• Watumishi wengine wa Kanda hiyo waliopo katika Wilaya tano za Mkoa huo nao washiriki kwa njia ya mtandao ‘Virtual Court’
Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile amewaongoza watumishi wa Mahakama hiyo kupata mafunzo ya maadili ya watumishi yaliyofanyika tarehe 13 Desemba, 2024 katika ukumbi wa wazi wa Mahakama Kuu Kigoma.
Akizungumza wakati wa Mafunzo hayo, Afisa Maadili wa Kanda ya Magharibi Tabora, Bw. Vupalla Mbwilo alisema maadili kwa watumishi wa umma ndio roho ya utumishi, ambapo alieleza kuwa, Sheria ya Maadili kifungu cha 2 cha sheria hiyo, kimetoa tamko kwa viongozi wa umma kuhusu Rasilimali, Madeni na juu ya ujazwaji wa fomu ya maadili kwa Viongozi wa Umma.
Bw. Mbwilo alisema kuwa, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa umma ilitoa maelekezo ya namna ya kujaza fomu ya maadili kwa viongozi wa umma hasa kwa Majaji na Mahakimu kwa njia ya mtandao (online decralation) na kuwataka viongozi hao kuwasilisha nyaraka hizo kwa muda uliopangwa na Sheria ya Maadili ya Viongozi.
Hata hivyo alisisitiza kuwa, ukijaza fomu hiyo kwa njia ya mtandao (mfumo) na ikidhibitishwa kuwa wewe ni Kiongozi lazima utatumiwa ujumbe mfupi wa maneno kwa namba 15200 katika simu na itakupa maelekezo ya ujazwaji wa fomu hiyo kwa njia ya (online decralation) na kwamba kama hujapata ujumbe mfupi unaweza ukaendelea na taratibu zote za ujazwaji wa fomu na kupewa maelekezo ya namna gani utaweza pata fomu kutumia tovuti ya www.maadili.go.tz.
Aidha, aliendelea kusema kwamba kwa watumishi wasio viongozi, maadili yao yatasimamiwa na viongozi wa umma ambao wanafuata sheria na kutoa haki katika umma anaouongoza, katika hilo alitoa rai kuwa, kila mtumishi wa umma alipo aishi maadili yaliyotajwa katika Sheria ya Maadili pamoja na zile za Utumishi wa Umma.
“Mtumishi wa umma lazima ahakikishe kuwa anatenda haki kwa wananchi ama wateja wanaokuja mbele yake kutaka huduma kwa kuangalia mwenye haki na asiye na haki bila kufanya upendeleo wa aina yeyote,” alisema Afisa Maadili huyo.
Aliongeza kwa kusisitiza kuwa, watumishi wa umma lazima wawe waadilifu na ili waweze kumuhudumia mwananchi ama mteja anayekuja mahakamani kwa kumpatia haki au huduma nzuri ili kuweza kuwa na imani na Mahakama. Vilevile huduma bora kwa umma hususani wa Mahakama lazima ahakikishe kuwa anatoa huduma iliyo bora kwa mteja ama wananchi wanaokuja kufuata huduma katika eneo la kazi pamoja na kuwajibika kwa umma na kuheshimu sheria.
Kwa upande wake Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi akitoa neno kwa niaba ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, alisema kuwa mafunzo yamekuwa mazuri na yenye kujaa weledi mkubwa yatakayowawezesha kuimarisha utendaji kazi pamoja na kuleta hamasa kubwa ya kukuza maadili ya watumishi katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Aidha, aliwapongeza Sekretarieti ya Maadili kuchagua kutoa mafunzo hayo kwa watumishi wa Mahakama kwani wamepata uelewa mkubwa juu ya maadili ya mtumishi wa umma hasa wa Mahakama.
Naye, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa akitoa shukrani kwa Sekretarieti ya Maadili pamoja na watumishi wa Mahakama wa Kanda hiyo, alisema Mahakama ina mifumo wezeshi ya kuwaunganisha watumishi wote walioko Wilaya zote tano za Kanda hiyo na kwamba nao walijiunga katika mafunzo hayo kwa njia ya mfumo wa (Virtual Court).
“Elimu hii ya maadili ya viongozi na watumishi wa umma imewafikia, hivyo ushiriki wao ndio umekuwa mafanikio ya mafunzo haya, naomba niwahakikishie kuwa kuwa yote yaliyofundishwa yatakwenda kufanyiwa kazi ili kuboresha huduma zitolewazo kwa wananchi katika Mahakama zote hapa Kigoma,” alisema Mhe. Mbelwa.
Jaji Mafiwidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile (kushoto) pamoja na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi na sehemu ya watumishi wengine wa Kanda hiyo wakifuatilia mafunzo ya Maadili yaliyokuwa yakitolewa hivi karibuni na Afisa Maadili kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Magharibi Tabora (hayupo katika picha).
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa akitoa neno la utangulizi kabla ya Mafunzo ya Maadili kuanza tarehe 13 Desemba, 2024 katika ukumbi wa Mahakama ya wazi uliopo katika jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma.
Afisa Maadili wa Kanda ya Magharibi Tabora, Bw. Vupalla Mbwilo akiwasilisha mada kwa Watumishi wa Mahakama Kanda ya Kigoma kuhusu Maadili ya Viongozi na Watumishi wa Umma yaliyotolewa tarehe 13 Desemba, 2024 katika ukumbi wa Mahakama ya wazi uliopo katika jengo la Mahakama Kuu Kigoma.
Picha ya sehemu ya watumishi wa Mahakama Kanda ya Kigoma wakifuatilia mada kuhusu maadili ya watumishi wa umma iliyokuwa ikitolewa na Afisa Maadili wa Kanda ya Magharibi Tabora, Bw. Vupalla Mbwilo (hayupo katika picha).
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Aristida Tarimo akiuliza jambo kwa mtoa mada (hayupo katika picha).
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni