Na EVELINA ODEMBA – Mahakama Morogoro
Kaimu Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Steven Magoiga amesema kuwa
jumla ya wadau 45 kutoka Taasisi mbalimbali wamethibitisha kushirikiana na
Mahakama kutoa elimu ya sheria katika kipindi cha Wiki ya Sheria mkoani
Morogoro kwa mwaka 2025.
Mhe. Magoiga aliyasema
hayo jana tarehe 20 Januari, 2025 alipokuwa anazungumza na Vyombo vya Habari na
kutoa picha halisi ya namna ambavyo Mahakama imejiandaa kwenye maadhimisho hayo
yanayotegemewa kufunguliwa tarehe 25 Januari, 2025.
‘Napenda kuwajulisha
kwamba kwa mwaka huu tumeongeza kituo cha utoaji wa huduma za elimu ya sheria
katika viwanja vya standi ya treni ya mwendo kasi ya Jakaya Mrisho Kikwete
(SGR). Kituo hiki pia kitahusisha Wadau wetu wote na watoa huduma wa TRC. Hadi
sasa Wadau 45 wamethibitisha kushiriki,” alisema.
Miongoni mwa Wadau
watakaoshiriki ni Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Mawakili wa Kujitegemea, Jeshi la
Magereza, Jeshi la Polisi, Wakili Mkuu wa Serikali,TAWJA, Ustawi, Huduma za Uangalizi,
RITA, Uhamiaji, TCB, NHIF, PSSF, NMB na CRDB.
Akizungumzia kuhusu
ufunguzi, Mhe. Magoiga alisema Kanda ya Morogoro itazindua Wiki ya Sheria kwa
maandamano yatakayoanzia Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kuelekea stendi ya
zamani ya daladala iliyoko mjini Morogoro.
Alieleza kuwa katika maandamano
hayo kutakuwa na washiriki zaidi ya 1,000, wakiwemo Askali wa Jeshi la Wananchi
toka Shule ya Mafunzo na Huduma Pangawe, Askari Polisi, Askari Magereza,
Vikundi mbalimbali vya mchakamchaka (Jogging Clubs), pamoja na watumishi wa
Mahakama Kanda ya Morogoro.
Aidha, Mhe. Magoiga
aliongeza kuwa Kanda ya Morogoro pamoja na Wilaya zake ambazo ni Mvomero,
Gairo, Ulanga, Malinyi, Kilombero, wataadhimisha Wiki ya Sheria katika Wilaya
zao, hivyo aliwaomba Viongozi wa Serikali katika Wilaya hizo kutoa ushirikiano kama
ambavyo wamekuwa wakifanya kwa miaka mingine.
Wakati huo huo, Mdau
kutoka Huduma za Uangalizi Mkoa wa Morogoro, Bw. Yusuph Ponela alisema kuwa
tayari wamejipanga na wanasubiria uzinduzi ili waingie kuelimisha Wananchi
waweze kujua masuala mbalimbali yanayohusu huduma za uangalizi na namna
wanavyoshirikiana na Mahakama kuifikia dira ya Taifa ya Maendeleo kwa kusimamia
adhabu mbadala na wafungwa wanapata muda wa kutumikia vifungo vyao, huku
wakipata nafasi ya kushiriki shughuli zao za uzalishaji mali.
Naye Mdau kutoka Mamlama
ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Chacha Gotora alisema kuwa katika maadhimisho hayo
ya Wiki ya Sheria wamejipanga kutoa elimu ya sheria za kodi, kupokea changamoto
wanazopata Wananchi kulingana na sheria za kodi na watapata wasaa wa kupatiwa
ufafanuzi.
Wiki ya Sheria itahitimishwa
tarehe 1 Februari, 2025 ikifuatiwa na maadhimisho ya Siku ya Sheria tarehe 3
Februari, 2025. Matukio hayo yanaafungua shughuli za Mahakama rasmi kwa mwaka
2025 kwa kutoa dira kamili. Maadhimisho hayo yanabebwa na Kauli Mbiu inayosema,
“Tanzania ya Miaka 50: Nafasi ya Taasisi zinazosimamia Haki Madai katika Kufikia
Malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo.”
Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Stephen Magoiga akizungumza Waandishi wa Habari (hawapo pichani).
Mtendaji wa Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Bw. Ahmed Ng’eni (kulia) pamoja na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Morogoro, Mhe. Mary Kallomo, wakifuatilia hotoba ya Mhe. Magoiga kwa Vyombo vya Habari.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni