Ijumaa, 17 Januari 2025

JAJI KIONGOZI AHIMIZA UWEKEZAJI MIFUMO KWENYE NJIA MBADALA ZA UTATUZI WA MIGOGORO

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar-es-Salaam

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani amewahimiza wadau wa usuluhishi, ikiwemo mashirika ya kimataifa, asasi za kiraia, Wasuluhishi na jamii kwa ujumla kuendelea kuwekeza katika mifumo kwenye njia mbadala za utatuzi wa migogoro, ikiwemo usuluhishi ili kuimarisha haki na utawala bora nchini.

Mhe. Dkt. Siyani ametoa wito huo jana tarehe 16 Januari, 2025 kwenye hafla ya utoaji Tuzo kwa Wadau mbalimbali wa usuluhishi na upatanishi iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano Mlimani City, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

“Litakuwa jambo zuri kama Wadau katika mnyororo wa haki madai wataendelea kuwekeza katika maeneo mbalimbali, ikiwemo mafunzo ya Wasuluhishi, kubadilishana uzoefu, kuboresha mbinu za kisasa za usuluhishi na kuhakikisha kuwa huduma hizi zinawafikia wananchi wengi zaidi katika nchi yetu,” alisema.

Jaji Kinongozi alibainisha pia kuwa ili kujenga mfumo wa usuluhishi unganishi, ushiriki wa wadau mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Serikali, asasi za kiraia, jamii za wenyeji na Taasisi za kimataifa zinazohusika na haki za binadamu ni muhimu, huku Viongozi wa Dini na wazee wakiwa na jukumu katika kusimamia na kutoa mwongozo kuhusu njia bora za utatuzi wa migogoro.

Aidha, alieleza kuwa pamoja na Tanzania kuwa na zaidi ya Sheria 24 zinazohusu utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala, bado migogoro mingi imeendelea kuwepo mahakamani, hivyo ni wazi mifumo ya kisasa ya usuluhishi inahitaji kuangaliwa upya kwa mtazamo wa ubunifu ili kuendana na mabadiliko na mahitaji ya sasa kijamii na kiuchumi.

“Kwa kuunganisha mifumo ya jadi na kisasa tunaweza kufikia matokeo bora katika utatuzi wa migogoro, kupunguza mzigo kwa Mahakama zetu na kuhakikisha kwamba haki za binadamu zinaheshimiwa,” Mhe. Dkt. Siyani alisema kwenye hafla hiyo iliyoandaliwa na Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi kwa kushirikiana na Shirika la Misaada la Kijerumani GIZ.

Kadhalika, Jaji Kiongozi alibainisha kuwa hafla na makongamano kama hayo hutoa fursa ya kufikiri namna ya kuboresha mfumo wa haki madai na hivyo kuihakikishia jamii upatikanaji wa haki kwa wakati na gharama nafuu.

Alitumia fursa hiyo kuwaomba Wadau kuendeleza majadiliano kama hayo kwa lengo la kuthathimini mchango wa mbinu za jadi na namna zinavyoweza kuunganishwa na zile za kisasa katika utatuzi wa migogoro ili kupata mfumo bora jumuishi wa haki madai.

“Kwa kufanya hivyo, Nchi yetu inaweza kukuza mfumo wa haki madai ulio bora, shirikishi na wenye ufanisi, utakaoberesha mchakato wa upatikanaji wa haki na hivyo kuimarisha mshikamano wa kijamii, huku tukihifadhi na kuheshimu tamaduni zetu…

“Hili ni jambo bora sana hasa wakati huu tunapotengeneza Dira ya Taifa kuelekea mwaka 2050. Kila mmoja wetu anapaswa kujiuliza anapenda Tanzania ya mwaka 2050 iweje linapokuja suala la utatuzi wa migogoro na achangie maoni yake ili kuiboresha Dira ijayo ya Maendeleo ya Taifa letu,” Mhe. Dkt. Siyani alisema.

Awali akizungumza katika hafla hiyo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma alieleza kuwa migogoro katika jamii ni jambo ambalo haliwezi kuepukika, kwani katika Dunia ya leo migogoro na tofauti za kijamii zinaendelea kuongezeka katika masuala ya ardhi, ajira, familia, biashara na mengine.

“Jambo la msingi ni kuweka mifumo ambayo itawezesha kutatua migogoro hiyo. Usuluhishi ni moja ya mifumo katika kutatua migogoro, kama inavyosisitizwa chini ya Ibara ya 107A(2)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hivyo usuluhishi hauwezi kupuuzwa kwani ni njia yenye kuleta maelewano na kutafuta suluhu kwa pamoja ambazo zinaweza kuleta manufaa kwa pande zote zinazohusika katika mgogoro,” alisema.

Jaji Mfawidhi alibainisha pia kuwa usuluhishi hauwezi kuepukika katika zama hizi za mapinduzi ya viwanda ambapo mabadiliko makubwa yanaonekana katika teknolojia, uchumi na jamii ambayo inahitaji njia za haraka na nyepesi zisizo na gharama katika kushughulikia migogoro.

Alieleza kuwa ndiyo sababu kuna ongezeko na kukua kwa kasi ya matumizi ya njia za usuluhishi katika utatuzi wa migogoro duniani kote, hivyo usuluhishi katika jamii za kiafrika siyo jambo jipya, kwani ulikuwepo toka enzi za mababu karne ya 19, ukitumika katika kutatua migogoro kwa kufuata taratibu za kimira, kitamaduni na umekuwa wenye manufaa makubwa.

“Bado Viongozi katika jamii wana nafasi na mchango kubwa katika kutatua migogoro hiyo kwa amani kupitia usuluhishi. Hali hii inatuonesha kuwa usuluhishi ni njia sahihi ya kujenga madaraja badala ya kuta na kuleta umoja badala ya mgawanyiko,” Mhe. Maruma alisema.

Hafla hiyo ya utoaji Tuzo ilihudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Mahakama, Wadau wa Upatanishi, Viongozi wa Serikali na Dini, Wanasheria, Wanafunzi kutoka Shule ya Sheria kwa Vitendo na Watumishi wa Mahakama.

Jumla ya Wadau 23 walikabidhiwa Tuzo hizo, wakiwemo Majaji wa Mahakama Kuu, Mahakimu, Mawakili wa Serikali na Kujitegemea, Wapatanishi Binafsi, Mifuko ya Kijamii ya NSSSF na PSPSF, Wasomi na Watumishi kutoka Taasisi mbalimbali.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (juu na chini) akizungumza kwenye hafla ya utoaji Tuzo kwa Wadau mbalimbali wa usuluhishi.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma akifafanua jambo wakati anazungumza kwenye hafla hiyo.

Sehemu ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania (juu na chini) na Wadau mbalimbali wakifuatilia yaliyokuwa yanajiri kwenye hafla hiyo.


Naibu Wasajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania (juu na chini) na Wadau mbalimbali wakifuatilia yaliyokuwa yanajiri kwenye hafla hiyo.

Watumishi kutoka Shirika la Misaada la Kijerumani GIZ wakiwa kwenye hafla hiyo. Picha chini ni Wadau wenye usikivu hafifu wakiwa kwenye hafla ya utoaji wa Tuzo hizo. Mmoja wao naye alipata Tuzo.


Sehemu ya Wadau (juu na chini) ikiwa katika hafla hiyo.


Sehemu nyingine ya Wadau (juu na picha mbili chini) wakifuatilia kilichokuwa kinajiri.





 Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Augustina Mmbando (kushoto) akitoa utambulisho wa Viongozi na Wadau mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo. Kulia ni mtaalam wa kutafsiri alama za lugha kwa watu wenye usikivu hafifu waliokuwa kwenye hafla hiyo.

Meza Kuu inayoongozwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (katikati). Wengine kutoka kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi, Mhe. Elinaza Luvanda, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya.


Meza Kuu inayoongozwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Meza Kuu inayoongozwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na Viongozi Waandamizi wa  wa Mahakama Kuu. Picha chini ni Naibu Wasajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania.



Meza Kuu inayoongozwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na Watendaji na Afisa Utumishi wa Mahakama Kuu.

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni