Jumatano, 2 Aprili 2025

WAFANYAKAZI KANDA YA IRINGA WATAKIWA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAO IPASAVYO

Na ABDALLAH SALUM, Mahakama-Njombe

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Dunstan Ndunguru ametoa rai kwa watumishi wa Kanda hiyo kuwa, wanapaswa kuwajibika ili waweze kudai haki zao za msingi.

Akizungumza kwenye mkutano wa Baraza hilo alisema Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kanda ya Iringa lililoketi tarehe 29 Machi, 2025 katika ukumbi wa wazi wa Mahakama  ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Ndunguru alisema, “siyo unadai haki wakati wewe mwenyewe mtumishi hauwajibiki katika utendaji kazi wako.”

Mhe. Ndunguru alitoa mfano wa kuwasilisha cheti baada kumaliza masomo ya kujiendeleza ili upandishwe lakini unakuwa haujawasilisha cheti hivyo, hauwezi kupata haki ya kupandishwa cheo wala mshahara hali ambayo inasababisha kushindwa kudai haki husika.

Jaji Ndunguru alihimiza Chama cha Wafanyakazi (TUGHE) kishirikiane na menejimenti ya Mahakama kanda ya Iringa na Mkoa wa Njombe kutoa elimu mara kwa mara kwa watumishi juu ya umuhimu wa kujiunga na Chama hicho pamoja na ushirikishwaji wa uamuzi mbalimbali wa utendaji kazi.

Jaji Mfawidhi alijibu hoja mbalimbali za watumishi ambazo ziliwasilishwa mbele yake, zingine zilijibiwa palepale na nyingine zitapelekwa kwenye Mkutano wa Baraza Kuu la Kitaifa la Mahakama.

Naye, Mtendaji wa Mahakama Kuu kanda ya Iringa, Bi. Melea Mkongwa aliwasisitiza watumishi  juu ya umuhimu wa kuchangia na kujiunga na Chama Cha Wafanyakazi pamoja na elimu kutolewa hasa kwa watumishi wapya kwa kuwa Mahakama kila mwaka kuna watumishi wanaostaafu na vilevile kuna watumishi wapya.

Katika Baraza hilo ziliwasilishwa taarifa za utekelezaji wa shughuli za Mahakama Kuu Kanda ya Iringa pamoja na Mkoa wa Njombe kwa kipindi cha kuanzia Julai 2024 hadi Machi, 2025 ambazo ziliwasilishwa kwa kila Wilaya zilizopo ndani ya Kanda ya Iringa.

Vilevile, Katibu wa TUGHE, Bw. Kuguru Retabuka alichangia hoja mbalimbali za watumishi kuhusu stahiki za wafanyakazi pamoja na kutoa neno la shukrani kwa ushiriki wa mkutano huo na kutoa ahadi juu ya kuwapa elimu watumishi juu ya umuhimu wa kujiunga na Chama hicho.

Katika Mkutano huo alichaguliwa mfanyakazi bora wa Kanda kwa kushindanishwa na mtumishi mmoja wa Mkoa wa Iringa na mwingine kutoka Mkoa wa Njombe kwa kupigiwa kura ambaye mtumishi huyo ataenda kuiwakilisha Mahakama Kanda ya Iringa kwa kushindanishwa na Mahakama za Kanda nyingine  ili kupata mtumishi bora wa Taasisi.

Kwa Kanda ya Iringa alishinda mtumishi kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe aitwaye Ramadhani Hassani Saidi.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Dunstan Ndunguru (katikati) akiongoza Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Kanda hiyo. Kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi, Mhe. Barnaba Mwangi na kushoto ni Katibu wa Baraza la Wafanyakazi Iringa, Bi. Amina Zuberi.

Mtendaji wa Mahakama Kuu kanda ya Iringa, Bi. Melea Mkongwa aliyeshika karatasi pamoja na sehemu ya wajumbe wengine walioshiriki katika mkutano wa Baraza la wafanyakazi wa Mahakama Kanda ya Iringa uliofanyika mkoani Njombe.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Dunstan Ndunguru (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watumishi wa Mahakama Kanda ya Iringa mara baada ya Kikao cha Baraza la Kanda hiyo kilichofanyika tarehe 29 Machi, 2025. 


Picha ya juu na chini ni  wajumbe waliokuwepo kwenye Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi uliofanyika katika ukumbi wa wazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe wakifuatilia kwa makini kinachoendelea kwenye mkutano huo.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma) 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni