Jumatano, 2 Aprili 2025

SHUGHULIKIENI MATATIZO YA WATUMISHI YANAYOWASILISHWA MBELE YENU: JAJI RWIZILE

Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma

Jaji Mfawidhi wa  Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile amewataka Viongozi wa Mahakama wa Kanda hiyo kushughulikia matatizo ya watumishi yanayowasilishwa na kuwataka watumishi kutosubiri vikao vya Baraza la Kanda ndio wayasemee. 

Mhe. Rwizile aliyasema hayo wakati akiongoza kikao cha sita cha Baraza la Wafanyakazi wa Kanda hiyo kilichoketi tarehe 29 Machi, 2025 katika ukumbi wa Mikutano wa Mahahakama Kuu Kigoma ambapo aliwataka wajumbe wa kikao hicho kuwasilisha hoja za kisera na zile za kiutendaji ambazo zimeshindwa kupatiwa suluhu kwa muda mrefu katika maeneo yao ili kikao kiweze kuwa na tija.

“Viongozi nawasisitiza tengeni muda kutatua changamoto za kiutendaji katika maeneo yenu ili kupunguza malalamiko kwa watumishi na hakikisheni mnatoa mrejesho kwa watumishi juu ya mambo yaliyojadiliwa katika baraza hili na rejesheni majibu ya hoja zilizotoka Mkutano Mkuu ili kuwa na uelewa wa pamoja,” alisema Jaji Rwizile. 

Jaji Mfawidhi huyo aliwataka, Afisa Kazi Mfawidhi Mkoa wa Kigoma na Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) Mkoa wa Kigoma kutembelea Mahakama zote Kanda ya Kigoma kutoa elimu ya uendeshaji wa Mabaraza ya Wafanyakazi pamoja na kusikiliza kero zao ili chama cha Chama hicho kiweze kujulikana vema  ili watumishi waweze kuona  faida yake na kuendelea kujiunga.

Aidha, alitumia fursa ya Baraza hilo kuwapongeza watumishi wa Kanda hiyo kwa kufanya vizuri katika Utendaji Kazi huku akiwajuza kuwa, katika tathmini iliyofanyika Mahakama Kanda ya Kigoma iliingia katika nafasi tano bora kitaifa hivyo kuwataka Viongozi na watumishi kuendelea kufanya kazi kwa kushirikiana ili kubakia kuwa bora kitaifa katika usikilizaji wa mashauri na kiutendaji. 

Baada ya baraza hilo, Jaji Rwizile aligawa vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa jumla ya Mahakimu sita ili kurahisisha shughuli zao za kusikiliza mashauri katika vituo vyao vya Mahakama za Mwanzo.

Kwa upande wake, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Bw. Filbert Matotay alilijulisha baraza kupitia taarifa ya utendaji kazi iliyosomwa na Afisa Utumishi Mwandamizi, Bw. Festo Sanga kuwa, utekelezaji wa bajeti tarajiwa ya Mwaka 2025/2026 utazingatia vipaumbele vilivyomo katika Mpango Mkakati wa Mahakama awamu ya pili, vipaumbele vya Nchi na maagizo ya Viongozi Wakuu wa Mahakama.

Bw. Sanga alisema kuwa, lengo kuu ni kumaliza mashauri ya mlundikano na kutekeleza kwa vitendo Dira ya Mahakama ya Utoaji wa Haki Sawa kwa Wote na kwa Wakati. 

Aidha, pamoja na mambo mengine taarifa hiyo  ilionesha kuwa, jumla ya watumishi 54 wa Kada mbalimbali walipanda vyeo katika kipindi cha kuanzia mwezi Aprili 2024 hadi Machi, 2025. 

Vilevile, taarifa hiyo imeonesha maboresho mbalimbali yanayofanywa na Mahakama ya Tanzania kwa kupokea miradi mitatu ya ujenzi wa Mahakama Mwanzo tatu (Kigoma Kaskazini, Manyovu na Heru Juu) ambazo zinaendelea kujengwa. Kukamilika kwa miradi hiyo kutasogeza huduma kwa wananchi na utoaji wa haki kwa wakati. 

Naye, Afisa Kazi Mfawidhi Mkoa wa Kigoma, Bw Venance Kadago alifurahishwa na namna Viongozi wa Mahakama wanavyoshughulikia hoja  za  watumishi na kuahidi kuendelea kutoa elimu ya uendeshaji wa mabaraza na wajibu kati ya mwajiri na mwajiriwa katika maeneo ya kazi katika taasisi za umma huku akiwataka watumishi pia kutumia njia sahihi za kuwasilisha hoja na changamoto zao kwa mwajiri ili kuleta ufanisi na tija  mahala pa kazi.

Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu (TUGHE) Mkoa, Bw. Mgassa Chimola, alisema baraza la wafanyakazi ni jukwaa la kisheria la majadiliano ya pamoja kati ya viongozi na watumishi kuhusu wajibu na maslahi ya watumishi.

Bw. Chimola aliongeza kuwa, Mabaraza ya wafanyakazi ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la Mwaka 1970, Utekelezaji wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya Mwaka 2004 Kifungu 73 (1-3) kinachoelekeza juu ya kutekeleza sera ya kuwashirikisha wafanyakazi katika uongozi  wa pamoja.

Aliongeza kuwa, kukutana kwa baraza hilo ni kwa mjibu wa sheria ya majadiliano ya pamoja katika utumishi wa umma No. 19 ya Mwaka 2003, hivyo aliwapongeza wajumbe wote kushiriki na kuleta hoja kutoka kwa watumishi ili baraza liweze kujadili kwa pamoja na kuamua masuala muhimu ya kiutumishi ili kuboresha utendaji kazi kwa watumishi.

Wajumbe wa Baraza kwa pamoja waliazimia kuziwasilisha hoja za kisera zilizoshindwa kupata majibu katika baraza hilo na kuhimizana kutekeleza maazimio ya kiutendaji yaliyowasilishwa ambayo yako ndani ya uwezo wa Viongozi Kanda hiyo.

Sehemu ya wajumbe wa baraza wakiwa katika dua na sala ya ufunguzi wa baraza  hilo,dua iliyoongozwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kasulu, Mhe. Imani Batenzi, wapili(kulia) wengine ni wajumbe baraza hilo.

Sehemu ya wajumbe wa Baraza la Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma wakiwa katika dua na sala ya ufunguzi wa baraza  hilo lililofanyika tarehe 29 Machi, 2025 katika ukumbi wa Mikutano wa Mahahakama Kuu Kigoma.

Jaji Mfawidhi wa  Mahakama Kuu ya Tanzanua Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile (kulia) akikabidhi vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Nyakitonto Kasulu, Mhe. Dorothea Daudi.

Jaji Mfawidhi wa  Mahakama Kuu kanda ya kigoma Mhe. Augustine Karichuba Rwizile, akikabidhi cheti kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kibondo, Mhe. Maila Makonya kwa Mahakama yake  kuwa hodari wa kumaliza mashauri ya mlundikano kwa mwaka 2024.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa akifafanua jambo kwa wajumbe wakati wa Kikao cha Baraza la Wafanyakazi kiliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa  Mahakama Kuu Kigoma tarehe 29 Machi, 2025.

Afisa Kazi Mfawidhi Mkoa wa Kigoma, Bw. Venance Kadago akitoa ufafanuzi kwa wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la wa  Mahakama Kuu Kigoma katika kikao kilichofanyika tarehe 29 Machi, 2025.

Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu (TUGHE) Mkoa wa Kigoma,  Bw. Mgassa Chimola (aliyesimama) akisisitiza jambo alipokuwa akieleza namna TUGHE inavyofanya kazi kwa kila tawi na uratibu wa vikao vyake.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni