Na SETH KAZIMOTO, Mahakama-Arusha
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahimu Juma amesema kuwa Mahakama ya Tanzania imepiga hatua kubwa katika suala zima la kuwa na idadi ya kutosha ya Majaji na Mahakimu wanawake ikilinganishwa na kipindi cha nyuma.
Jaji Mkuu ameyasema hayo leo tarehe 20 Januari 2025 katika hafla ya ufunguzi wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya Chama cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
“Hadi kufikia Januari 20, mwaka huu, Mahakama ya Rufani ina jumla ya Majaji wa Rufani 40. Kati ya hao, Wanaume ni 27, huku Majaji wa Rufani Wanawake wakiwa 13. Kwa upande wa Mahakama Kuu kwa kipindi hicho, kuna jumla ya Majaji 105, kati ya hao 65 ni wanaume, na 40 ni Wanawake,” amesema Mhe. Prof. Juma.
Ameeleza kuwa mwaka 1999, ambao ni mwaka mmoja kabla ya kuanzishwa TAWJA (2000), Mahakama Kuu ilikuwa na jumla ya Majaji 29 kati ya hao 26 walikuwa wanauma na wanawake walikuwa watatu pekee, ambapo aliwataja Majaji wanawake hao kuwa ni Mhe. Eusebia Munuo, Mhe.Agusta Bubeshi na Mhe. Engera Kileo.
“Mwaka 2000, wakati TAWJA inaanzishwa, Mahakama ya Rufani ilikuwa na jumla ya Majaji 8 wa Rufani, ambao wote walikuwa ni wanaume. Mahakama ya Tanzania ilihitaji kuwa na idadi ya kutosha ya Mahakimu na Majaji Wanawake ili kuwa na ufanisi na matokeo chanya katika jamii, na kwamba kumekuwa na nia thabiti ya Serikali ya Jamhuri ya Muungani wa Tanzania kuwa utayari kuendelea kuongeza idadi ya Mahakimu na Majaji,” amesema Mhe. Prof. Juma.
Aidha, Mhe. Prof. Juma amesema mwaka 2000 TAWJA ilipoanzishwa hadi Desemba 2024, Serikali iliiwezesha Tume ya Utumishi wa Mahakama (Judicial Service Commission) kuajiri jumla ya Mahakimu 1,441. Katika kipindi hicho cha miaka takriban 25, Tume ya Utumishi Mahakama iliajiri jumla ya Mahakimu Wanawake 688 na Mahakimu wanaume walikuwa 753.
Prof. Juma amesisitiza kuwa, TAWJA inaposherehekea miaka 25 ya kuendeleza nafasi ya wanawake katika mfumo wa sheria na kukuza usawa wa kijinsia, ni vema kuipongeza pia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua za makusudi za kuongeza idadi ya Majaji na Mahakimu Wanawake.
Aidha, kupitia sherehe hizo za Jubilei ya miaka 25 ya TAWJA, Jaji Mkuu amewapongeza viongozi na wanachama wa zamani na wa sasa wa TAWJA kwa kazi nzuri wanayofanya kwa kujitolea na mara nyingi kwa kutumia rasilimali fedha na muda wao. Ameongeza, “kwa miaka hii 25, huduma zenu zimesambaa na kufikia jamii, na kufikisha taswira chanya ya Mahakama kwa jamii, hususan katika masuala ya usawa wa kijinsia.”
Jaji Mkuu ameisifu TAWJA kuwa imekuwa mstari wa mbele katika kupaza sauti kutetea usawa wa kijinsia na haki, kutetea haki za wanawake, watoto na makundi maalum na kwamba uwepo wa Majaji Wanawake umesaidia kujenga mitazamo mipya na chanya kwa baadhi ya wananchi waliolelewa katika mifumo ya kijamii na kitamaduni isiyotoa nafasi sawa kwa jinsi zote.
Vilevile, amewaasa Majaji na Mahakimu Wanawake kuwa wao ni viongozi, hivyo, katika miaka 25 ijayo, wahakikishe huduma za TAWJA zinaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kuibua programu zitakazowajengea wanawake na wasichana uwezo na ushawishi kupitia sheria zitakazotungwa kutekeleza Dira hiyo.
Amesisitiza kuwa, TAWJA inao wajibu wa kuhakikisha kuwa ahadi zilizomo katika Rasimu ya Dira 2050 zinaleta mabadiliko makubwa, kama vile uzingatiaji wa suala la usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake. Pia, kupiga vita aina zote za ukatili, ikiwa ni pamoja na ukatili wa kijinsia, ukatili kwa watoto na kwa watu wenye ulemavu.
Aliongeza kwa kusema kuwa, kupitia uongozi imara unaozingatia weledi na usawa wa kijinsia, Tanzania itaweza kuandaa vijana kwa uchumi wa dunia na mapinduzi ya viwanda kwa kuweka kipaumbele katika Masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati.
Mhe. Prof. Juma ameiasa TAWJA kusaidia kubadili Mfumo wa kisheria uliopo pamoja na mila na desturi ambazo zimechangia kukosekana kwa usawa wa kijinsia, ambao kwa kiasi kikubwa unawaathiri wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika umiliki na upatikanaji wa ardhi.
Aidha, Jaji Mkuu ametoa rai kwa Majaji na Mahakimu Wanaume kuwa na utayari wa kujifunza na kujisomea wao wenyewe kwa lengo la kufahamu vikwazo vingi vilivyopo katika mifumo dume vinayowakabili wasichana na wanawake huku akihimiza kuzitambua nafuu na faida zote wanazopata kwa sababu tu wao ni wanaume na kujiuliza kwa nini wasichana au wanawake wanazikosa kwa sababu tu ya jinsia yao.
Ameongeza kuwa ni wajibu wa viongozi wa Mahakama wanaume kutoruhusu Majaji na Mahakimu Wanawake waachwe nyuma na maendeleo makubwa katika na mifumo ya kidijitali ambayo huongeza ufanisi, kuwezesha kupata ujuzi na maarifa mapya na husaidia kuwaongezea Majaji na Mahakimu Wanawake uwezo katika usimamizi.
Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango ambaye pia alikuwa mgeni rasmi akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla, Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Mhe. Mohammed Chande Othman, Naibu Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mhe. Jumanne Sagini, Majaji Wastaafu, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya, Meya wa Jiji la Arusha na wengine.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni