Jumamosi, 5 Aprili 2025

HISTORIA MPYA YAANDIKWA TANZANIA

  • Mhimili wa Mahakama wapata Makao Makuu mapya
  • Rais Samia azindua jengo kubwa la kisasa Dodoma
  • Jengo hilo la sita duniani, la kwanza Afrika

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 5 Aprili, 2025 ameandika historia mpya Tanzania baada ya kuzindua jengo jipya la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini hapa.

Hatua hiyo inaufanya Mhimili huo wa Dola kuwa na Makao Makuu mapya ambayo, hapo awali yalikuwa katika jiji la kibiashara, Dar es Salaam. Jengo hilo lenye ukubwa wa mita za mraba 63,244, kwa majengo ya Makao Makuu ya Mahakama, ni la sita duniani na la kwanza Afrika.

Jengo la Makao Makuu ya Mahakama lililogharimu kiasi cha bilioni 129.7 za Kitanzania lina jumla ya vyumba vya ofisi 510 vyenye samani za kisasa, vyumba vya Mahakama za wazi 10, ukumbi mkubwa wa mikutano wenye uwezo wa kuchukua watu 346 na kumbi ndogo 22 za mikutano.

Sherehe za uzinduzi wa jengo hilo lililopo katika eneo la Tambuka Reli, zilianza saa 2.30 asubuhi na kuhudhuriwa na Viongozi wa Serikali, Bunge, Mahakama, Watumishi, Wastaafu na Wananchi kutoka maeneo mbalimbali katika jiji la Dodoma, ambalo ni Makao Makuu ya Tanzania.

Katika sherehe hiyo, Rais Samia pia alizindua Nyumba za Makazi ya Majaji zilizopo katika eneo la Iyumbu, pembezoni mwa barabara inayoelekea Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), ambazo zimegharimu kiasi cha bilioni 42.3 za Kitanzania.

Kadhalika, Mkuu wa Nchi alizindua Jengo la Makao Makuu ya Tume ya Utumishi wa Mahakama, lililopo pembezoni mwa Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, ambalo limegharimu kiasi cha bilioni 14.3 za Kitanzania.

Rais Samia aliwasili katika eneo la sherehe hiyo majira ya saa 5.00 hivi asubuhi na kupokelewa na wenyeji wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani.

Wakati wa mapokezi hayo, walikuwepo pia Viongozi wengine wa Mahakama, wakiwemo Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya.

Viongozi wengine ni Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule na wengine wengi.

Baada ya kuwasili katika viunga vya Makao Makuu mapya ya Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Samia alielekea kwenye eneo maalum lililokuwa limeandaliwa kwa ajili ya kupanda mti wa kumbukumbu.

Viongozi wengine waliopanda miti wakati huo ni Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani.

Baada ya tukio hilo, Mhe. Prof. Juma alimwongoza Rais Samia kwenye eneo la uzinduzi ambapo alipata maelezo mafupi kuhusu miradi mitatu ya majengo ambayo yamezinduliwa, yaani Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, Nyumba za Makazi ya Majaji na Jengo la Tume ya Utumishi wa Mahakama.

Rais Samia, baada ya kupata maelezo hayo, alifunua kitambaa maalum kwenye jiwe la uzinduzi wa Jengo la Makao Makuu kama ishara ya uzinduzi rasmi wa majengo hayo matatu na baadaye kukata utepe.

Zoezi hilo lilimwezesha Rais Samia kuingia ndani na kuanza kulitembelea rasmi jengo hilo la Makao Makuu ya Mahakama lenye sakafu tisa na mbawa tatu, yaani Mahakama ya Juu/Upeo (Supreme Court), Mahakama ya Rufani (Court of Appeal) na Mahakama Kuu, ambazo katikati zinaunda eneo la Ofisi za Utawala.

Rais Samia alianza kutembelea Chumba kikubwa cha kisasa cha wazi cha kuendeshea mashauri ambacho kimefungwa vifaa bora vya teknolojia na mifumo ya kisasa, ikiwemo ule wa kusikiliza mashauri kupitia Mkutano Mtandao na ule wa Tafsiri na Unukuzi unaowawezesha Majaji na Mahakimu kuendesha mashauri bila kuandika mwenendo kwa mkono.

Baadaye, Rais Samia aliongozwa kwenye Chumba Maalum cha Mifumo ya Kutolea Taarifa za Kimahakama (Judiciary Situation Room) kinachowawezesha Viongozi wa Mahakama kujua kila kitu kwa wakati mmoja kinachofanyika katika Mahakama zote nchini.

Mhe. Dkt. Samia pia alitembelea Chumba cha Huduma kwa Mteja (Customer Service Center), ambacho kina Watumishi wanaofanya kazi kwa masaa 24 kupokea mrejesho, yaani malalamiko, pongezi na changamoto mbalimbali zinazohusu huduma za utoaji haki kwa ujumla kutoka kwa Wananchi.

Kadhalika, Mhe. Dkt. Samia aliongozwa kwenye Ofisi ya Jaji Mkuu na kujionea kumbukumbu kadhaa ikiwemo picha za Majaji Wakuu ambao wamehudumu kabla na baada ya uhuru hadi sasa. Akiwa ndani ya ofisi hiyo, Rais Samia alifanya mazungumzo mafupi na Jaji Mkuu.

Baada ya kutembelea maeneo hayo, Rais Samia alielekea kwenye eneo maalum lililokuwa limeandaliwa kwa ajili ya kukabidhi funguo baada ya kuzindua na kutembelea jengo hilo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania.

Rais Samia alikabidhi funguo tatu kwa Jaji Mkuu wa Tanzania, moja wa Makao Makuu ya Mahakama, mwingine wa Makazi ya Majaji na tatu wa Jengo la Makao Makuu ya Tume ya Utumishi wa Mahakama, tukio lililopokelewa kwa shangwe, nderemo na vifijo na Wananchi waliokuwa wamefurika kuzidi uwezo wa eneo lililokuwa limeandaliwa kwa ajili ya sherehe hiyo.

Baada ya zoezi hili lililoongozwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Samia, akiwa ameongozana na Wenyeji wake, alielekea Jukwaa Kuu kabla ya Bendi ya Jeshi la Polisi kuwaongoza Watanzani kuimba na Wimbo wa Taifa na ule wa Afrika Mashariki kwenye sherehe iliyokuwa inarushwa mubashara na vyombo mbalimbali vya Habari ya Kimataifa na Kitaifa, ikiwemo mtandao wa Mahakama ya Tanzania.

Muda mchache baada ya Rais Samia kukaa kwenye nafasi yake, Muongozaji wa Sherehe hiyo, Bw.  Shaban Kisu, ambaye alishirikiana kwa karibu na Mzee Peter Mavunde pamoja na Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mashauri wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Desdery Kamugisha, aliendelea na ratiba nyingine, ikiwemo kutoa nafasi kwa Viongozi mbalimbali kuzungumza na Taifa.

Sherehe hizo zimepambwa na burudani kutoka vikundi mbalimbali, ikiwemo Kwaya ya Mahakama ya Tanzania, maarufu kama Ng’aring’ari, Kwaya ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kwaya ya Utumishi wa Umma. Kulikuwa pia na vikundi vya ngoma vya Kibati kutoka jijini Dodoma na Nyota kutoka Zanzibar.  


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan-kushoto-akimkabidhi ufunguo wa Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwenye sherehe ya uzinduzi wa Majengo Matatu ya Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, Nyumba za Makazi za Majaji na Jengo la Tume ya Utumishi wa Mahakama.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan-kushoto-akikabidhi ufunguo wa Nyumba za Makazi ya Majaji.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan-kushoto-akikabidhi ufunguo wa Jengo la Makao Makuu ya Tume ya Utumishi wa Mahakama.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan-katikati-akijiandaa kukata utepe kama ishara ya uzinduzi wa Majengo ya Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, Makazi ya Majaji na Tume ya Utumishi wa Mahakama, huku Viongozi wengine wakishuhudia. Picha chini akikata utepe huo.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan-wa pili kulia- akifungua kitambaa maalum kuashiria uzinduzi wa majengo hayo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan-juu na chini- akipata maelezo mafupi kuhusu miradi ya ujenzi wa majengo hayo kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel.


Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Kalege Enock akitoa maelezo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan namna Chumba Maalum cha Mifumo ya Kutolea Taarifa mbalimbali za Mahakama kinavyofanya kazi. Picha chini akipata maelezo kwenye Chumba cha Huduma kwa Mteja.




Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiongozwa na Viongozi wa Mahakama ya Tanzania kuelekea kwenye Ofisi ya Jaji Mkuu wa Tanzania. Picha chini akiingia kwenye eneo la Ofisi hiyo.



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akisaini kitabu cha wageni akiwa kwenye Ofisi ya Jaji Mkuu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa ndani ya Ofisi ya Jaji Mkuu.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akimwonyesha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan moja ya picha ya majengo ya Mahakama ya zamani yaliyotumiwa na Majaji.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan-kushoto- akiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimwagilia mti wa kumbukumbu kufuatia uzinduzi wa Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akimwagilia mti wa kumbukumbu kufuatia uzinduzi wa Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.


Kikundi cha Ngoma cha Kibati kutoka Zanzibar kikitumbuiza kwenye uzinduzi huo huku Viongozi na wageni mbalimbali wakimiminika kuwatunza.

Kwaya ya Mahakama ya Tanzania, maarufu Ng'aring'ari kikikonga mioyo ya Viongozi na wageni mbalimbali waliohudhuria uzinduzi huo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwaaga Wananchi baada ya kuhitimishwa kwa sherehe ya uzinduzi huo.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni