Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar-es-Salaam
Mahakama Kuu ya Tanzania
Kituo cha Usuluhishi jana tarehe 16 Januari, 2025, kwa mara nyingine, imetoa Tuzo
23 kwa Wapatanishi mbalimbali baada ya kutambua mchango wao katika kukuza
matumizi ya njia mbadala za utatuzi wa migogoro, ikiwemo usuluhishi.
Hatua hiyo inalenga
kutekeleza agizo la Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma
alilolitoa katika hafla ya kwanza ya utoaji tuzo kama hizo iliyofanyika mwaka
jana 2024.
Hafla hiyo iliyofanyika
katika Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es
Salaam ilihudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Mahakama, Wadau wa Upatanishi,
Viongozi wa Serikali na Dini, Wanasheria, Wanafunzi kutoka Shule ya Sheria kwa
Vitendo na Watumishi wa Mahakama.
Jaji Kiongozi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, ambaye alikuwa Mgeni Rasmi
katika hafla hiyo, alikabidhi Tuzo hizo kwa baadhi ya Wadau wa Upatanishi,
wakiwemo Majaji wa Mahakama Kuu, Mawakili wa Serikali na Kujitegemea,
Wapatanishi Binafsi, mifuko ya Kijamii ya NSSSF na PSPSF, Wasomi na Watumishi
kutoka Taasisi mbalimbali.
Hafla hiyo iliyoandaliwa
na Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi kwa kushirikiana na Shirika la Misaada la Kijerumani
GIZ, ilipambwa na uwasilishaji wa mada inayohusu, "Kuangalia Upya Mila na
Ubunifu katika Usuluhishi ili Kuimarisha Mfumo wa Haki Madai Tanzania,"
iliyowasilishwa na Mhadhiri Mwandamizi wa Shule ya Sheria kwa Vitendo Tanzania,
Prof. Clement Mashamba.
Mada hiyo ilijadiliwa na
wasomi mbalimbali, akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Dar-es-Salaam, Mhe. Albert
Chalamila, Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria, Bw. George Mandepo,
Mtaalam wa Ushauri, Bw. Francis Gimara na Naibu Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa
Mahakama Lushoto, Bw. Goodlack Chuwa. Mwezeshaji wa mjadala huyo alikuwa Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar-es-Salaam, Mhe. Salma
Maghimbi.
Uwasilishaji wa mada hiyo
ulitanguliwa na mjadala kabambe ulioongozwa na Mhe. Maghimbi uliowahusisha
Viongozi wa Kimila, Chief Kingalu 15 Mwanabanzi 11 na Mzee Maarufu
anayesuluhisha migogoro wakati wa usiku kutoka Mtwara, Bw. Issa Mkumba,
Viongozi wa Dini, Sheikh Issa Othman Issa na Padri wa Kanisa Katoliki, Fr. Nicholaus
Masamba na Afisa Ustawi wa Jamii, Bi. Aisha Mbaruku.
Wakati wa mjadala huo,
Viongozi hao walitoa uzoefu wao na changamoto wanazokutana nazo wakati wa
upatanishi, huku Mzee Mkumba akitoboa siri kwa nini anapenda kusuluhisha
migogoro wakati wa usiku.
Kadhalika, kulifanyika katika hafla hiyo uzinduzi wa Jarida la Kituo cha Usuluhishi linalochapishwa kwa lugha mbili za Kiswahili, "Tunu ya Usuluhishi " na Kiingereza, "Treasure of Mediation," uliofanywa na Jaji Kiongozi. Jarida hilo linachapishwa mara moja kwa mwaka.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani akionesha Tuzo yake baada ya kukabidhiwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma katika hafla ya utoaji Tuzo kwa Wadau mbalimbali wa usuluhishi iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana tarehe 16 Januari, 2025.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina (kulia) akipokea Tuzo yake.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza, Mhe. Wilbert Chuma akipokea Tuzo yake.
Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Vincent Makaramba akionesha Tuzo yake baada ya kukabidhiwa.
Chief Kingalu 15 Mwanabanzi 11 kutoka mkoani Morogoro akipokea Tuzo yake.
Mzee Maarufu anayesuluhisha migogoro wakati wa usiku kutoka Mtwara, Bw. Issa Mkumba akisalimiana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma baada ya kukabidhiwa Tuzo yake, ikiwa ni mara yake ya pili.Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina (kulia) akiwa na Majaji wenzake wa Mahakama Kuu baada ya zoezi la utoaji Tuzo.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza, Mhe. Wilbert Chuma akiwa na Majaji wenzake wa Mahakama Kuu baada ya kupokea Tuzo yake.
Wadau mbalimbali wakifurahia Tuzo zao
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi akiendesha mjadala kabambe uliowahusisha Viongozi wa Kimila, Viongozi wa Dini na Afisa Ustawi wa Jamii (picha chini) na uwasilishaji wa mada inayohusu, "Kuangalia Upya Mila na Ubunifu katika Usuluhishi ili Kuimarisha Mfumo wa Haki Madai Tanzania (picha ya pili chini) wakati wa hafla hiyo ya utoaji Tuzo.
Wadau mbalimbali wakiwa katika picha ya pamoja na Meza Kuu huku wakiwa na Tuzo zao walizokabidhiwa.
Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo cha Usuluhishi wakiwa katika picha ya pamoja na Meza Kuu baada ya kufanikisha hafla ya utoaji Tuzo.
(Picha na Bakari Mtaula)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni