika kisaikolojia na kupata msongo wa mawazo na hivyo kuathiri utendaji kazi wao,” alieleza Mhe. Chalamila.
“Ni vema tukafahamu kwamba Usuluhishi ni aina mojawapo ya utatuzi wa migogoro unaohimiza wahusika katika migogoro kuzungumza na kutatua tofauti zao wao wenyewe kwa kusaidiwa na mtu wa tatu hivyo kufanya maamuzi hayo kufikiwa na wanandoa wenyewe na hivyo kuwa rahisi katika utekelezaji,” alisisitiza Mkuu wa Mkoa huyo.
Katika Kikao hicho mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwemo Mbinu na Taratibu za Usuluhishi; iliyowasilishwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mhe. Mohamed Burhan, mada nyingine ni Usuluhishi katika Mashauri ya ndoa iliyowasilishwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mhe Loveness Mwakyambiki.
Mada nyingine zilizowasilishwa katika Mafunzo hayo ni pamoja na Mbinu bora katika ujazwaji wa Fomu Na.3 iliyotolewa na Hakimu Mkazi Mahakama ya Mwanzo, Mhe. Edna Mollel na Wosia wa Mwisho, Faida na hatua za Kimahakama iliyowasilishwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya katika Kituo Jumuishi Temeke, Mhe. Simon Swai.
Akihitimisha Mafunzo hayo, Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke aliishukuru na kuipongeza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kushirikiana nao bega kwa bega katika kuandaa mafunzo hayo yenye lengo la kubadilishana uzoefu miongoni mwa Wasuluhishi na kujifunza mbinu bora za usuluhishi na kuwasaidia wananchi kupunguza migogoro kwa njia salama na kuwezesha upatikanaji wa haki kwa wakati.
“Katika kipindi cha miaka mitatu, sisi kama Kituo tumeangazia miongoni mwa changamoto wakati wa usuluhishi wa ndoa ni kutosuluhishwa kikamilifu na kutojazwa vizuri kwa Fomu Na.3 jambo hili linaweza kusababisha uamuzi wa Mashauri ya ndoa kubatilishwa na Mahakama za juu. Hivyo basi Kituo kiliona ni muhimu kendesha mafunzo haya ili kuwajengea uwezo na kuwapa mbinu bora za usuluhushi wajumbe wa Mabaraza ya Usuluhishi wa Ndoa,” alisema Mhe. Mnyukwa.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Wajumbe wa Mabaraza ya Usuluhishi wa Ndoa, Wenyeviti na Makatibu wa Mabaraza ya Usuluhishi wa Ndoa kutoka katika Kata mbalimbali za Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Viongozi wa Dini.
Mafunzo yalifungwa na Mheshimiwa John Msafiri Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Temeke.
Katika kuadhimisha miaka mitatu ya Kituo hicho, Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke kilishirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam na kufanya mafunzo hayo muhimu.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila akizungumza hivi karibuni katika Mafunzo ya Wajumbe wa Mabaraza ya Usuluhishi wa Ndoa yaliyofanyika katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.
Naibu Msajili wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Frank Moshi akizungumza katika Kikao cha Wajumbe wa Mabaraza ya Usuluhishi wa Ndoa katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.
Wajumbe pamoja na Mahakimu wakisikiliza kwa Makini hotuba iliyokuwa ikitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Ndugu Albert Chalamila (hayupo katika picha) alipokuwa akizungumza katika Kikao na Wajumbe wa Mabaraza ya Usuluhishi wa Ndoa katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.
Wajumbe wa Kikao cha Baraza wakisikiliza kwa Makini hotuba ya ufunguzi wa mafunzo iliyokuwa ikitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila (hayupo katika picha) alipokuwa akitoa hotuba ya ufunguzi wa mafunzo kwa Wajumbe wa Mabaraza ya Usuluhishi wa Ndoa yaliyofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni