Jumamosi, 5 Aprili 2025

JAJI MKUU AMWAGIA SIFA KEMKEM RAIS DKT. SAMIA

 Na INNOCENT KANSHA- Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mchango wake mkubwa wa kufanikisha maboresho yaliyotekelezwa na yanayoendelea kutekelezwa na Mahakama ya Tanzania kwa kuongeza idadi ya Majaji, Mahakimu na ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma ya haki kwa wananchi.

Ameyasema hayo, leo tarehe 05 Aprili, 2025 jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa kihistoria wa majengo matatu ya Mahakama likiwemo jengo la Makao Makuu ya Mahakama, jengo la Tume ya Utumishi wa Mahakama na Majengo ya makazi ya Majaji.

Mhe. Prof. Juma amenukuu hotuba ya Mhe. Dkt. Samia ya kwanza alipolihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mara ya kwanza mara baada ya kuapishwa kwake kuwa Rais, alisema "tutaenzi na kuendeleza mambo yote mazuri lakini pia tutafanya mabadiliko pale inapobidi kwa lengo la kukuza ufanisi na tija katika kazi,".

Aidha, Mhe. Prof. Juma ameongeza kuwa, Mahakama ya Tanzania ni wanufaika wakubwa sana wa hiyo sehemu ya hotuba ya Mhe. Dkt. Samia kwa sababu Mahakama imeshuhudia mapinduzi makubwa ya kuuwezesha Muhimili kutimiza ndoto ya miaka takribani 100 ya uwepo wa Mahakama nchini Tanzania.

Vilevile, Mhe. Prof. Juma amesema kuwa, Mhe. Dkt. Samia aliahidi kwamba, "tutashirikiana na Mhimili wa Mahakama katika kuimarisha mifumo ya utoaji haki ikiwemo kuendeleza kujenga miundombinu ya Mahakama na tumeshudia katika kipindi cha miaka minne Mahakama imejenga sana nchi nzima majengo ya kisasa ya kutolea huduma za haki kwa wakati kwa wananchi,".

“Kuongeza idadi ya Majaji na Mahakimu tumeona Rais akifanya hivyo, kukuza matumizi ya TEHAMA ambayo Mhe. Dkt. Samia umejionea mwenyewe wakati wa ukaguzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama, namna ambavyo Mahakama inatumia TEHAMA, na pia wakati ukiwa kwenye chumba maalum cha taarifa za kimahakama (Situation Room) na ulielezwa na wataalum wetu kwamba, katika chumba hicho teknolojia hiyo Mahakama ilikwenda kujifunza nchini Kazakhstan na ambao wao pia watakuja kujifunza kwetu kwa sababu katika zama hizi za teknolojia kila mmoja anajaribu kumshinda mwenzake,” amesisitiza Mhe. Prof. Juma.

Mhe. Prof. Juma amechukua wasaha huo kumshukuru sana Mhe. Dkt. Samia kwa hotuba yako "uliyoitoa Bungeni ilinisaidia sana, ilinipa nguvu na kuweza kwenda kuweka jiwe la msingi la jengo hili ambalo umelizindua leo. Hii simulizi imethibitisha kwamba Mhe. Dkt. Samia amejitoa kwa kiasi kikubwa kuhakikisha Mahakama inatimiza Dira yake ya Utoaji Haki sawa kwa wote na kwa wakati,".  

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia mamia ya watanzania wakati wa hafla ya uzinduzi wa Majengo ya Mahakama iliyofanyika leo tarehe 05 Aprili, 2025 katika viwanja vya jengo la Makao Makuu ya Mahakama mtaa wa tambuka reli jijini Dodoma

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akitoa hotuba wakati wa hafla ya uzinduzi wa majengo ya Mahakama leo tarehe 5 Aprili, 2025 jijini Dodoma

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel akitoa historia ya ujenzi wa majengo ya Mahakama wakati wa hafla ya uzinduzi wa Majengo hayo iliyofanyika leo tarehe 05 Aprili, 2025 katika viwanja vya jengo la Makao Makuu ya Mahakama mtaa wa tambuka reli jijini Dodoma


















Sehemu ya Majaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania wakifuatilia hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa uzinduzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

(Picha na Innocent Kansha -Mahakama)

    


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni