Na Salum Tawani - Mahakama, Dar es Salaam
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania
Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani jana tarehe 17 Januari, 2025 alishiriki
katika kikao Kazi cha Kuandaa Mkakati wa Kitaifa wa Kutambua na Kuzuia Uhalifu
nchini na kusisitiza ushirikiano katika kuzuia na kupambana na uhalifu wa aina
hiyo kwa Taasisi zote zinazohusika.
Akizungumza katika kikao hicho
kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Ofisi za Bandari jijini Dar es
Salaam, Mhe Dkt. Siyani alisema anaishukuru Tume hiyo kwa kuishirikisha
Mahakama katika kila hatua ya kuandaa mkakati huo kuanzia hatua za mwanzo na
sasa katika utekelezaji wake, kwani Mahakama imekuwa sehemu ya maboresho ambayo
Serikali inaendelea kuchukua hatua.
“Ifahamike kuwa wajibu mkubwa wa Mahakama na
jukumu lake kikatiba ni kutoa haki kwa mujibu wa Ibara ya 107 A ya Katiba ya
Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Ibara 107 B inasema katika kutimimiza
majukumu yake Mahakama itapaswa kuwa huru,” alisema Mhe. Dkt. Siyani.
Mhe. Dkt. Siyani alisema, Mahakama huwa inapata
kazi baada ya matukio ya aina hiyo kuwa yamefanyika ama kutokea, maana kazi ya
Mahakama ni kutoa haki kwa hiyo, makosa yakifanyika na wanaodhaniwa au kushukiwa
kufanya makosa wanapo bainika na kufikishwa mahakamani. Hivyo Mahakama inakuwa
na wajibu wa kupima ikiwa waliofikishwa mbele ya Mahakama wamefanya makosa hayo
kwa kuzingatia ushahidi uliowasilishwa.
Wajibu huo wa Mahakama unaweza usionekane moja
kwa moja wakati wa kazi ya kupambana na kuzuia uhalifu huo, kwahiyo unaweza
kuiona picha ya jinsi gani kazi za Mahakama zinaweza kusaidia kuzuia uhalifu wakati
tukio limeshatokea.
Vilevile, Mhe. Dkt. Siyani alisema, kwa sasa ili Mahakama isaidie kuzuia uhalifu
kuna mambo kadhaa yanapaswa yafanyike kwa mfano, imani kwa umma juu ya Mahakama
ni lazima iwe kubwa, umma ungependa kuona waliyofanaya makosa na kupatikana na
hatia wanahukumiwa kwa haraka kwa mujibu wa sheria, mambo haya mawili yakitokea
umma utakuwa na imani na Mahakama.
“Mashauri ya aina hiyo yanapochukua muda
mrefu mpaka umma ukasahau matukio yaliyotokea umma unaweza poteza imani na
Mahakama, sasa ili wahalifu waliopatikana na makosa hayo wahukumiwe kwa haraka
na kwa mujibu wa sheria. Mahakama inapaswa kushirikiana na vyombo vingine
vinavyohusika kuharakisha mchakato wa uendeshaji wa mashauri hayo ili Mahakama
yenyewe iweze kutimiza majukumu yake ipasavyo”, amesema Jaji Siyani.
Aidha, Mhe. Dkt. Siyani alisema kuwa, ili
Mahakama iweze kuzuia uhalifu ni lazima pia ilinde haki za binadamu katika
kutimiza majukumu yake bila kuathiri imani ya wananchi kwa Mahakama. Lakini pia
ili Mahakama itoe mchango wake ni lazima iwe na mifumo ya kuratibu mashauri
hayo, uzalishaji wa taarifa muhimu na ubadilishanaji wa taarifa za waalifu na uhalifu
wenyewe kati yake na Taasisi nyingine za haki jinai.
“Makosa sita yaliyoonekana kuwasilishwa kwa
wingi mahakamani kwa mwaka 2023 na 2024 ni usalama barabarani, ubakaji, madawa
ya kulevya, mauaji, uhamiaji haramu pamoja na ukatli wa kijinsia na pia kuna
matukio ya uhalifu mpya wa wizi wa kimtandao ambao umeibua mbinu mpya za kosa
la wizi, hata hivyo makosa ya zamani yanatumia mbinu mpya ni kama usafirishaji
haramu wa binadamu’’, aliongeza Mhe. Dkt. Siyani.
Kwa upande wa madawa ya kulevya na ujangili
Mhe. Dkt. Siyani alisema, wahalifu wamekuwa wakibuni njia mpya tofauti na
zamani wahalifu walikuwa wakisafirisha pembe za ndovu kama zilivyo lakini kwa
sasa wahalifu hao wana mashine za kusaga, wanasaga zile pembe vizuri na
ukikutana nao utafikiri wamebeba unga wa sembe kumbe wanasafirisha unga wa pembe
za ndovu, vilevile hata madawa ya kulevya wahalifu hawamezi kete tumboni kama ilivyozoeleka
hilo linavyoonyesha mbinu mpya zinazobuniwa kila wakati na wahalifu.
“Mahakama inatoa mafunzo katika maeneo
mapya ya kiuhalifu mfano, makosa ya kimtandao, utakatishaji wa fedha na kwenye
maeneo mengine ya uhalifu wa kijinai. Vilevile Mahakama imekuwa ikipata ushirikiano
mzuri kutoka kwa wadau, Taasisi za Serikali na Taasisi za kimataifa kwa ajili
kutoa mafunzo kwa Waheshimiwa Majaji na Mahakimu na kubadilishana uzoefu,
tunatengeneza miongozo mbalimabli ili kukabiliana na mahitaji mapya kwa mfano
muongozo wa utoaji wa adhabu wa mwaka 2023 na pia Mahakama inakamilisha
miongozo mingine ya adhabu ipatayo 59 na ndani yake ikuhusisha makosa ya wizi,
kugushi na uharibifu wa miundombinu ya reli,” alisema Jaji Siyani.
Naye, Mwenyekiti wa Kikosi kazi hicho, Prof. Sifune Ernest Mchome alisema kuwa, ni wakati sasa wa kushirikiana na kupeana taarifa zinazoashiria dalili za uhalifu ili kuweza kuzizuia zisitokee, kwa upande wa Mahakama kuna taarifa nyingi ambazo tukipeana mapema zinaweza kusaidia kuzuia uhalifu usiweze tokea na kwasababu baadhi ya mifumo inasomana ni wakati sahihi kupata tarifa hizi mapema ili kuweka mikakati iliyo bora ili kuzuia makoa ya kiuhalifu yasitokee na hivyo kupelekea jamii kuishi kwa utulivu na amani.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani akiwasilisha mada kwenye kikao Kazi cha Kuandaa Mkakati wa Kitaifa wa Kutambua na Kuzuia Uhalifu nchini kilichofanyika jana tarehe 17 Januari, 2025 Jijini Dar es Salaam.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Mustapher
Mohamed Siyani (kulia) na Msajili Mkuu wa
Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Kiaki Nkya (kushoto) wakisikiliza kwa makini hoja zilizokuwa ziktolewa katika kikao Kazi cha Kuandaa Mkakati wa Kitaifa
wa Kutambua na Kuzuia Uhalifu nchini kilichofanyika Jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya Wadau mbalimbali walishiriki katika kikao Kazi cha Kuandaa Mkakati wa Kitaifa
wa Kutambua na Kuzuia Uhalifu nchini kilichofanyika jijini Dar es Salaam wakimsikiliza kwa makini Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani
hayupo pichani wakati akitoa wasilisho lake wakati wa kikao hicho.
Mwenyekiti wa Kikosi kazi hicho Profesa Sifune Ernest Mchome (wa kwanza kushoto) akielezea jambo akiwa na wadau wengine katika kikao Kazi cha Kuandaa Mkakati wa Kitaifa wa Kutambua na Kuzuia Uhalifu nchini kilichofanyika Jijini Dar es Salaam.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu na Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Usimamizi wa Mashauri Mahakama ya Tanzania Mhe. Desderi Kamugisha akisikiliza kwa makini hoja zilizokuwa zikiwakilishwa katika kikao Kazi cha Kuandaa Mkakati wa Kitaifa wa Kutambua na Kuzuia Uhalifu nchini na kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Katibu wa Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Dkt. Jovine Bishanga.
(Picha na Tawani Salum - Mahakama.)
Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni