- Ahimiza ujenzi wa Mahakama za Mwanzo tano kukamilika haraka
- Amtaka Mkandarasi kufanya kazi usiku na mchana
Na
MWANDISHI WETU-Mahakama, Dar es Salaam
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi amemtaka Mkandarasi wa Ujenzi wa
majengo ya Mahakama za Mwanzo
tano zilizopo katika Kanda hiyo, Deep
Construction Ltd kufanya kazi
usiku na mchana ili kukamilisha mradi huo kwa wakati.
Mhe. Maghibi alieleza akiwa kwenye zira
yake ya ukaguzi wa shughuli za usimamizi wa Mahakama na Magereza kwa robo mwaka
ya Jan hadi Machi 2025 kuwa ujenzi wa
Mahakama za Mwanzo Msata, Kimanzichana
na Bungu Mkoa wa Pwani na Mbagala na Somangila Mkoa wa Dar es Salaam upo nyuma na unatakiwa kukamilika ifikapo mwezi Mei,
2025.
Awali, akiwa katika mradi wa Mahakama ya
Mwanzo Mbagala jijini
Dar es Salaam, Jaji Maghimbi alipokea
taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo mitano kutoka kwa Msanifu Majenzi, Bw.Henry Mwoleka ambaye ni Mwakilishi wa Mtaalamu Mshauri wa
miradi hiyo kutoka Kampuni ya Jaji Norman&Dawbarn (T)Ltd.
Taarifa
hiyo ilionesha kuwa miradi hiyo ilitakiwa kuwa imekamilika ifikapo mwezi Februari, 2025 lakini kutokana na sababu
mbalimbali kubwa ikiwamo
Mkandarasi kutotimiza wajibu wake kikamilifu, imesababisha kuwa nyuma ya ratiba, jambo lililosababisha muda wa ujenzi kuongezwa.
Alisema kwamba Mkandarasi ameweza kukamilisha
katika miradi yote ujenzi wa msingi tu (Sub structure) sawa na asilimia 15, sasa ameanza ujenzi
wa kuta unaotarajiwa kukamilika ndani ya wiki mbili.
Kufuatia
taarifa hiyo na ukaguzi uliofanyika katika miradi yote kati ya tarehe 25-27
Machi,2025, Mhe Maghimbi hakufurahia kasi iliyopo ya ujenzi na pia hali
isiyoridhisha ya vifaa vya kufanyia kazi kama matofali,saruji,nondo na mchanga
hivyo, kumtaka Mkandarasi
kufanya kazi usiku na mchana.
“Nimekagua
miradi yote mitano na kukuta kasi ya ujenzi siyo ya kuridhisha ikilinganishwa
na muda uliobaki wa kutekeleza mradi huu. Namtaka Mkandarasi kuongeza kasi kwa kufanya
kazi usiku na mchana ili kukamilisha miradi hiyo ifikapo mwezi Mei,2025.
Namtaka pia kuongeza
wafanyakazi wataalamu na vibarua, kuongeza matofali, saruji, nondo, mchanga na vifaa muhimu hitajiwa
haraka.Nitarudi tena kukagua hata kwa ratiba isiyo rasmi” a,lisema Jaji Maghimbi.
Kwa
upande mwingine, Jaji Maghimbi alimtaka Mtaalamu Mshauri Kampuni ya Norman&Dawbarn (T) Ltd kutimiza wajibu waliopewa wa
kusimamia kwa karibu miradi hiyo ili
ikamilike kwa wakati. Alikumbusha umuhimu wa miradi hiyo kwa Mahakama hususani maeneo ya Mbagala
ambako imelazimika kukodi nyumba ya mtu binfsi ili kuendeshea mashauri wakati wakisubiri ujenzi kukamilika.
Mhe
Maghimbi alikagua pia shughuli za usimamizi wa Mahakama za Mwanzo Bungu, Kimanzichana, Mbagala , Msata, Mwambao Ikerege pamoja na Gereza la Wazo Hill ambako
alihimiza matumizi sahihi ya mfumo wa usajili wa mashauri upitia Programu tumizi ya Mahakama za
Mwanzo.
Kadhalika, alihimiza uzingatiaji wa
taratibu za uendeshaji wa mashauri katika Mahakama za Mwanzo, miongozo
mbalimbali ya usimamaizi wa Mahakama na kuondoa mlundikano wa mashauri na Mahabusu
magerezeni,
hususani wanaotokana na mashauri ya Mahakama za Mwanzo.
Katika
ziara hiyo, Jaji
Maghimbi aliongozana na Viongozi
wengine, akiwepo Naibu Msajili Mfawidhi Kanda
ya Dar es Salaam, Mhe Mary Moyo na Mtendaji wa
Mahakama, Bw.Moses Mashaka.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi akiwa kwenye ukaguzi Msata-juu na chini.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi akiwa kwenye ukaguzi Bungu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni