Alhamisi, 3 Aprili 2025

RAIS SAMIA KUZINDUA JENGO LA MAKAO MAKUU YA MAHAKAMA YA TANZANIA APRILI TANO

Jengo la Tume ya Utumishi wa Mahakama na Nyumba za Makazi ya Majaji nayo kuzinduliwa

Mtendaji Mkuu aishukuru Serikali kwa maboresho ya miundombinu ya majengo ya Mahakama

Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma

Jengo la kwanza kwa ukubwa kwa upande wa majengo ya Makao Makuu ya Mahakama barani Afrika na la Sita duniani linatarajiwa kuzinduliwa rasmi tarehe 05 Aprili, 2025 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo tarehe 03 Aprili, 2025 kwenye ukumbi wa mikutano uliopo katika Jengo hilo lililopo jijini Dodoma, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amesema kuwa, uzinduzi wa jengo hilo lililogharimu jumla ya shilingi bilioni 129.7 za Kitanzania utakwenda sambamba na uzinduzi wa Jengo la Makao Makuu ya Tume ya Utumishi wa Mahakama na Nyumba za Makazi ya Majaji.

“Dhima ya Mkutano wetu huu pamoja nanyi leo ni kuwajuza mambo kadhaa kuhusiana na uzinduzi wa majengo yetu hapa Makao Makuu ya Nchi na Serikali ambayo Siku ya Jumamosi tarehe 05 Aprili, 2025, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atayazindua rasmi na kuanza kutumika katika utekelezaji wa jukumu kuu la Mahakama ya Tanzania kwa Wananchi, yaani utoaji haki sawa na kwa wakati,” amesema Prof. Ole Gabriel. 

Mtendaji Mkuu amesema kuwa, Jengo la Makao Makuu ya Mahakama litakalozinduliwa siku hiyo kwa miaka 104 sasa tangu kuanza kwa Mahakama Kuu nchini ndilo jengo la kwanza rasmi la Makao Makuu ya Mahakama tangu kuandikwa kwa historia ya Mahakama nchini. Awali jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na la Mahakama ya Rufani ndiyo yalitumika kama Makao Makuu. 

Akizungumzia sifa za jengo hilo lenye sakafu tisa na muundo wa nyota, Prof. Ole Gabriel amesema kwamba, limejumuisha mbawa (wings) tatu ambazo ni pamoja na sehemu ya Mahakama ya Upeo (Supreme Court) licha ya kuwa kwa sasa hakuna ngazi ya Mahakama hiyo hapa nchini ila imewekwa ikitokea Mahakama hiyo imeanzishwa kuwe na Ofisi za Mahakama hiyo, vilevile lina sehemu ya Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu na katikati ya jengo hilo kuna sehemu ya Utawala. 

Prof. Ole Gabriel amesema, Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania lina hadhi ya kuwa Makao Makuu ya Mhimili kwakuwa linaendana na gharama zilizotumika (Value for Money) na kwamba Jengo hilo limewekewa vifaa vyote muhimu na mifumo mbalimbali ya kuwezesha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ikiwa ni pamoja na kuwekewa ofisi na maeneo ambayo wametengewa wadau muhimu wa Mahakama ambao wako katika mnyororo wa utoaji haki. 

Kadhalika amesema kuwa, ndani ya jengo hilo kuna Chumba maalum cha kutolea taarifa mbalimbali za Mahakama (Judiciary Situation Room), eneo la Kituo cha Huduma kwa Mteja ambapo wateja wa Nchi nzima wanaweza kupiga simu ndani ya saa 24 kuelezea mahitaji yao na ama kuridhika kwao kwa huduma za Kimahakama. 

Ameongeza kuwa, jengo hilo limejengwa kwenye eneo la ukubwa wa hekta 18.9, takribani hekari 45, ambalo pamoja na vitu mengine, kutakuwa na viwanja vya michezo ya aina mbalimbali ambavyo vitajengwa kwenye eneo hili. 

Mtendaji Mkuu amesema kuwa, uwepo wa jengo hilo utawawezesha Wananchi wanaotafuta huduma za Mihimili yote mitatu ya dola kuipata katika Jiji la Dodoma na hivyo kuwapunguzia muda na gharama za kufuata huduma hizo mahali pengine.

Aidha, Mtendaji Mkuu ameeleza kuwa, kwa upande wa Mradi wa Jengo la Tume ya Utumishi wa Mahakama utakaozinduliwa pia umegharimu jumla ya shilingi bilioni 14.3 na Nyumba za Makazi ya Majaji zimegharimu kiasi cha shilingi za Kitanzania bilioni 42.3.

Aidha, Prof. Ole Gabriel ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya majengo ya Mahakama ikiwemo ujenzi na ukarabati wa Mahakama za Mwanzo, Wilaya na Mahakama Kuu lengo likiwa ni kusogeza karibu huduma ya utoaji haki kwa wananchi.

Hafla ya uzinduzi wa Majengo tajwa itafanyika katika viwanja vya Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania Barabara ya 9 ya Mahakama iliyopo Mtaa wa Tambukareli kuanzia saa moja asubuhi na inatarajiwa kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Mahakama na Serikali, Watumishi wa Mahakama pamoja na wageni waalikwa wengine.


Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel Akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo katika picha) leo tarehe 03 Aprili, 2025 kwenye ukumbi wa mikutano wa Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania.

Baadhi ya Viongozi wa Mahakama ya Tanzania walioshiriki katika Mkutano kati ya Mtendaji Mkuu na Waandishi wa Habari uliofanyika leo tarehe 03 Aprili, 2025. Wa kwanza kushoto ni Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa, wa pili kushoto ni Mkurugenzi wa Mipango na Uratibu Mahakama ya Tanzania, Bw. Erasmus Uisso, katikati ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Bi. Beatrice Patrick, wa pili dulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Kuu, Mhe. Mwajabu Mvungi na wa kwanza kulia ni Katibu wa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Meja Majuto Mdenya.


Waandishi wa Habari walioshiriki katika Mkutano huo.

(Picha na INNOCENT KANSHA, Mahakama-Dodoma)















Hakuna maoni:

Chapisha Maoni