Na MARY GWERA, Mahakama-Arusha
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango ametoa wito kwa wananchi, Taasisi za kitaifa na kimataifa na mashirika yasiyo ya kiserikali kushiriki katika kupigania haki na usawa wa kijinsia nchini na duniani kote.
Mhe. Dkt. Mpango ametoa rai hiyo leo tarehe 20 Januari, 2025 kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) wakati wa hafla ya ufunguzi wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA).
“Napenda kutoa wito kwa watanzania wote, pamoja na kushiriki ni vema kutoa taarifa juu ya vitendo vya ukatili wa kijinsia bila kusahau ukatili kwa watoto wa kiume ili kuwezesha taratibu za kisheria kuchukua mkondo wake,” amesema Mhe. Dkt. Mpango.
Amesema kwamba, pamoja na dhamira njema ya Serikali ya kuhakikisha usawa wa kijinsia hapa nchini, bado wanawake ambao idadi yao ni zaidi ya nusu ya watu hapa nchini, wanapewa nafasi ndogo katika umiliki wa mali na wanabaguliwa kwa msingi wa jinsia.
“Kwa mujibu wa Mpango wa Kitaifa wa Kupinga vitendo vya Kikatili dhidi ya Wanawake wa mwaka 2016, kati ya wanawake 10, wanne wamepitia ukatili wa kimwili, na mmoja kati ya watano wamepitia ukatili wa kingono maishani mwao wakiwa na umri mdogo (chini ya miaka 15). Kulingana na Ripoti ya ‘UN Women Social Institution and Gender Index (SIGI) 2022’, ukatili wa kijinsia nchini Tanzania unabainishwa zaidi kupitia ndoa za utotoni, ubaguzi ndani ya familia, ukatili dhidi ya wanawake, ukosefu wa uhuru katika kupanga uzazi, upatikanaji na umiliki wa ardhi,” amebainisha Mgeni Rasmi huyo.
Ameongeza kuwa, Taarifa ya Tathmini ya Ukatili wa Kijinsia Tanzania iliyoandaliwa na Benki ya Dunia mwaka 2022 inaonesha asilimia 40 ya wanawake wenye umri wa miaka 15 hadi 49 wamefanyiwa ukatili wa kimwili na asilimia 17 wamepitia ukatili wa kingono au kimwili na wenza wao na ndugu wa karibu.
“Kwa mujibu wa tathmini hiyo, takribani asilimia 30 ya wasichana wamepitia ukatili wa kingono kabla ya kufikia umri wa miaka 18 na wastani wa kuenea kwa ukeketaji kwa wanawake na wasichana kote nchini ni asilimia 10, vilevile, Taarifa hiyo inaeleza kuhusu jinsi jamii inavyohalalisha unyanyasaji, ambapo asilimia 58 ya wanawake na asilimia 40 ya wanaume wanaamini kuwa mume anayo haki ya kumpiga mke wake katika mazingira fulani,” ameeleza Mhe. Dkt. Mpango.
Aidha, amesema kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imejizatiti kuimarisha usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake hapa nchini kwa kuanzisha Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ambayo inasimamia masuala ya usawa wa kijinsia.
“Dhamira hiyo ya Serikali inaonekana zaidi kupitia mikakati, mipango na sera za kitaifa kama vile Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, Mipango ya Maendeleo ya Taifa ya Miaka Mitano (2011/2012–2015/2016, 2016/2017 – 2020/2021 na 2021/2022 – 2025/2026), Mkakati wa Kitaifa wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (NSGR) na Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya 2000,” amesisitiza.
Amesema, Serikali ya Tanzania chini ya Uongozi wa Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imesaini na kuridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa inayotambua na kulinda usawa wa kijinsia, imedhihirisha kwa vitendo dhamira yake ya kuboresha utendaji katika utoaji haki, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha usawa wa kijinsia katika ngazi mbalimbali za uongozi wa Mahakama.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais ameupongeza uongozi wa TAWJA, Waanzilishi pamoja na wanachama wote kwa kuadhimisha miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Chama hicho huku akitaja sehemu ya mafanikio kuwa ni pamoja na kuchangia marekebisho ya sheria, hususan Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kwa kuongeza kifungu kinachohusu rushwa ya ngono ili kudhibiti matumizi mabaya ya madaraka yanayohusisha rushwa ya ngono; kuandaa mwongozo wa Majaji na Mahakimu katika kushughulikia kesi za ukatili wa kijinsia Tanzania Bara na mengine.
Akitoa neno la utangulizi katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA), Mhe. Barke Sehel amesema katika miaka 25 wanajivunia mafanikio kadhaa ikiwemo kulea na kukuza vipaji kwa wanachama wake, Mahakimu na wadau wote wa Mahakama kwa njia mbalimbali, kuwaleta pamoja Majaji na Mahakimu wa ngazi zote kuanzia mahakama za mwanzo, Wilaya, Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mahakama Kuu, Mahakama ya Rufani na wadau wengine kwa lengo la kujifunza, kujadiliana na kubadilishana uzoefu katika kazi.
“Tunashukuru kwa mafanikio makubwa ya TAWJA ambayo yametokana na juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kujitahidi kuweka mifumo ya usawa wa kijinsia. Aidha, mafanikio haya yanatokana na ushirikiano wa karibu kutoka Mahakama ya Tanzania na Mahkama ya Zanzibar,” amesema Mhe. Sehel.
Hafla ya ufunguzi wa Maadhimisho ya Jubilei ya miaka 25 ya TAWJA imebeba kaulimbiu inayosema “Jubilei ya Miaka 25 ya TAWJA: Kusherehekea Utofauti na Mshikamano katika Usawa wa Kijinsia”. Imehudhuriwa na wageni mbalimbali wakiwemo Mlezi wa Chama hicho ambaye ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Naibu Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mhe. Jumanne Abdallah Sagini, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla, baadhi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Mkuu Mstaafu, Mhe. Mohamed Chande Othman, Mwakilishi Mkazi wa UNWOMEN, Bw. Shigeki Komatsubara, Mwakilishi Mkazi wa UNDP na wengine.
TAWJA ni Chama cha kitaaluma na kimeandikishwa chini ya Sheria ya Asasi zisizo za Kiserikali kwa namba na pia ni chama shirikishi cha Chama cha Majaji Wanawake Duniani (IAWJ). Wanachama wa TAWJA ni Majaji na Mahakimu wanawake waliopo kazini na waliostaafu katika ngazi zote za Mahakama ya Tanzania, Tanzania Bara na Visiwani. Pia, wakufunzi wa kiume wanatambuliwa kama wanachama wa heshima wa TAWJA. Mpaka sasa Chama hiki kina wanachama wapatao 500.
Picha mbalimbali za matukio za hafla ya ufunguzi wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (katikati) pamoja na Viongozi na wajumbe wa Mkutano wakiimba wimbo wa Taifa wakati wa hafla ya ufunguzi wa Maadhimishi ya Jubilei ya Miaka 25 ya Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA). Wa tatu kushoto ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, wa pili kulia ni Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla, wa tatu kulia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA), wa pili kushoto ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Jumanne Sagini na wengine.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni