Alhamisi, 3 Aprili 2025

MANYARA YAFANYA KIKAO CHA BARAZA LA WAFANYAKAZI

Na Christopher Msagati- Mahakama, Manyara

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara Mhe. John Kahyoza leo tarehe 03 Aprili, 2025 amewaongoza watumishi wa Mahakama Kanda hiyo, kufanya kikao cha Baraza la wafanyakazi cha Mwaka 2025, kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa Wazi wa Mahakama Kuu Manyara.

Akifungua kikao hicho Mhe. Kahyoza aliwaambia watumishi kuwa Mabaraza hayo ni muhimu sana kwa watumishi kutoa maoni yao kuhusu nini kinatakiwa kifanyike katika kuboresha mazingira ya mahala pa kazi. “Kimsingi huwa tunakutana katika mabaraza haya mara chache katika mwaka, hivyo ninawasihi watumishi msiwe na wasiwasi katika kutoa mawazo yenu ili tuweze kuyafanyia kazi kwa yale tunayoyaweza hapa, yale ambayo yatapaswa kufikishwa katika Baraza la Taifa litakalofanyika Dodoma siku za hivi karibuni,” alisema Mhe. Kahyoza.

Akizungumza na wajumbe katika kuchangia hoja ya Bajeti ya matumizi ya Mwaka wa fedha 2025/2026, Mhe. Kahyoza alisisitiza kuwa Mabaraza ya Wafanyakazi ni muhimu sana kwa ajili ya kuangalia matumizi ya fedha ya Bajeti ya mwaka wa fedha unaokuja. “Ni muhimu sana kuhudhuria vikao hivi kwa sababu pia wajumbe tunapata kujadiliana juu ya matumizi ya Bajeti katika mwaka wa fedha ujao, hivyo ninawaasa kushirikiana kwa dhati katika maandalizi ya Bajeti kwa sababu bajeti hizi ndizo zinazofanya majukumu yetu ya Mahakama yatekelezeke,” alisema Mhe. Kahyoza.

Akisoma hoja za watumishi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara Kiongozi wa TUGHE Tawi la Mahakama Manyara Bw. Shadrack Aron amesema kuwa miongoni mwa hoja zilizotolewa na watumishi wa Mahakama ni pamoja na kupatiwa mafunzo ya mara kwa mara kwa ajili ya kuongeza motisha kwa watumishi ili wawezesha kuendana na mabadiliko ya matumizi ya TEHAMA ambayo yanajitokeza kwa sasa.

Akizungumza katika kikao hicho Katibu wa TUGHE Mkoa wa Manyara Bw. Tamson Mshighati aliwashauri wajumbe wa kikao hicho wajitahidi kujenga hoja zao vizuri ili zitakapopelekwa katika Kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Taifa ziweze kujibiwa vizuri na viongozi. “Nawashauri mjenge hoja zenu na mawazo yenu vizuri ili zipate kueleweka vema kwa waajiri ambao tunaamini kuwa watayafanyia kazi na mtapata majibu mazuri,” alisema Bw. Mshighati.

Watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara wameweza kushiriki katika kikao hicho cha kujadili masuala mbalimbali ya kiutumishi ikiwa ni maandalizi ya Kikao kitakachofanyika Dodoma mnamo tarehe 10 Aprili, 2025.

Kwa upande wake, Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Bi. Nyanzobe Hemedi alizitolea ufafanuzi baadhi ya hoja ambazo zinaweza kutatulika ndani ya Kanda na kuahidi kuwasilisha hoja ambazo zingepaswa kuwasilishwa Makao Makuu.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe. John Kahyoza (wa kwanza kulia) akifungua Kikao cha Baraza la Wafanyakazi kwa Watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara kilichofanyika leo tarehe 03 Aprili, 2025 katika ukumbi wa Wazi wa Mahakama Kuu Manyara. Aliyekaa upande wa kushoto ni Katibu wa Kikao Bw. Sylivanus Rwegumisa.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe. John Kahyoza (aliyekaa katikati) akifuatilia Kikao cha Baraza la Wafanyakazi kwa Watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara 

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara, Mhe. Bernard Mpepo (aliyeketi katikati) akifuatilia Kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Mahakama Kuu Kanda hiyo,  kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara Mhe. Mariam Lusewa na kushoto ni Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kiteto Mhe. Mossy Sasi.


Sehemu ya wajumbe wa Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara wakiimba wimbo wa “Solidarity Forever” wakati wa Kikao.

Afisa Utumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara Bi. Glory Makuru akichangia mada katika kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Mahakama Kuu Kanda ya Manyara.


Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Mbulu Mhe Vitus Kapugi akichangia mada katika kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Mahakama Kuu Kanda ya Manyara.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha-Mahakama)






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni