Alhamisi, 3 Aprili 2025

MENEJIMENTI YA MAHAKAMA KANDA YA SUMBAWANGA YAKUTANA

Na Fredrick Mahava – Mahakama, Sumbawanga

Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga jana tarehe 02 Aprili, 2025 imekutana na kufanya kikao cha robo ya tatu ya mwaka ambacho kimefanyika katika ukumbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga.

Akifungua kikao hicho Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga Mhe. Fredrick Manyanda ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa kikao hicho alisema vikao hivyo ni muhimu sana na vimekuwa vikifanya kila robo ya mwaka na kutoa fursa ya kujadili mambo mbalimbali ya kiutendaji kama vile shughuli mama ya uendeshaji wa mashauri.

Naye, Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga Bw. Machumu E. Essaba aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Mahakama katika Kanda hiyo kwa kipindi cha kuanzia Julai 2024 hadi Machi 2025. Katika taarifa hiyo ambayo ilikuwa imegawanyika katika sehemu mbili iliainisha masuala ya kiutawala na masuala ya uendeshaji mashauri.

Kwa upande wa masuala ya utawala, Bw. Essaba alisema kuwa, utekelezaji wa mambo mbalimbali ya kiutawala kama vile utekelezaji wa bajeti kwa mwaka 2024/2025, masuala ya kushughulikia madeni, masuala ya watumishi, majengo na viwanja vya Mahakama, miradi ya ujenzi inayoendelea, vitendea kazi, uwekaji wa taarifa kwenye mfumo wa Mahakama wa ramani (JMap) na ukusanyaji wa maduhuri kwa mwaka fedha 2024/2025.

Vilevile, kwa upande wa masuala ya mashauri Bw. Essaba alitoa takwimu za mashauri yaliyofunguliwa, mashauri yaliyoamuliwa, mashauri yanayosubili kusikilizwa na mashauri ya mlundikano yaliyopo katika kila ngazi ya Mahakama yani kuanzia Mahakama Kuu hadi Mahakama za mwanzo na mikakati ya namna ya kuyashughulikia.

Aidha, Mtendaji huyo, alielezea mafanikio yaliyopatikana kwa kipindi cha kuanzia Julai 2024 hadi Machi 2025 ambayo ni kuwezesha kufanyika kwa vikao vya Mahakama Kuu, kupunguza mlundikano wa mashauri, kuanzisha kitabu cha utendaji kazi wa mwaka, kupata hati za kiwanja cha Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga na nyumba ya Jaji (Judges lodges), kuwawezesha watumishi mbalimbali kuhudhuria mafunzo ya muda mfupi na mrefu.

Pamoja na hayo, Mtendaji huyo alisema kuwa, kwenye mafanikio changamoto pia mbalimbali zinazoikabiri Mahakama Kanda ya Sumbawanga ambapo kubwa ni ufinyu wa bajeti za kuendeshea mashauri, ufinyu wa bajeti ya matengenezo ya magari, ufinyu wa bajeti ya kutosheleza stahiki na maslahi ya watumishi na pia uhaba wa vitendea kazi.

Naye, Jaji Mfawidhi ambaye alikuwa ni mwenyekiti wa kikao hicho aliruhusu wajumbe wa kikao hicho kutoa maoni, ushauri, mapendekezo kuhusu ajenda mbalimbali zilizojadiliwa wakati wa kikao hicho kwani baadhi ya changamoto zilizowasilishwa zipo ndani ya uwezo zikitafakariwa zinaweza kupata suluhisho.

Wajumbe waliohudhuria kikao hicho cha menejimenti ambao ni viongozi kutoka mikoa ya Rukwa na Katavi walitoa maoni, ushauri kuhusu masuala mbalimbali yaliyowasilishwa kwenye kikao na kuahidi kwenda kutekeleza yote yaliopitishwa na kikao hicho.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga Mhe. Fredrick Manyanda akifungua kikao cha menimenti. 

Wajumbe wa kikao cha menejimenti Kanda ya Sumbawanga wakisikiliza taarifa inayotolewa wakati wa kikao 

Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga Bw. Machumu E. Essaba akitoa taarifa ya utekelezaji kwa kipindi cha kuanzia Julai 2024 hadi Machi 2025.

Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha-Mahakama)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni