Jumapili, 19 Januari 2025

MBIO MIAKA 25 YA TAWJA ZAFANA ARUSHA

Ni ishara ya uzinduzi wa Maadhimisho ya miaka 25 ya Chama hicho

Ukatili wa Kijinsia wakemewa vikali

Na MARY GWERA, Mahakama-Arusha

Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) leo tarehe 19 Januari, 2025 kimefanya mbio maalum zilizohusisha Majaji, Naibu Wasajili, Mahakimu, vikundi vya riadha pamoja na Wadau mbalimbali ili kupinga vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwake.

Mbio hizo ambazo zilijumuisha umbali wa kilomita tano, 10 na 21 zilianza majira ya saa 12:30 Asubuhi kwenye viwanja vya Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) na kuongozwa na Mgeni Rasmi, Mhe. Shally Joseph Raymond, Mbunge na Mwenyekiti wa Wabunge wanawake Bunge la Tanzania na pia Mwenyekiti wa Bunge la Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ambaye amemwakilisha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson pamoja na  Mlezi wa TAWJA, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.

Akitoa salaam mara baada ya kumalizika kwa mbio hizo, Mwakilishi huyo wa Mgeni Rasmi, Mhe. Shally Joseph Raymond amesema mila gandamizi kama ndoa za utotoni, ukeketaji wa wanawake (FGM), umiliki wa ardhi, nafasi za uongozi na maamuzi bado ni vikwazo katika kufikia usawa wa kijinsia na kwamba mila na tamaduni potofu ni changamoto kubwa inayosababisha kufisha ndoto za wengi katika kujiletea maendeleo ya kweli.

“Juhudi za pamoja na mbinu mbalimbali za kujikwamua kutoka katika madhila haya zinafanyika ili kubomoa mifumo gandamizi na kuvunja minyororo iliyojikita katika jamii zetu kwa karne nyingi. Hivyo, jubilei ya TAWJA ni tukio linalostahili kusherehekewa, siyo tu kwa sababu ya umri bali dira na dhima ya Chama tangu awali, ya kuwa mshumaa  wa mwanga na matumaini, ikipigania haki za kijinsia, hususani za wanawake na watoto,” amesema Mhe. Shally. 

Ametoa rai kwa TAWJA kuwa, inapoadhimisha miaka 25 pamoja na kujivunia mafanikio ni vema pia kutafakari kwa pamoja changamoto zinazoikabili jamii kwa kuwa bado kuna mila, tamaduni na mifumo gandamizi na nyingi zikiwa zimepitwa na wakati na vilevile wanawake na watoto bado wapo nyuma katika kulinda na kuteteta haki zao za msingi.

“Ni heshima kubwa sana kwangu kusimama mbele yenu leo, kama Mgeni Rasmi, katika tukio hili adhimu lililoandaliwa na Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA). Leo, hatushiriki tu katika mbio hizi bali ni sehemu ya harakati zinazolenga kuleta mabadiliko, kuzindua uelewa na kupinga masuala ya ukatili wa kijinsia (GBV) yaliyoshamiri na kukithiri katika jamii yetu,” ameeleza.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA), Mhe. Barke Sehel amesema mbio hizo ni ishara ya kuanza kwa maadhimisho ya Jubilei ya miaka 25 ya TAWJA, pamoja na kuwashirikisha, kuhamasisha na kujenga uelewa kwa jamii na umma kuhusu hatua za kuchukua dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia (GBV) dhidi ya wanawake na Watoto.

“Ni jukumu letu sote kuhakikisha kuwa jamii ya Tanzania ina haki na inazingatia usawa kwa wote. Hivyo, tukio la leo, linathibitisha kwamba hatuko peke yetu katika kusimamia haki na usawa. Ni faraja kwangu kuona kuwa kwa pamoja tumeweza na tunaweza kuleta mabadiliko na kuhakikisha kuwa kila mwanamke na mtoto nchini Tanzania anapata haki na fursa anayostahili,” amesema Mhe. Sehel.

Mwenyekiti huyo amebainisha kuwa, TAWJA imekuwa ikijikita kwenye kukuza haki za binadamu na usawa kwa wote, hususan kwa wanawake, watoto na makundi maalum na kwamba wanapoadhimisha Jubilei ya miaka 25, TAWJA inajivunia kwa hatua kubwa ilifokia kwani imeweza kuletea mchango chanya kwenye jamii kwa upande wa haki.

Mhe. Sehel ameongeza kuwa, Chama hicho kimechangia kwenye mabadiliko ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, na kueleza kuwa, “TAWJA ilichukua juhudi za makususdi za kutoa elimu kwa wadau wa haki jinai, wabunge na jamii, kuhusu rushwa ya ngono (sextortion) na hivyo kuleta uelewa mpana katika jamii juu ya uwepo na athari ya vitendo vya rushwa ya ngono na hatimaye kubadilishwa kwa sheria kwa kuongeza kifungu maalum kuhusiana na rushwa ya ngono.”

Amesema baada yam bio hizo, wamepanga kutembela Shule za Sekondari sita, ambazo ni Ilboru, Arusha, Kimandolu, Kaloleni, Muriet na Sinoni kwa ajili ya kuanzisha Klabu za Haki za Kijinsia Mashuleni (Gender Justice Clubs) ambapo Wanachama wa TAWJA watapata fursa ya kutoa elimu kwa wanafunzi kuhusu kutambua aina zote za ukatili wa kijinsia, jinsi na wapi ya kuripoti ukatili wa kijinsia na kuwapa ujuzi muhimu wa maisha ikiwemo kuweka malengo ya kibinafsi na kujali afya na usafi wao.  

Mwenyekiti huyo ametoa shukran kwa Mahakama ya Tanzania, Mahkama ya Zanzibar, Kamati ya Maandalizi, wanachama wa TAWJA, wadau ambao ni UN Women, UNDP, WCF, PSSSF, Benki ya Equity, Jeshi la Polisi na Magereza, Hospitali ya Moyo, Vyama vya Riadha na wananchi wote waliojumuika kuungana nao na kufanikisha tukio hilo muhimu.

Mbio hizo zimebeba kaulimbiu, “Mshikamano katika Haki za Kijinsia Huanzia Hapa: “Shiriki na Elimisha.” Sambamba na hilo katika maadhimisho ya miaka 25 ya TAWJA kuna mabanda ya wadau mbalimbali likiwemo la Chama hicho ambao wanatoa elimu kuhusiana na huduma zao.

Ufunguzi wa Maadhimisho ya miaka 25 ya TAWJA unatarajiwa kufanyika kesho tarehe 20 Januari, 2025 ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango.

Picha mbalimbali zinazoonesha tukio la Mbio maalumu za uzinduzi wa Maadhimisho ya Miaka 25 ya Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) zilizofanyika leo tarehe 19 Januari, 2025 jijini Arusha.
























(Picha na MARY GWERA & SETH KAZIMOTO, Mahakama-Arusha)





 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni