Na AHMED MBILINYI – Mahakama, Bukoba
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba, Mhe. Immakulata Banzi hivi karibuni aliongoza Kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Kanda ili kujadili mambo mbalimbali ya kiutendaji na utumishi.
Kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Mahakama Kuu Bukoba, kilihudhuriwa pia na Viongozi Waandamizi wa Mahakama hiyo, akiwemo, Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Mhe. Saidi Mkasiwa, Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Bukoba Bw. Lothan Simkoko, na wajumbe kutoka wilaya zote za Mkoa wa Kagera.
Baada ya kufungua Kikao hicho, Mhe. Banzi aliwakaribisha wajumbe kuimba wimbo maarufu wa wafanyakazi wa ‘solidarity forever’ na baadaye kufanya utambulisho wa wajumbe na kumruhusu Katibu wa Baraza hilo, Bi. Febronia Serapion kusoma agenda.
Akiwakaribisha wajumbe katika Kikao hicho, Mhe. Banzi aliwaomba kuwa huru kuchangia na kutoa maoni mazuri yatakayosaidia Baraza hilo kufikia maazimio yatakayowasaidia siyo tu watumishi wa mahakama kanda ya Bukoba, bali pia wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania kwa ujumla.
“Niwashukuru wajumbe kwa kuhudhuria kwenye Kikao cha Baraza hili. Ushiriki wenu ni muhimu kwani michango ya mawazo mtakayotoa itasaidia kufikia maazimio yenye tija yatakayopelekwa kwenye Baraza Kuu siyo kwa manufaa yetu sisi bali pia watumishi wa Mahakama kwa ujumla,” alisema.
Katika Baraza hilo, wajumbe walijadili masuala mbalimbali yakiwemo mapitio ya Bajeti, ukomo wa bajeti, utekelezaji wa bajeti, changamoto za utekelezaji wa bajeti, kupokea na kujadili hoja za watumishi na pia majibu na ufafanuzi ulitolewa na viongozi mbalimbali.
Kadhalika Mhe. Banzi alisisitiza kwa watumishi wote kuendelea kufanya kazi kwa bidii, uadilifu, ushirikiano kwa watumishi na wadau wa mahakama, na kuwakumbusha kujiendeleza kielimu katika taaluma zao pamoja na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Katika Kikao hicho kilichohudhuriwa piya na Katibu wa TUGHE wa Mkoa wa Kagera, Bw. Edward Mwashitanda aliyeelezea faida za kutumia mabaraza ya wafanyakazi katika kutatua changamoto za watumishi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba, Mhe. Immaculata Banzi (katikati) akiongoza Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Kanda hiyo. (Kulia) ni Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi, Bw. Lucas Mwilu na (kushoto) ni Katibu wa Baraza la Wafanyakazi Bukoba, Bi. Febronia Serapion.

Kaimu Afisa Bajeti wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba, Bw. Rojas Rwanyumba akiwasilisha Taarifa ya Bajeti ya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba, 2024 /2025.
Katibu wa Tughe Mkoa wa Kagera, Bw. Edward Mwashitanda mwenye suti nyeusi akiwa katika Baraza la Wafanyakazi Kanda ya Bukoba (kulia) ni Afisa Tawala Mwandamizi Mahakama ya Wilaya Bukoba, Bi. Luciana Lucas.
Picha ya juu na chini ni wajumbe waliokuwepo kwenye mkutano wa Baraza la Wafanyakazi uliofanyika katika ukumbi wa wazi wa Mahakama Kuu Bukoba wakifuatilia kwa makini kinachoendelea kwenye mkutano huo.
(Habari hii imehaririwa na MAGRETH KINABO, Mahakama, Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni