Jumatano, 2 Aprili 2025

JAJI MFAWIDHI IRINGA AFANYA UKAGUZI WILAYANI MUFINDI

  • Awakumbusha watumishi kujiepusha na vitendo vya rushwa

Na LUSAKO MWANG’ONDA, Mahakama-Iringa

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mhe. Dustan Ndunguru amefanya ziara ya kikazi kutembelea na kukagua shughuli mbalimbali za Mahakama katika Wilaya ya Mufindi.

Mhe. Ndunguru alifanya ziara wilayani humo tarehe 28 Machi, 2025 ambapo pia alipata fursa ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo ya Mafinga Mjini.

Akizungumza na Watumishi wa Mahakama wilayani humo, Mhe. Ndunguru aliwaasa kutojihusisha na vitendo vya rushwa kwakuwa inachafua taswira nzuri ya Mahakama.

“Kwa yule ambaye atatuhumiwa  humu na kuthibitika na Mahakama kuwa ameshiriki katika vitendo vya rushwa, atachukuliwa hatua stahiki za kisheria ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi,” alisisitiza Jaji Ndunguru.

Aidha, aliwapongeza watumishi kwa kufanya kazi kwa ushirikiano na kuwasisitiza kuendelea kuwa na nidhamu kazini pamoja na kufuata maadili ya utumishi wa umma ili kuboresha utendaji kazi wa shughuli za Mahakama.

Mhe. Ndunguru alipata pia fursa ya kutembelea Gereza la Wilaya ya Mufindi liitwalo Isupilo lengo likiwa ni kubaini changamoto mbalimbali walizo nazo wafungwa gerezani hapo na kuzitolea ufumbuzi.  

Akiwa gerezani hapo, Jaji Ndunguru alisomewa taarifa ya utendaji wa Gereza hilo kutoka kwa Mkuu wa Gereza hilo SSP Rajabu Said Chitope na alipata pia wasaa wa kuzungumza na wafungwa ambao waliweza kuwasilisha kwake malalalamiko mbalimbali ambayo mengi yalipata majibu ya papo kwa papo.

Katika ziara hiyo, Mhe. Jaji Mfawidhi aliambatana na Viongozi wengine wa Mahakama akiwemo Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Bernazitha Maziku na Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Bi. Melea Richard Mkongwa.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Dustan Beda Ndunguru (katikati) akizunguzmza na watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Mufindi (hawapo katika picha) akiwa katika ziara ya kikazi aliyofanya hivi karibuni katika Wilaya hiyo. Kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Bernazitha Maziku na kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Bi. Melea Richard Mkongwa.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mufindi, Mhe. Benedict Nkomola (aliyesimama) akitoa taarifa ya utendaji wa Kituo kwa Jaji Mfawidhi, Mhe. Dunstan Ndunguru.

Sehemu ya Watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Mufindi wakimsikiliza kwa makini Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Dunstan Ndunguru (hayupo katika picha).

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa akiingia eneo la jengo la Mahakama ya Mwanzo Mafinga Mjini kukagua maendeleo ya ujenzi.

Muonekano wa jengo  la Mahakama ya Mwanzo ya Mafinga Mjini linaloendelea kujengwa. Jengo hilo lipo katika hatua za mwisho na linategemewa kukamilika hivi karibuni.

(Habari na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni