Alhamisi, 3 Aprili 2025

BARAZA LA WAFANYAKAZI MAHAKAMA KANDA YA SUMBAWANGA LAKUTANA

Na Fredrick Mahava- Mahakama, Sumbawanga

Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kanda ya Sumbawanga linalojuisha mikoa ya Sumbawanga na Katavi lilikutana jana tarehe 02 Aprili, 2025 na kujadili mambo mbalimbali yanayohusu watumishi hasa ushirikishwaji katika utoaji wa maamuzi, baraza hilo lilifanyika katika Ukumbi wa Mahakama uliopo katika Jengo la Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga.

Akizungumza wakati wa kufungua Baraza hilo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga Mhe. Frederick Kapela Manyanda ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa kikao hicho alisema, utaratibu wa kuwa na mabaraza unalenga kukuza uwazi na ushirikishwaji katika maamuzi mbalimbali.

Aidha, Mhe. Manyanda alihimiza  menejimenti  ya Mahakama Kanda ya Sumbawanga na Chama cha wafanyakazi (TUGHE) kushirikiana   kwa pamoja  katika kutatua kero mbalimbali za watumishi  ili kuongeza morali ya watumishi ambao ni wachache na wanafanya kazi nyingi.

Vilevile, wakati wa kikao hicho cha Baraza kulikuwa na uwasilishwaji wa mapitio ya bajeti  ya  mwaka wa fedha 2025/2026 ambayo kwa upande wa mkoa wa Katavi iliwasilishwa na Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi Bw. Epaphras A.Tenganamba na kwa upande wa Mkoa wa Rukwa  iliwasilishwa na Afisa bajeti wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga BiT. Irene T. Mlangwa.

Naye, Katibu TUGHE mkoa wa Rukwa Bw. Amin R. Msambwa aliomba kutekelezwa kwa vikao viwili vya Baraza la wafanyakazi kama sheria inavyoelekeza ambapo kikao cha kwanza kijadili mambo ya bajeti na kikao cha pili kijadili utekekelezaji wa bajeti na pia utekelezaji wa hoja za kiutumishi zilizoibuliwa kwenye mabaraza yaliyopita

Wakati wa Baraza hilo wajumbe walijadili masuala mbalimbali ikiwemo mapitio ya Bajeti, ukomo wa bajeti, utekelezaji wa bajeti, changamoto za utekelezaji wa bajeti, kupokea na kujadili hoja za watumishi na pia majibu na ufafanuzi ulitolewa na viongozi mbalimbali.

Wajumbe waliohudhuria Baraza hilo kwa pamoja walikubaliana na kuweka mikakati ya pamoja ya kutekeleza wa shughuli mbalimbali ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi na pia kuboresha baadhi ya mambo wakati wa Baraza lijalo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga Mhe. Frederick Kapela Manyanda akiongoza kikao cha Baraza la wafanyakazi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga.

Mjumbe wa Baraza Bw. Jacob A. Mwakajengele akichangia hoja wakati wa kikao cha baraza la wafanyakazi Mahakama Kanda ya Sumbawanga.

Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga Bw. Machumu E. Essaba akichangia hoja wakati wa kikao cha baraza la wafanyakazi kilichofanyika Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga

Katibu wa TUGHE mkoa wa Rukwa Bw. Amin R. Msambwa akichangia hoja wakati wa kikao cha baraza la wafanyakazi Mahakama kuu Kanda ya Sumbawanga

Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi Bw. Epaphras A.Tenganamba akiwasilisha mapitio ya bajeti ya mwaka 2025/2026 kwa mkoa wa Katavi.

Afisa Bajeti wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbwanga Bi Irene T. Mlangwa akiwasilisha mapitio ya bajeti ya mwaka 2025/2026 kwa mkoa wa Rukwa

 

Sehemu ya Wajumbe wa Baraza la wafanyakazi Mahakama kuu Kanda ya Sumbwanga wakisikiliza

(Habari Hii Imehariri na Innocent Kansha-Mahakama) 



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni