Jumamosi, 29 Machi 2025

BARAZA LA WAFANYAKAZI MAHAKAMA KUU DIVISHENI YA KAZI LAKUTANA

Na LIGHTNESS KABAJU-Mahakama, Kazi

Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi imefanya Kikao cha Baraza la Wafanyakazi jana tarehe 28 Machi, 2025 mjini Morogoro ili kujadili mambo mbalimbali yanayohusu wafanyakazi.

Kikao hicho kilifunguliwa na Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Joseph Mlyambina.

Katika kikao hicho, Katibu wa Baraza alikuwa Bw. Robert Mchocha na Katibu Msaidizi, Bw. Aloyce Lyimo, wote wakiwa Watumishi wa Mahakama Kuu kutoka Divisheni hiyo.

 Aidha, Wajumbe wengine wa Baraza la Wafanyakazi katika kikao hicho walikuwa ni Watumishi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi pamoja na wajumbe wengine kutoka Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE).

Kikao kilianza kwa kuainisha agenda zilizoandaliwa wajumbe walipata wasaa wa kujadili hoja mbalimbali zilizokusanywa na kupata mchakato unaoendelea  katika kutatua changamoto za Wafanyakazi bila kuathiri utendaji kazi mahala pa kazi.

Naye Katibu Mkuu wa TUGHE wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Michael Masubo alipokea hoja hizo zilizojadiliwa na kupitishwa na Wajumbe kwa ajili ya kuziwasilisha katika sehemu husika.

Vilevile katika kikao hicho, Mtendaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Bw. Jumanne Muna aliwasilisha na kuwapitisha Wajumbe kwenye taarifa ya utendaji kazi.

Kadhalika,Mhasibu Mkuu wa Mahakama hiyo, Bi. Joyce Mulugu aliwasilisha bajeti ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi kwa mwaka 2025/2026.


Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina-katikati-akiongoza Kikao cha Baraza hilo.


Mtendaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Bw. Jumanne Muna akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi kwenye Baraza hilo.

Wajumbe wa Baraza-juu na chini-wakifuatilia kilichokuwa kinajiri wakati wa kikao hicho.


Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni