Jumapili, 22 Desemba 2024

MAAFISA RASILIMALI WATU NA WATUNZA KUMBUKUMBU WATAKIWA KUWA MAKINI

NA DANIEL SICHULA- Mahakama Kuu, Mbeya

Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu  ya  Tanzania Mkoa wa Mbeya, Bw. Alintula Ngalile amewataka washiriki  wa kikao  kazi kwa maafisa rasilimali watu na watunza kumbukumbu kusikiliza kwa makini mafunzo  yatakoyofundishwa na wataalamu kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania.

Akifungua kikao kazi hicho kilichofanyika tarehe 18 Desemba,2024 katika ukumbi wa mikutano Mahakama Kuu  ya Tanzania Kanda ya Mbeya,ambacho kiliwashirikisha maafisa rasilimali watu na watunza kumbukumbu kutoka Mahakama Kuu, Mahakama ya Mkoa na Mahakama za Wilaya Mkoa wa Mbeya. 

“Naomba kila mmoja awe makini kwenye kikao kazi hiki kwani miongozo ya utunzaji kumbukumbu kila mtu alipatiwa lakini wengi wenu mmekua hamfuati miongozo hiyo na kupelekea nyaraka katika masijala zetu kuwa katika hali isiyoridhisha kwa hiyo baada ya kikako kazi hiki ni imani yangu kila mmoja wetu atatekeleza kazi ya utunzaji wa kumbukumbu kwa kufuata miongozo iliyopo.” alisema Bw. Ngalile. 

Naye mtaalamu kutoka Mahakama Kuu  ya Tanzania, ambaye ni Mtunza Kumbukumbu, Bw.Kelvin Peter Mayala aliwakumbusha washiriki  hao kuwa miongozo inayotumika katika utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka mbalimbali hasa kwa masijala za wazi na siri na kuwapa ujumbe kutoka kwa viongozi wa juu wa Mahakama kuwa wanatakiwa kutambua vifaa vyote vilivyotumika enzi za zamani katika mahakama zetu vitambulike na kuviweka katika kumbukumbu muhimu za Mahakama na kudijiti rejista zote za kesi zilizotumka miaka ya nyuma.

Wakati huohuo mtaalamu mwingine, Bi.Devotha Anatory aliwakumbusha matumizi ya mfumo wa e.office ambao ulianzisha kwa ajili ya kuondoa matumizi ya karatasi (paperless) na kuweka kumbukumbu za nyaraka za kimahakama katika hali ya usalama. 

“Kwa hiyo huu mfumo inaonekana maafisa na waheshimiwa wengi wanakwepa kuutumia, sasa hili ni wajibu wenu nyinyi maafisa rasilimali watu na watunza kumbukumbu hasa wamasijala za wazi kuacha kupokea majadala au nyaraka kama vile madokezo na barua kwa njia ya mkono, tuhimizane katika kutumia mfumo wa e-office,” alisema Bi. Devotha.

Aidha kutokana na kikao kazi hicho washiriki mbalimbali waliweza kutoa mawazo yao na changamoto katika miongozo ya utunzaji wa kumbukumbu pamoja na matumizi ya mfumo wa kielekroniki (e-office) katika utunzaji wakumbukumbu za kimahakama.

“Tunaomba mafunzo haya yawe yanafanyika mara kwa mara kwani katika utunzaji wa kumbukumbu watumishi wameajiriwa katika kada tofauti tofauti za elimu, kuna waliosoma sheria, wao inakua vigumu sana kujua miongozo ya utunzaji wa kumbukumbu lakini mafunzo kama haya yakiwa yanafanyika mara kwa mara yatakua na mchango mkubwa  katika kukumbushana wajibu wetu,” alisema mmoja wa washiriki.

Aidha Bw. Mayala aliwasisitiza washiriki wote kupendelea kutumia mifumo ya kielectroniki ya kimahakama kwenye kushughulia majalada na nyaraka mbalimbali za kimahakama na kuondokana na kutembeza majalada kwa njia ya mkono, pia kushughulikia barua pepe zilizokaa muda mrefu bila kufanyia kazi hasa kwa watumishi waliohama mahakamani kwa kushirikiana na kitengo cha Teknolojia ya Habari, Elimu na Mawasiliano( TEHAMA).

Wakati huohuo akifunga kikao kazi hicho, Kaimu Mtendaji huyo  Bw. Ngalile awashukuru watumishi waliohudhuria kikao kazi hicho na kuwataka wakafanyie kazi yote waliyofundishwa, pia aliwashukuru wataalamu kwa mafunzo waliyotoa.

Kaimu Mtendaji  wa Mahakama Kuu  ya  Tanzania Mkoa wa Mbeya, Bw. Alintula Ngalile akifungua kikao kazi kwa maafisa rasilimali watu na watunza kumbukumbu.
Mtunza Kumbukumbu kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw.Kelvin Peter Mayala akitoa ufafanuzi juu ya miongozo ya utunzaji kumbukumbu.

 Mshiriki  wa kikao kazi hicho, Bw.  Michael Mihayo akichangia na kutoa mawazo yake juu ya matumizi wa mfumo wa e-office.

Washiriki wa kikao kazi  hicho.

 Washiriki wengine.

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni